Malipo ya kidijitali yazidi kushika kasi Tanzania
Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Stanbic Bank Tanzania, Emmanuel Mahodanga (kushoto), na Meneja Mkazi wa Visa Tanzania, Victor Makere (kulia), wakimkabidhi zawadi Ofisa wa Kitengo cha Wateja Maalum wa Stanbic Bank, Leila Lembariti, kwa kutambua mchango wake katika kampeni ya kuhamasisha matumizi ya kadi badala ya fedha taslimu (XB Campaign). Hafla ya utoaji wa tuzo hizo ilifanyika jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Uanzishaji wa matumizi ya kadi uliongezeka kwa asilimia 3,082 kwa idadi ya miamala na asilimia 449 kwa thamani, jambo linaloashiria kuongezeka kwa matumizi ya huduma za malipo ya kidijitali.
Dar es Salaam. Matumizi ya malipo ya kidijitali nchini yanaendelea kuongezeka huku watumiaji wengi wakihama kutoka matumizi ya fedha taslimu kwenda kadi za malipo, hali inayotajwa kuendana na jitihada za Serikali za kujenga uchumi wa kidijitali na kuongeza ujumuishwaji wa kifedha.
Mwelekeo huo umebainishwa na Benki ya Stanbic kwa kushirikiana na Visa baada ya kukamilisha kampeni ya kuhamasisha matumizi ya kadi, ambapo idadi ya miamala iliongezeka kwa asilimia 113 na thamani ya miamala kupanda kwa asilimia 201.
Aidha, uanzishaji wa matumizi ya kadi (card activation) uliongezeka kwa asilimia 3,082 kwa idadi ya miamala na asilimia 449 kwa thamani, jambo linaloashiria kuongezeka kwa matumizi ya huduma za malipo ya kidijitali.
Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Stanbic Bank, Emmanuel Mahodanga, amesema matokeo hayo yanaonyesha Watanzania wanaendelea kujenga imani katika matumizi ya malipo salama ya kidijitali, hususan kwa miamala inayovuka mipaka.
Amesema benki hiyo itaendelea kushirikiana na Visa kuwawezesha wateja kufanya miamala kwa usalama wanaposafiri, kufanya biashara, kulipia elimu au kununua bidhaa na huduma mtandaoni.
Kwa upande wake, Meneja Mkazi wa Visa Tanzania, Victor Makere, amesema ukuaji huo unaonyesha mchango wa ushirikiano kati ya sekta ya benki na kampuni za teknolojia ya malipo katika kuharakisha matumizi ya huduma za kidijitali.
Amesema hatua hiyo inaunga mkono azma ya Tanzania ya kujenga uchumi usiotegemea fedha taslimu na kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi.
Stanbic Bank na Visa zimesema zitaendelea kuimarisha ushirikiano wao kwa kupanua elimu kuhusu matumizi ya malipo ya kidijitali, kuongeza upatikanaji wa ofa na huduma za kimataifa kwa wamiliki wa kadi pamoja na kutumia teknolojia na uchambuzi wa takwimu kuboresha huduma zinazotolewa kwa wateja, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono mpito wa Tanzania kuelekea uchumi wa kidijitali na jumuishi zaidi kifedha.