Ongezeko bajeti ya ulinzi lawashtua wadau wa maendeleo
Waziri wa Fedha, Muhammad Aurangzeb
Wadau wa maendeleo na wachumi nchini Pakistan wamekosoa uamuzi wa Bunge kupitisha bajeti kubwa ya ulinzi na jeshi wakati nchi hiyo ikikabiliwa na changamoto nyingi katika sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na watoto wengi kushindwa kwenda shule kutokana na sababu mbalimbali.
Katika bajeti iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha, Muhammad Aurangzeb, serikali imeongeza matumizi ya ulinzi kwa karibu asilimia 18 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Hatua hiyo imezua mjadala katika jamii kutokana na fedha zilizotengwa katika sekta ya elimu kuwa ndogo na chini ya viwango vinavyopendekezwa kimataifa.
Hata hivyo, wakati wa uwasilishwaji wa bajeti hiyo, serikali ilieleza sababu ya kutenga fedha nyingi kwenye usalama kuwa kunatokana na kuongezeka kwa mashambulizi ya kigaidi na masharti magumu ya mikopo inayotakiwa kulipwa kwa wakati.
Tamko la wadau hao wa maendeleo na wachumi kwenda serikalini limebainisha kuwa ulinzi na jeshi zimetengwa Rupia trilioni 3.01 huku katika elimu ikitengwa Rupia bilioni 117.75.
‘’Serikali imetenga Rupia bilioni tatu tu kiasi ambacho ni kidogo sana kwa ajili ya miradi ya kuwarejesha shuleni watoto waliokosa fursa hiyo,’’
‘’Takribani Rupia bilioni 46 kwa ajili ya elimu ya juu na rupia bilioni 25 kwa ajili ya huduma ya afya zimetengwa. Ukijumlisha kiasi hicho chote ni kidogo ikilinganishwa na bajeti kubwa ya ulinzi,’’ inaeleza sehemu ya tamko hilo lililosainiwa na mmoja wa viongozi wa muungano wa wachumi na wadau wa maendeleo, Dkt. Fahd Ali.
Linaeleza kuwa umasikini Pakistan umeongezeka miaka ya hivi karibuni likinukuu takwimu za utafiti wa uchumi Pakistan mwaka 2025/26 unaoeleza idadi ya watu masikini kuongezeka hadi asilimia 28.9 mwaka 2024-25, kutoka asilimia 21.9 mwaka 2018-19.
‘’Changamoto nyingine tuliyoieleza ni kiasi kikubwa cha fedha kutumika kulipa deni la serikali, hii hupunguza kiwango cha fedha zinazopaswa kutengwa kwa ajili ya miradi ya Maendeleo,’’ inaeleza sehemu ya tamko hilo.
Linaeleza kuwa nchini Pakistan takribani watoto milioni 25 wenye umri kati ya miaka mitano hadi 16 hawajapata elimu na wengine wanakwama kuhudhuria masomo kikamilifu.