Kesi ya kiongozi wa Shincheonji yazua mjadala uhuru wa dini Korea Kusini
Muktasari:
- Kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Kanisa la Shincheonji la Yesu, Lee Man-hee, imeibua mjadala kuhusu uhuru wa dini na utawala wa sheria nchini Korea Kusini, huku wadau wakitofautiana kuhusu hatua ya kumfungulia mashtaka na kumweka rumande.
Seoul, Korea Kusini. Kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Kanisa la Shincheonji la Yesu, Lee Man-hee (95), imeibua mjadala kuhusu uhuru wa dini na mwenendo wa mfumo wa sheria nchini Korea Kusini, huku wadau wakihoji namna mamlaka zinavyoshughulikia suala hilo.
Lee alikamatwa Juni 24, 2026 na kufunguliwa rasmi mashtaka Juni 30 kwa tuhuma za kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa, akidaiwa kuratibu usajili wa takribani waumini 50,000 wa kanisa hilo kujiunga na Chama cha People Power Party (PPP) kwa lengo la kushawishi uchaguzi wa ndani wa chama hicho.
Siku hiyo hiyo ya kufunguliwa mashtaka, Waziri wa Sheria wa Korea Kusini, Jeong Seong-ho, aliandika katika mitandao ya kijamii kuwa adhabu kali ya jinai dhidi ya Lee "haiwezi kuepukika," akihitimisha ujumbe wake kwa kunukuu Mathayo 7:15 unaohusu "manabii wa uongo."
Kauli hiyo imezua ukosoaji kutoka kwa mwanasosholojia wa dini wa Italia, Dk Massimo Introvigne, ambaye kupitia makala zake katika jarida la Bitter Winter amesema matamshi hayo yanaweza kutafsiriwa kama kutoa hukumu kabla ya mahakama kusikiliza na kuamua shauri hilo.
Dk Introvigne pia amepinga hatua ya kumweka rumande Lee mwenye umri wa miaka 95, akisema hatua hiyo haiendani na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu, hasa kwa kuwa kesi inayomkabili haihusiani na tuhuma za vurugu au uhalifu mkubwa.
Kwa upande wake, Kanisa la Shincheonji la Yesu limesema lilishirikiana kikamilifu na uchunguzi uliofanywa na mamlaka na kusisitiza kuwa hakuna mwanachama aliyelazimishwa kujiunga na chama chochote cha siasa, kinyume na madai ya waendesha mashtaka.
Kwa mujibu wa Dk Introvigne, hoja kuu ya kesi hiyo ni kubaini iwapo wanachama wa kanisa hilo walijiunga na chama cha siasa kwa hiari au walishinikizwa kufanya hivyo. Amesema kila raia ana haki ya kushiriki shughuli za kisiasa bila kubaguliwa kutokana na imani yake ya dini.
Amesema namna kesi hiyo itakavyosikilizwa na kuamuliwa itakuwa kipimo cha jinsi Korea Kusini inavyolinda uhuru wa dini, haki ya kupata usikilizwaji wa haki na misingi ya utawala wa sheria.