Ruwasa: Upatikanaji wa maji vijijini wafikia asilimia 85.2
Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara ya Maji na Mratibu wa Programu ya Malipo kwa Matokeo, Mashaka Sitta, akizungumza wakati wa mafunzo ya kupitia vigezo vitakavyotumika katika utekelezaji na uhakiki wa miradi ya maji, afya na elimu chini ya Programu Endelevu ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Awamu ya Pili (SRWSSP II), yaliyofanyika jijini Mwanza.
Muktasari:
- Ruwasa yasema upatikanaji wa huduma ya maji vijijini umeongezeka kutoka asilimia 64.8 mwaka 2019 hadi asilimia 85.2 kufikia Desemba 2025.
Mwanza. Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) umesema upatikanaji wa huduma ya maji vijijini umeongezeka kutoka asilimia 64.8 mwaka 2019 hadi asilimia 85.2 kufikia Desemba 2025, kupitia utekelezaji wa Programu Endelevu ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (SRWSSP).
Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa, Wolta Kirita, amesema mafanikio hayo yamepatikana kupitia programu iliyokuwa ikitekelezwa kwa mfumo wa Payment for Results, unaolenga kutoa fedha kulingana na matokeo yaliyofikiwa.
Kirita alitoa kauli hiyo leo jijini Mwanza wakati wa mafunzo ya kupitia vigezo vitakavyotumika katika utekelezaji na uhakiki wa miradi ya maji, afya na elimu chini ya Programu Endelevu ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Awamu ya Pili (SRWSSP II).
Alisema wakati programu inaanza mwaka 2019, sambamba na kuanzishwa kwa Ruwasa, upatikanaji wa maji vijijini ulikuwa asilimia 64.8, lakini uliongezeka hadi kufikia asilimia 85.2 ifikapo Desemba 2025.
"Programu hii haikujenga miradi pekee, bali ilitusaidia kujenga utamaduni wa kufanya kazi kwa kuzingatia matokeo, kwa sababu mfumo wake ni Payment for Results," amesema Kirita.
Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa, Wolta Kirita, akifafanua jambo wakati wa mafunzo ya siku tatu ya kupitia vigezo vitakavyotumika katika utekelezaji na uhakiki wa miradi ya maji, afya na elimu itakayotekelezwa kupitia Programu Endelevu ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Awamu ya Pili (SRWSSP II), yanayofanyika jijini Mwanza.
Amesema katika kipindi cha utekelezaji, zaidi ya wananchi milioni 10.2 walipata huduma ya maji safi na salama, idadi inayozidi kwa asilimia 116 lengo lililowekwa mwanzoni mwa programu.
Mbali na kuongeza idadi ya wananchi wanaopata huduma, alisema programu ililenga kuhakikisha miradi inabaki kufanya kazi kwa ufanisi hata baada ya kukamilika.
"Kila mwaka tulifanya tathmini ya vituo vya maji. Lengo lilikuwa angalau asilimia 75 ya vituo viendelee kufanya kazi, lakini tulifanikiwa kuvifikisha zaidi ya vituo 83,000 vinaendelea kutoa huduma," amesema.
Kirita amesema programu pia imeimarisha usimamizi wa fedha, matumizi ya kemikali za kutibu maji, uwasilishaji wa taarifa kwa wakati pamoja na kuimarisha uwezo wa taasisi.
Amesema Ruwasa sasa ina makao makuu ya kudumu, mameneja wa mikoa 25 na mameneja wa wilaya 128, huku juhudi za kuboresha miundombinu ya ofisi zikiendelea.
Waratibu wa Programu ya Malipo kwa Matokeo (PforR) wakifuatilia mafunzo ya kujengewa uwezo kuelekea kuanza kwa utekelezaji wa Programu Endelevu ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Awamu ya Pili (SRWSSP II), yanayofanyika jijini Mwanza.
Aidha, ameishukuru Serikali na wadau wa maendeleo kwa kuwezesha utekelezaji wa programu kupitia Mfuko wa Maji, Serikali Kuu na Benki ya Dunia.
Pamoja na mafanikio hayo, Kirita amesema bado kuna changamoto za upatikanaji wa maji katika baadhi ya maeneo, hivyo awamu ya pili ya programu itaweka mkazo katika kuhakikisha miradi iliyojengwa inakuwa endelevu na inaendelea kutoa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mratibu wa Programu kutoka Wizara ya Maji, Mashaka Sitta, amesema SRWSSP ni programu ya sekta ya maji, usafi wa mazingira na afya inayotekelezwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Maji, Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu, kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.
Amesema kwa upande wa maji, utekelezaji unasimamiwa na Ruwasa, huku shughuli za usafi wa mazingira zikitekelezwa kupitia Ofisi ya Rais-Tamisemi.
Sitta amesema awamu ya kwanza ya programu iliyoanza mwaka 2019 na kumalizika mwaka 2025 ilipata mafanikio makubwa, ikiwemo kujenga zaidi ya vyoo 830 katika shule, kuvifikia zaidi ya vituo 2,000 vya kutolea huduma za afya kwa maji na huduma za usafi wa mazingira, pamoja na kuwezesha zaidi ya wananchi milioni 12 vijijini kuwa na vyoo bora.
Kutokana na mafanikio hayo, amesema Benki ya Dunia imeidhinisha zaidi ya dola milioni 200 kwa ajili ya utekelezaji wa awamu ya pili ya programu kwa kushirikiana na Serikali.
Alisema utekelezaji wa awamu hiyo ulianza Februari mwaka huu na unafanyika katika mikoa 25 ya Tanzania Bara, ukihusisha halmashauri 137, isipokuwa Mkoa wa Dar es Salaam.