Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nchimbi: Rais Samia anaitaka Katiba mpya

Muktasari:

  • Dk Nchimbi amewataka Watanzania kutumia fursa ya Katiba mpya ambayo tayari ameshaonyesha nia kabla hajatoka madarakani.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Emmanuel Nchimbi, amesema ipo haja ya kutumia utayari ulioonyeshwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuendeleza mchakato wa Katiba mpya ili ukamilike kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2028 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2030.

Dk Nchimbi ametoa kauli hiyo leo Ijumaa, Julai 24, 2026, wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Amesema katika mfumo wa uendeshaji wa Baraza la Mawaziri, Rais ndiye mwenye mamlaka ya kuamua ajenda zinazojadiliwa, huku wajumbe wengine wakitoa ushauri, jambo linaloonyesha kuwa dhamira ya mkuu wa nchi ni muhimu katika kuamua hatima ya mchakato wa Katiba mpya.

Akizungumzia hatua zilizofikiwa, Dk Nchimbi amesema alipokuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na msimamizi wa uandishi wa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho, kamati iliyokusanya maoni ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini ilibaini kuwa Katiba mpya ilikuwa miongoni mwa vipaumbele vikuu vilivyotajwa na wananchi.

Amesema aliwasilisha mapendekezo hayo kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan, na kusisitiza kuwa hoja ya Katiba Mpya ipewe nafasi katika Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho kwa kuwa ilitokana na matakwa ya wananchi.

"Baada ya kamati kutueleza kuwa Watanzania wanahitaji Katiba mpya, tulimshauri mgombea urais wa CCM wakati huo kuingiza ahadi hiyo kwenye ilani, na akaikubali," amesema.

Dk Nchimbi amesema baada ya kuingia madarakani, Rais Samia alianza kutekeleza ahadi hiyo kwa kuunda tume ya kushughulikia mchakato wa Katiba mpya.

Ameongeza kuwa mapendekezo ya Tume ya Jaji Francis Nyalali pamoja na Tume ya Jaji Robert Chande yalielekeza umuhimu wa Katiba mpya kupatikana kabla ya chaguzi za mwaka 2028 na 2030 ili itumike katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu.

Kutokana na mazingira hayo, Dk Nchimbi amesema Watanzania wanapaswa kutumia fursa iliyopo sasa badala ya kusubiri uongozi mwingine ambao huenda usiwe na dhamira ya kuendeleza mchakato huo.

"Katiba ya sasa inampa Rais madaraka makubwa. Si kila kiongozi anaweza kuwa tayari kuyaacha. Ndiyo maana ni muhimu wananchi washikilie fursa iliyopo sasa kwa kuwa Rais Samia ameonyesha utayari wa kuendeleza mchakato wa Katiba mpya," amesema.