Prime
Mchakamchaka waanza urais, wagombea 17 wapewa magari
Muktasari:
- Vyama 17 kati ya 18 vimetimiza masharti ya kuanza kampeni za urais kabla ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025. Wagombea walioteuliwa na INEC wapewa magari, madereva na ulinzi.
Dodoma. Vyama 17 kati ya 18 vimetimiza masharti ya kuanza safari ya kuisaka Ikulu kupitia sanduku la kura katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewateua wagombea 17 wa urais na kuanzia kesho, Alhamisi Agosti 28, 2025, wataanza mchakamchaka wa kampeni kwa siku 61, kuzunguka nchi nzima kunadi ilani zao kwa wananchi.
Kampeni hizo, ambazo zitakoma Oktoba 28, zinahusisha uchaguzi wa madiwani, wabunge na Rais. Vyama vitakuwa na kazi ya kuomba ridhaa kwa wananchi ya kuwatumikia kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Chama ambacho mgombea wake hakuteuliwa ni ACT-Wazalendo, ambacho kilipanga kumsimamisha Luhaga Mpina, ambaye leo Jumatano mbio zake zimeishia geti la ofisi ya INEC, Njedengwa, jijini Dodoma.
Msafara wa ACT-Wazalendo ulifika ofisi za tume saa 6:37 mchana na baada ya kufika, lango la kuingia ndani lilifungwa, huku Polisi wenye silaha na virungu walisogea wengine wakishuka kwenye gari, na wengine waliendelea kuwapo kwenye magari.
Mabishano yalidumu kwa dakika kadhaa, lakini Polisi waligoma kufungua geti wala kuruhusu kiongozi wa ACT-Wazalendo aingie ndani, kama alivyokuwa ameomba, na kuwataka wawasiliane na viongozi wa tume, lakini siyo kuingia.
Baada ya mabishano yaliyodumu zaidi ya dakika 10, mgombea wa chama hicho, Mpina, alinyanyua mkoba aliopewa siku alipochukua fomu, kisha yeye na mgombea mwenza wake, Fatuma Abdulhabib Fereji, waliingia kwenye magari yao na msafara ukaondoka, kisha Polisi nao waliondoka.
Mapema asubuhi, INEC ilitoa ratiba iliyoonesha ACT-Wazalendo wangechukua fomu wakiwa chama cha 18, kama ilivyokuwa wakati wa uchukuaji.
Mpina, aliyewahi kuwa mbunge wa Kisesa (CCM) kwa miaka 20 mfululizo, alihamia ACT-Wazalendo Agosti 5, na kesho yake, Agosti 6, akapitishwa na mkutano mkuu kuwania urais.
Hata hivyo, Katibu Mwenezi wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Ndala, alipinga hatua hiyo kwamba ni kinyume cha kanuni za uendeshaji wa chama hicho. Majadiliano ya barua baina ya ofisi ya msajili na chama chake yalihitimishwa kwa msajili kukubali malalamiko ya Monalisa kwamba yako sahihi.
Hakukuwa na mbwembwe
Tofauti na wakati waliokwenda kuchukua fomu, leo kulikuwa na utulivu mkubwa kwa wagombea, kuwa na vikundi vya watu wachache bila mbwembwe za namna yoyote, ingawa vioja vya mavazi na matumizi ya gari moja kwa chama zaidi ya kimoja vilikuwapo.
Kituko kingine kilikuwa kwa mgombea Doyo Hassan Doyo wa chama Cha NRA, aliyezikwepa kamera kutopanda gari alilopewa, kitendo kilichotafsiriwa kama kukimbia kauli aliyoitoa kwamba akipewa nchi, atauza magari yote aina ya VX na kutaka watu watumie gari za kawaida.
Baada ya kukabidhiwa gari, mlinzi alifungua mlango na mgombea huyo aliingia, lakini kabla ya kukaa alishuka, ndipo akaanza kutembea akielekea lango kuu.
Kitendo cha kushuka kilimfanya mlinzi naye akateremke na kuongozana naye, lakini mgombea mwenza alibaki ndani ya gari, na dereva akaanza kuondoka mwendo wa taratibu. Alipotoka nje ya lango, gari ilisimama na wawili hao walionekana wakipanda.
Kama ilivyokuwa wakati wa uchukuaji wa fomu, mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, alifungua pazia hilo, huku Yustas Rwamugira wa TLP akifunga pazia.
Wengine walioteuliwa na INEC na vyama vyao katika mabano ni David Mwaijojele (CCK), Salim Mwalimu (Chaumma), Kunje Ngombale (AAFP), Doyo Hassan Doyo (NLD), na Majalio Kyara wa SAU.
Wengine ni Ambali Hamis (NCCR-Mageuzi), Georges Busungu (Tadea), Wilson Mulumbe (ADC), na mgombea wa chama cha NRA, Hassan Almas.
Uteuzi huo pia umewagusa Samandito Gombo (CUF), Mwajuma Mirambo (UMD), Twalib Kadege (UPDP), Abdul Mluya (DP), pamoja na mgombea Coaster Kibonde (Chama cha Makini).
Ukiacha msafara wa mgombea urais wa CCM, wagombea wengine walilazimika kusubiriana kila eneo la mapumziko, kwani walikuwa wakiingia kwa kufuatana, kabla ya wengine hawajatoka, waliingia wengine na kutakiwa wasubiri.
Wagombea washtukizwa
Katika hali ambayo iliwastua, baadhi ya wagombea ni kama hawakujua au hawakuwa na taarifa za kupewa magari na ulinzi kwa ajili ya kampeni.
Kila mgombea aliyekidhi vigezo na kuteuliwa, alikabidhiwa gari jipya lenye mafuta yaliyojaa tanki (kwa mujibu wa madereva).
Mbali na magari, wagombea hao walipewa madereva wa Serikali na ulinzi katika kipindi chote cha kampeni hadi siku ya kutangazwa matokeo.
"Gari hili unapewa kwa ajili ya kampeni, kumbuka ni mali ya Serikali, ila unaruhusiwa kubadilisha stika zako kwa gharama zako, na utazitoa kwa gharama zako," amesema kwa kurudia Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima, wakati akiwakabidhi magari hayo kwa nyakati tofauti.
Hata hivyo, Kailima hakutoa ufafanuzi wa nani anahudumia magari hayo kwenye mafuta huko mikoani na kama gari litaharibika, nani anawajibika kwenye matengenezo.
Akizungumza wakati akikabidhi gari na masharti kwa mgombea wa CUF, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima amesema uamuzi wa kutoa magari kwa wagombea ni baada ya kuona baadhi ya vyama vilikuwa na nguvu ndogo ya kufika katika maeneo yote.
"Tunakupa gari hili jipya, tunakupa na dereva na mlinzi, gari hili ni mali ya Serikali. Litakusaidia katika kipindi chote cha kampeni, na hii inaondoa lawama kwamba baadhi ya wagombea wasingeweza kufika maeneo mengine kwa changamoto za usafiri," amesema Kailima.
Alipotakiwa kutoa ufafanuzi juu ya jambo hilo, Kailima amesema baada ya shughuli zote kukamilika si muda wa kuzungumza, kwani kazi imekwisha.
Vyama viwili, wagombea wake walikuja na usafiri wa gari moja lililokuja kwa awamu mbili tofauti, ambapo awali Tadea walikuja na gari hilo, na baadaye NCCR-Mageuzi walilitumia pia.
Dereva aliyekuwa na gari hilo amesema kuwa, Tadea walikuwa wamekodi kwa ajili ya kuwapeleka INEC mtaa wa Njedengwa, lakini mara zote huwa wanalitumia watu wa NCCR-Mageuzi, ingawa pia huwa wanalipia.
Fomu zimebandikwa
Saa 9:52 alasiri, watumishi wa INEC walitoka nje ya lango na kubandika orodha ya wagombea walioteuliwa kwenye mchakamchaka huo.
Kailima amesema ni takwa la kisheria kubandika majina, ili kama kuna watu wangetaka kuangalia au kukata rufaa, waruhusiwe kufanya hivyo.
"Mheshimiwa mwenyekiti, kama inavyotaka sheria, tayari tumebandika majina ya wagombea waliokidhi vigezo na kuteuliwa, hapa anaruhusiwa mtu yeyote kuja kutazama, na akiona kuna mapungufu kwenye fomu, anaweza kukata rufaa dhidi ya mgombea," amesema Kailima alipokuwa akimuonesha Mwenyekiti wa INEC, Jaji mstaafu wa Rufani, Jakobo Mwambegele.