Prime
Kivumbi ubunge, udiwani kutua INEC
Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) leo imepuliza kipenga cha uchukuaji na urejeshaji fomu za uteuzi kwa nafasi za ubunge na udiwani, huku vyama kadhaa vikibaki katika hatua za mwisho za kukamilisha michakato ya ndani ya kuwapata wagombea.
Kwa mujibu wa ratiba ya INEC, hatua hiyo inaanza leo Agosti 14 hadi 27, 2025, ikitanguliwa na uchukuaji wa fomu za wanaoomba urais na makamu wa rais, ulioanza Agosti 9 mwaka huu.
Uteuzi kwa nafasi zote hizo utafanyika Agosti 27 na kuanzia Agosti 28 hadi Oktoba 28, 2025 kutakuwa na kampeni za uchaguzi mkuu, kabla ya upigaji kura Jumatano, Oktoba 29.
Hata hivyo, licha ya pazia kufunguliwa, chama pekee kilichokamilisha mchakato wa ndani wa uteuzi hadi jana ni CUF pekee.
Chama tawala CCM kipo katika hatua za mwisho kukamilisha uteuzi huo wa wagombea wa udiwani, huku wale wa ubunge wakitarajiwa kuteuliwa Agosti 22, mwaka huu kwa mujibu wa ratiba yake huku baadhi ya mikoa ikianza kutangaza wagombea wa udiwani.
Mkoani Dodoma, jumla ya wagombea 208 kati ya 209 wa nafasi ya udiwani waliopata ushindi kwenye kura za maoni, wamepitishwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM mkoa kugombea nafasi hiyo.
Mgombea mmoja wa Kata ya Ihumwa jijini Dodoma ameondolewa kwenye orodha hiyo na nafasi yake kupewa aliyeshika nafasi ya pili, kutokana na sababu za kimaadili.
Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni msimamizi wa uchaguzi wa chama hicho kwa ngazi hiyo, Jawadu Mohammed, amesema uamuzi huo umechukuliwa ili kuendana na matakwa ya wanachama na kanuni za chama.
“Mkoa wa Dodoma una jumla ya kata 209 na wagombea wote walioongoza kwenye kura za maoni wamepitishwa na Halmashauri Kuu ya mkoa, isipokuwa Kata ya Ihumwa. Huyu jina lake halijarudi na nafasi yake amepewa aliyeshika nafasi ya pili kwa sababu za kimaadili, kikanuni na kutokana na maoni ya watu wengi, hapaswi kukiwakilisha chama kugombea nafasi hiyo,” amesema Jawadu.
Katika Mkoa wa Mbeya, nako CCM imekamilisha uteuzi wa wagombea wa udiwani, huku wale walioongoza katika kura za maoni wakiwa ndiyo walioteuliwa na Halmashauri Kuu ya chama hicho mkoa.
Taarifa za ndani zilizopatikana jana Agosti 13 zimeeleza kuwa kikao hicho kilipendekeza majina ya walioshinda kura za maoni wapewe nafasi kuendelea na hatua nyingine.
Imeelezwa kuwa kwa sasa madiwani hao wanatarajia kuanza kuchukua fomu leo na kupewa ratiba rasmi ya kuanza kampeni kwa mujibu wa taratibu za INEC.
Baadhi ya wagombea hao wamesema wanachosubiri ni barua kutoka kwa viongozi wa Wilaya au Kata kwa maelekezo zaidi.
Alipotafutwa Katibu wa chama hicho mkoani humo, Lengael Akyoo, amesema kwa sasa yuko nje ya ofisi na hana nyaraka yoyote.
“Kwa sasa siko ofisini, niko nje ya mji kwa majukumu kidogo na hapa nilipo sina documents (nyaraka) yoyote,” amesema Akyoo.
Kwa upande wa Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Elias Mpanda, amesema vikao vya mchujo wa kura za maoni kwa nafasi za udiwani vimekamilika.
“Kujua nani ameteuliwa kwa kila kata, itajulikana kesho kutwa (Agosti 15), baada ya majina kuwekwa hadharani kulingana na tulivyokubaliana,” amesema Mpanda.
Amewasihi makada wa chama hicho kuwa na subira kwani kila mmoja atajua nani ameteuliwa kugombea nafasi hiyo katika eneo lake.
Wakati akieleza hivyo, Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Omary Mtuwa, amesema majina ya walioteuliwa kwenye mchujo wa mwisho kwa nafasi ya udiwani yalitarajiwa kutangazwa usiku wa Agosti 13, baada ya kumaliza vikao vya ngazi ya mkoa.
“Uhakika wa kutangaza majina ya walioteuliwa katika mchujo wa mwisho ni kuanzia usiku wa leo, baada ya kukamilisha vikao kwa kila kata, na tutatoa utaratibu wa kuanza kuchukua fomu za kugombea,” amesema Mtuwa.
Kwa upande wa watia nia wa ubunge, CCM inatarajiwa kuwatangaza Agosti 22, mwaka huu, baada ya vikao vya uongozi wa chama hicho.
Mbali na CCM, Chama cha ACT Wazalendo nacho, hakijakamilisha mchakato huo kikiwa katika hatua ya kura za maoni.
Hali iko hivyo hata kwa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), ambacho hadi sasa kimeteua wagombea urais na makamu wa rais pekee, huku uteuzi wa wagombea wa udiwani na ubunge ukitarajiwa kuanza Agosti 16.
CUF kuanza kesho
Baada ya kukamilisha mchakato wake wa ndani, CUF imesema watiania wake wataanza kuchukua fomu za INEC kuanzia leo.
Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa CUF, Mohamed Ngulangwa amesema chama hicho kilishapata watiania wa nafasi hizo muda mrefu kabla ya mkutano mkuu uliowapitisha wagombea urais.
“Watiania wa CUF wapo tayari kuchukua fomu kesho (leo), kama unavyofahamu mchakato huu unachukua siku 14, kwa hiyo kadri siku zinavyosonga mbele watakuwa wanachukua fomu,” amesema.
Mwenyekiti wa Chama cha ADC, Shabaan Itutu amesema bado wanaendelea na mchakato wa kuwapata wagombea kupitia kura za maoni zinazofanyika katika mikoa mbalimbali.
“Hatuna ukomo sisi, bali ukomo wetu ni tarehe ya mwisho ya INEC ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu za uteuzi,” alieleza.
Vivyo hivyo, ndivyo ilivyo kwa Chama cha DP ambacho pia hakijakamilisha mchakato huo. Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdul Mluya amesema mchakato wa kuwapata watiania wa udiwani na ubunge utakoma hadi INEC watakapofunga dirisha la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za uteuzi.
“Kwa nini tufunge mlango sasa hivi? Tunataka kuwapa watu fursa ya ili kushiriki uchaguzi mkuu. Unaweza ukakatwa chama fulani, ukaja kwetu tukakupokea, sasa kwa nini tuhimitimishe mapema mchakato wa kuwapata watiania wa udiwani na ubunge?” amehoji.
Katibu Mkuu wa Chama cha United Democratic Party (UDP), Swaum Rashid amesema wameamua kusogeza muda mbele wa kura za maoni ili kutoa fursa zaidi kwa Watanzania kushiriki uchaguzi.
ACT kamili Zanzibar
Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu ameiambia Mwananchi mchakato wa kura za maoni kwa upande wa Zanzibar umekamilika katika majimbo yote 50.
Katika majimbo 222 ya Tanzania Bara, Ado amesema tayari mchakato umeshaanza katika majimbo na ukishakamilika watajadiliwa kwenye vikao vya juu hivi karibuni.
Katika hatua nyingine, Kiongozi mstaafu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ameibuka kidedea katika mchakato wa kura za maoni katika Jimbo la Kigoma Mjini.
Zitto ambaye ni mjumbe wa kamati kuu ya ACT Wazalendo, alipata kura 228 dhidi ya 37 alizozipata Abdul Nondo ambaye ni mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya chama hicho. Jumla ya kura zilizopigwa zilikuwa 269 kati ya hizo, nne ziliharibika.
Alipotafutwa aeleze hali ilivyo katika majimbo mengine, Katibu wa Idara ya Oganaizesheni wa ACT Wazalendo, Shaweji Mketo alisema kwa sasa yupo ‘bize’ kusimamia chaguzi zinazoendelea katika majimbo hayo.
“Naomba nikupigie baadaye nitakupa matokeo yote, bado tunaendelea kuyachakata hapa,” amesema Mketo.
Chaumma
Vivyo hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa Umma wa Chama cha Ukombozi wa Umma, (Chaumma), John Mrema amesema mchakato wa uchukuaji na urejeshaji fomu kwa ubunge na udiwani ndani ya chama hicho unaendelea.
“Agosti 15, 2025 ni mwisho wa kuomba kuteuliwa kwa nafasi ya ubunge na udiwani, kuanzia Agosti 16 kamati za utendaji za mikoa zitaketi kuchakata na kuandaa taarifa za wagombea na kutoa mapendekezo kwa sekretarieti ya Taifa,” amesema Mrema.