Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwalimu awaahidi Morogoro siku 100 za mwanzo Ikulu

Morogoro. Katika hekaheka za watiania wa urais kusaka wadhamini mikoani ili kupata ridhaa hiyo, mtiania wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu ametaja suluhu migogoro ya wakulima na wafugaji nchini.

Mwalimu ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chaumma ameyasema hayo leo Jumanne, Agosti 19, 2025 alipozungumza na wananchi mjini Mikumi, Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro akiomba udhamini wao.

Mwalimu ni miongoni mwa watinia 18 wa urais ambao Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewakabidhi fomu za kuomba kuteuliwa. Uteuzi utafanyika Agosti 27, 2025. Kampeni itakuwa Agosti 28 hadi Oktoba 28, 2025. Upigaji kura itakuwa Oktoba 29.

Mabango yenye ujumbe wa kumtaka Jonas Nkya kujiunga na Chaumma na kuwania ubunge wa Mikumi, yameonekana kwa wingi katika mkutano wa kampeni wa mgombea urais wa chama hicho, Salum Mwalimu, uliofanyika leo Jumanne Agosti 19, 2025, Mikumi baada ya kumaliza ziara yake Iringa.

Mwalimu ameahidi kutumia siku 100 za kwanza katika utawala wake kumaliza migogoro hiyo akitaja mbinu zinazohitajika.

"Mkoa wa Morogoro unaongoza kwa mauaji yanayotokana na mipigano ya wakulima na wafugaji, katika ilani ya Chaumma, suala hilo mkinipa ridhaa nitalitatua ndani ya siku 100 za utawala wangu," amesema.

"Migogoro ya ardhi Kilosa imekithiri, mifugo yetu imegeuka laana kwa wanakilosa, mapigano ya wakulima na wafugaji hayatamalizwa na CCM, imeshindwa, nipeni mimi ninawaahidi ndani ya siku 100 yatakwisha," ameongeza.

Amebainisha kutatua migogoro ya ardhi kunahitaji viongozi wenye hofu ya Mungu na utashi wa kisiasa wasio na historia chafu ili kuwa na ujasiri wa kukemea uovu.

"Kutatua matatizo ya ardhi nchini haihitaji muujiza, bali hofu ya Mungu kwa kiongozi na utashi wa kisiasa katika kumaliza kero hizi," amesema.

"Mnapochagua viongozi wenye makandokando Wanalindana niwalewale wote wachafu, wanashindwa kufanya maamzi magumu wakihofia yao pia kufukuliwa," ameongeza.

Kutokana na mwingiliano wa jamii za wafugaji wa wakulima katika wilaya za Kilosa na Ulanga, Mkoa wa Morogoro umekuwa ukiripotiwa kwa migogoro kati ya wakulima na wafugaji huku serikali iliendelea kushughulikia kero hiyo.

Akizungumza katika mkutano huo, mtiania mwenza wake wa urais, Devotha Minja amewaomba wakazi wa Morogoro kuchagua wagombea wa Chaumma ili kujenga mkoa huo upya.

"Tukatae kuwa shamba la bibi Morogoro, tupeni diwani wa Chaumma, tupeni mbunge, tupeni Rais wa Chaumma tukairudishe Morogoro kwenye msingi," amesema.


Amkaribisha Nkya

Kutokana na mabango waliyobeba wananchi wakiomba aliyekuwa mtiania wa ubunge wa Mikumi kupitia CCM, Jonas Nkya kujiunga na kugombea ubunge kwa chama hicho, Mwalimu amemtumia ujumbe akimkaribisha Chaumma.

Mabango yenye ujumbe wa kumtaka Jonas Nkya kujiunga na Chaumma na kuwania ubunge wa Mikumi, yameonekana kwa wingi katika mkutano wa kampeni wa mgombea urais wa chama hicho, Salum Mwalimu, uliofanyika leo Jumanne Agosti 19, 2025, Mikumi baada ya kumaliza ziara yake Iringa.

"Nimeona kiu yenu, Chaumma tunaheshimu maoni ya wananchi, mfikishieni taarifa zangu Jonas Nkya kuwa namkaribisha Chaumma, tupo tayali kumpokea wakati wowote," amesema.

"Akija nitakuja kumpokea hapa Mikumi, hata iwe saa nane usiku na Chaumma kwakuwa bado hatujateua wagombea wa ubunge, tutampa ridhaa ya kugombea jimbo hili kama mnavyoomba," amesema.

Mwalimu ameingia mkoani Morogoro akitokea Iringa katika ziara yake ya kutafuta wadhamini katika safari yake ya kugombea urais wa Tanzania.

Kutoka hapo, kesho ataendelea katika mikoa mingine ya kanda ya kati ikiwemo Dodoma na Singida kabla ya kuelekea Kanda ya Ziwa.

Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024, kifungo cha 33 (1) kinaeleza: Ili kuweza kuteuliwa kuwa mgombea halali wa kiti cha Rais, mtu anapaswa kudhaminiwa kwa maandishi na wadhamini walioandikishwa kuwa wapiga kura kwa madhumuni ya uchaguzi chini ya sheria hii wasiopungua 200 kwa kila mkoa, angalau kwa mikoa 10 ya Jamhuri ya Muungano, kati ya hiyo angalau mikoa miwili kutoka Zanzibar.