Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwalimu: Nipo tayari kuvivaa viatu vya Magufuli, kuinyoosha Tanzania upya

Mgombea urais kupitia Chaumma, Salum Mwalimu ameahidi kuendeleza misingi ya utawala wa Rais wa awamu ya tano, hayati  John Magufuli endapo atachaguliwa kuongoza dola katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

Muktasari:

  • Nawaomba wananchi wa Nkololo mkanichague nikavivae viatu vya Magufuli nikainyooshe hii nchi waliobakia wameshindwa, kuendeleza alipoishia.

Bariadi. Mgombea urais kupitia Chaumma, Salum Mwalimu ameahidi kuendeleza misingi ya utawala wa Rais wa awamu ya tano, hayati  John Magufuli endapo atachaguliwa kuongoza dola katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

Akihutubia maelfu ya wakazi wa Nkololo, Bariadi Vijijini mkoani Simiyu leo Septemba 12, 2025, Mwalimu amesema Serikali ya Magufuli ilijitahidi kutatua changamoto za wananchi, hasa katika sekta ya kilimo, miundombinu, na mapambano dhidi ya rushwa.

Hata hivyo, ameeleza kuwa baada ya kifo cha Magufuli, juhudi hizo zimedhoofika.

"Nichagueni niende Ikulu nikavae viatu vya Magufuli, nikainyooshe hii nchi... Alikuwa mwanaume mmoja tu aliyefanikisha; wengine wote wameshindwa," amesema kwa msisitizo.

Mwalimu ameahidi kuleta mabadiliko ya kweli kwa kuendeleza miradi ya maendeleo, kudhibiti unyonyaji wa wakulima, na kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali zao.

Ametolea mfano zao la pamba, kwamba enzi za Magufuli bei ilikuwa juu na wakulima walinufaika, lakini sasa wamelazimika kukabiliana na hali ngumu ya maisha kutokana na kuporomoka kwa bei na mifumo isiyo rafiki kwa mkulima.

“Nikiwa Ikulu, nitakuja na sera ya kurudisha heshima ya Kanda ya Ziwa… nitapigania bei ya pamba ipande kama ilivyokuwa enzi za Magufuli,” ameahidi.

Mwalimu amesema Tanzania haihitaji viongozi waoga, wala waliokata tamaa, akisisitiza kuwa Taifa linahitaji mtu mwenye uthubutu na moyo wa kizalendo.

“Nchi hii haihitaji mtu anayetembea na vidonge vya presha… ina utajiri mkubwa, ninawaomba mniamini niende nikawasaidie Watanzania,” amesema huku akishangiliwa na wananchi waliohudhuria mkutano huo.

Kuhusu changamoto za wakazi wa maeneo ya hifadhi kama Serengeti na pori la Maswa, Mwalimu amesema ni lazima wafaidike na rasilimali hizo, badala ya kuendelea kuwa waathirika wa migogoro isiyokwisha na vifo vinavyotokana na wanyamapori.

"Nikiwa rais kama nilivyosema Serengeti nitatengeneza utaratibu walau wananchi wanaoishi karibu na hifadhi wanufaike nitawapa vibali kama wanahitaji kitoweo cha mnyama ya swala basi wakawinde wale, kwa sababu Mungu alivyowaumba wakaishi jirani na hifadhi ndiyo neema yao, lazima waitumie,"  amesema.

Kwa upande wake, Kwandu Mpanduzi, mgombea ubunge wa Bariadi Vijijini kwa tiketi ya Chaumma, alitaka Serikali iitambue Nkololo kama mji mdogo ili huduma ziwafikie wananchi kwa ukaribu zaidi.

Amelalamikia bei ndogo ya pamba na kukosekana kwa huduma muhimu licha ya eneo hilo kuwa jirani na Hifadhi ya Serengeti.

“Tunalima pamba lakini hatupati faida. Bei ni ndogo mno kiasi kwamba haimudu hata gharama za uzalishaji,” amesema Mpanduzi.


Alitoa wito kwa Mwalimu

Iwapo atachaguliwa kuongoza nchi kuhakikisha kodi kwenye zao la pamba zinapunguzwa na soko huria linaanzishwa ili kuwapa wakulima faida halisi.