Prime
Sarakasi watiania udiwani kukatwa
Muktasari:
- Tangu jana Jumatano, baadhi ya maeneo yameripotiwa kuwapo maandamano na wengine wakibeba mabango yenye ujumbe wa kutaka majina ya watu wao yarejeshwe
Dar/Mikoani. Sarakasi za watiania ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) zimehamia kwa madiwani baada ya wananchi katika baadhi ya mikoa kuanzisha maandamano wakitaka majina ya wanaowataka yarejeshwe.
Tangu jana Jumatano, baadhi ya maeneo yameripotiwa kuwapo maandamano na wengine wakibeba mabango yenye ujumbe wa kutaka majina ya watu wao yarejeshwe.
Utaratibu wa uchaguzi ndani ya CCM ni kufanya mchujo wa majina ya wagombea ubunge, uwakilishi na udiwani ambao awali, Katiba ilitaka majina matatu kabla ya kufanya marekebisho ambayo yameruhusu kwa baadhi ya kata na majimbo kuwa na wagombea wanaofikia hadi wanane.
Julai 29, 2025 majina ya wagombea nafasi ya udiwani ndani ya CCM yaliwekwa hadharani tayari kwa uchaguzi wa udiwani na ubunge ndani ya chama utakaofanyika Agosti 4, 2025 nchi nzima.
Leo wakazi wa Kata ya Muze Wilaya ya Sumbawanga Vijijini mkoani Rukwa, wamezuia msafara wa viongozi wa CCM, wakilalamikia mchakato wa uteuzi wa majina ya wagombea udiwani katika kata hiyo.
Kilio cha wananchi kinatokana na kile walichodai kuwa, orodha ya awali ya wagombea watatu iliyotangazwa Julai 29, 2025, ilibadilishwa jana asubuhi Julai 30 na jina la mgombea wa nne kuongezwa.
Kwa nyakati tofauti Stella Kwimba na Mzee Mazengo, wamesema lengo la kuzuia msafara huo ni kupata majibu juu ya suala hilo, kwa nini mchakato wa uteuzi haujazingatia masilahi ya wananchi.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi Wilaya ya Sumbawanga Vijijini lilifika eneo la tukio na kuwatawanya wananchi kisha kuusindikiza msafara wa viongozi hao hadi ofisi za CCM wilayani Sumbawanga.
Jijini Dar es Salaam katika Kata ya Kunduchi, Wilaya ya Kinondoni baada ya maandamano ya wananchi yaliyofanyika jana kudai kutoridhishwa na uamuzi wa kuondoshwa kwa jina la aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Michael Urio, leo Alhamisi, Julai 31, 2025 limerejeshwa kwenye ‘mkeka’ wa wagombea wa kata hiyo.
Jana, baadhi ya wanachama waliandamana hadi Ofisi ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam wakilalamikia kukatwa kwa jina la Urio ambaye pia alikuwa naibu meya wa Kinondoni na mtiania wa udiwani Kunduchi.
Wanachama hao walikutana na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Mtemvu, ambaye pia ni mlezi wa kata hiyo na kufanya naye kikao.
Baada ya kikao, Katibu wa CCM Tawi la Tandale Kibaoni, Bundala Malima alisema hawajaridhika na maelezo waliyopewa.
Lakini Mtemvu aliwahakikishia kuwa, vikao vya siasa vinavyofanyika leo na kesho, vitatoa majibu ya mwisho Agosti 2, 2025.
Jijini Dodoma, wakazi wa Kizota wameandamana kushinikiza jina la Jamal Ngalya aliyewahi kuwa naibu meya na diwani wa kata hiyo lirejeshwe.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kizota, Habibu Sinkara amekiri kuwepo kwa mkusanyiko huo akisema hayakuwa maandamano.
"Sisi Kamati ya Siasa tulikwenda wilayani kisha mkoani, wakatuambia twende makao makuu kujua kilichotokea, kina mama walichukua magari wakatufuata," amesema Sinkara.
Hata hivyo, mwenyekiti aliwaambia wananchi hao kuwa, warudi walikotoka kwa kuwa chama kina taratibu zake, kama kuna shida mgombea aende.
“Kila mgombea anajua utaratibu, sasa kama kuna shida au hajaridhika aje mwenyewe ofisini,” amesema Kizota.
Hali kama hiyo ilitokea jana Kata ya Kitangiri mkoani Mwanza wananchi walipinga kuondolewa kwa jina la aliyekuwa diwani wao, Donald Ndaro kwenye mchakato wa uteuzi.
Wakazi hao walisema Ndaro alikuwa kiongozi wa mfano wakahoji kwa nini jina lake limeondolewa.
Moshi Vijijini mambo shwari
Kwa upande wa halmashauri za Moshi na Hai, waliokuwa madiwani majina yao yameteuliwa na chama kwa ajili ya kuomba kuchaguliwa na wajumbe ili kutetea nafasi zao katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Katika wilaya za Hai na Moshi Vijijini, makatibu wa wilaya wamesema kwao hakuna mgogoro kwa kuwa, madiwani wa zamani wote walioomba majina yamerejeshwa kwenye ‘mkeka.’
Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini, Ramadhan Mahanyu na Katibu wa CCM Wilaya ya Hai, Hamisi Kura wamesema wote waliokuwa madiwani wamerejeshwa.
Imeandikwa na Janeth Joseph (Moshi), Habel Chidawali (Dodoma), Neema Mtuka (Rukwa), Sute Kamwelwe (Dar) na Saada Amiri (Mwanza)