Kukosekana mikataba ya kazi, kilio kwa wafanyakazi wa majumbani
Wafanyakazi wa majumbani nchini wamelalamikia kutotolewa mikataba ya maandishi licha ya kufanya kazi kwa saa nyingi kupita kiwango kilichowekwa kisheria.
Wengi wao wamekuwa wakinyimwa haki zao za msingi kutokana na kufanya kazi kwa kutegemea makubaliano ya mdomo ambayo hayana uthibitisho wowote.
Wakati wafanyakazi hao wakilalamikia hayo Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004 inaeleza wazi kuwa mfanyakazi anayefanya kazi zaidi ya saa 45 kwa wiki anapaswa kuwa na mkataba wa maandishi pamoja na malipo ya ziada. Ingawa waajiri wengi hawatekelezi wajibu huo.
Malalamiko hayo yametolewa na viongozi 25 wa elimu rika wa wafanyakazi wa nyumbani kutoka mikoa sita nchini, katika warsha ya mafunzo iliyoratibiwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO), Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu (OHCHR), Serikali pamoja na Chama cha Wafanyakazi wa Majumbani, Hifadhi, Hotelini, Huduma za Jamii na Ushauri (Chodawu). Wamesisitiza kuwa kutokuwepo kwa mikataba kumeendelea kuwa chanzo kikuu cha unyonyaji na migogoro isiyoisha kati ya waajiri na wafanyakazi.
Desdelia Simon, mfanyakazi wa nyumbani na Mwenyekiti wa wafanyakazi wa nyumbani Mkoa wa Morogoro, amesema mkataba wa maandishi ni nyenzo muhimu inayoweka bayana haki na wajibu wa pande zote. Amesema wafanyakazi wengi wamekuwa wakikosa mishahara yao kwa wakati, kunyimwa likizo kama wafanyakazi wengine, kukumbana na unyanyasaji wa kijinsia na hata kufukuzwa bila taarifa kwa sababu hawana nyaraka za kuwasilisha wanapodai haki zao.
Amesema waajiri wengi hukwepa mikataba wakidhani itawadhalilisha, ilihali ukweli ni kwamba mkataba unawalinda wote wawili na kupunguza migogoro inayoweza kutokea katika ajira.
Jenifer Mtanga kutoka Dodoma ametoa ushuhuda kuwa mkataba wa maandishi aliopewa na mwajiri wake mpya umebadilisha kabisa utendaji wake wa kazi. Baada ya kupata mwajiri anayefuata taratibu za Chodawu, sasa analipwa Sh150,000 kwa mwezi, anapata likizo, muda wa kupumzika na ruhusa za kuhudhuria mafunzo, tofauti na hapo awali alipofukuzwa bila sababu na kunyimwa mshahara wake.
Mkuu wa Idara ya sheria kutoka Chodawu, Asteria Gerald amesema mkataba ni msingi wa majadiliano, kwani huonyesha makubaliano ya malipo, muda wa kazi na masharti ya ajira. Amesema kukosekana kwa mkataba kunasababisha kipaumbele kutolewa kwa kauli ya mfanyakazi katika maamuzi ya mgogoro.
Ofisa kutoka Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Herman Komba amesema sheria inaeleza wazi kuwa mwajiri anapaswa kumpa mfanyakazi mkataba wa maandishi. Endapo mwajiri atashindwa kufanya hivyo, taarifa atakayotoa mfanyakazi kuhusu mshahara au masharti ya kazi ndiyo yatatumika kwenye maamuzi ya kimamlaka.