Shughuli kwa wanaousaka urais kutafuta wadhamini
Muktasari:
- Watiania hao watakuwa na kazi ya kuzunguka mikoani kutafuta wadhamini ili kutimiza masharti ya kisheria ili wateuliwe na INEC kuwa wagombea katika uchaguzi mkuu ulipangwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Dar es Salaam. Wakati Shughuli ya uchukuaji wa fomu za uteuzi kutoka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ikihitimishwa leo Agosti 15, 2025, shughuli iliyo mbele ya watiania wa vyama vya vyama vya siasa kwa sasa ni kutafuta wadhamini.
Watiania hao watakuwa na kazi ya kuzunguka mikoani kutafuta wadhamini ili kutimiza masharti ya kisheria ili wateuliwe na INEC kuwa wagombea katika uchaguzi mkuu ulipangwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Kwa mujibu wa kifungu cha 33(1) Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024, ili kuteuliwa kuwa mgombea halali wa kiti cha Rais, mtu anapaswa kudhaminiwa kwa maandishi na wadhamini walioandikishwa kuwa wapigakura wasiopungua 200 kwa kila mkoa, angalau kwa mikoa 10 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kati ya hiyo angalau mikoa miwili kutoka Zanzibar.
Kifungu cha 33(2) kinabainisha kwamba wadhamini wa mgombea wa nafasi ya kiti cha Rais na nafasi ya Makamu wa Rais watathibitishwa na Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo ambalo wadhamini husika wameandikishwa.
Vilevile, kifungu cha 34(1) kinafafanua: “Tume itatoa fomu za uteuzi kwa mgombea wa kiti cha Rais aliyependekezwa na chama cha siasa au mpigakura aliyeidhinishwa na chama cha siasa kwa maandishi na kwa idadi kadiri itakavyoelekezwa na tume.”
Kifungu cha 34(2) kinaongeza kila mgombea wa kiti cha Rais atawasilisha fomu za uteuzi kwa utaratibu na mahali kadiri Tume itakavyoelekeza, si zaidi ya saa 10 kamili alasiri ya siku ya uteuzi.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, vyama vya siasa 17 kati ya 19 vyenye usajili wa kudumu vilipendekeza na kuwadhamini wagombea katika nafasi hiyo. Vyama hivyo ni AAFP, ACT-Wazalendo, Ada – Tadea, ADC, CCK, CCM, Chadema, Chaumma, CUF, Makini, DP, NCCR-Mageuzi, NLD, NRA, SAU, UMD na UPDP.
Uteuzi wa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais ulifanyika Agosti 25, 2020. Wagombea wa vyama 16 kati ya 17 waliochukua fomu walirejeresha fomu za uteuzi kwenye Ofisi za Tume, Dodoma, kwa ajili ya uteuzi.
Mgombea kutoka chama cha NLD hakurejesha fomu ya uteuzi. Wagombea wa vyama 15 kati ya vyama 16 waliorejesha fomu za uteuzi waliteuliwa na tume baada ya kukidhi masharti ya uteuzi.
Wagombea hao ni kutoka vyama vya CCM, NRA, Ada-Tadea, Sau, Makini, NCCR-Mageuzi, CUF, DP, ACT-Wazalendo, ADC, UPDP, Chaumma, UMD, AAFP na Chaumma. Mgombea wa CCK hakukidhi masharti ya uteuzi, hivyo hakuteuliwa.
Kati ya wagombea 15 wa kiti cha Rais walioteuliwa, wanawake walikuwa wawili sawa na asilimia 13 na wanaume 13 sawa na asilimia 87. Pia, kati ya wagombea 15 wa kiti cha Makamu wa Rais, wanawake walikuwa watano sawa na asilimia 33 na wanaume 10, sawa na asilimia 67.
Uchukuaji fomu ulivyokuwa
Ilikuwa wiki ya nderemo na mavuno kwa vijana wakati wateule wa vyama vya siasa wanaowania kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walipokuwa wakipishana katika jengo la INEC kuchukua fomu.
Pazia la uchukuaji fomu lilifunguliwa na mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Rais Samia Suluhu Hassan Agosti 9, 2025, kwa mujibu wa ratiba ya INEC vyama 18 vilivyotangaza kushiriki uchaguzi vimetekeleza hatua hiyo.
Hadi siku ya mwisho katika barua ya INEC, vyama 18 kati ya 19 vyenye usajili wa kudumu vimechukua fomu na sasa wanapishana mikoani kusaka wadhamini. Ni Chadema pekee ndicho hakishiriki uchaguzi ujao kwa sababu kinashinikiza mabadiliko katika mifumo ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa ratiba ya INEC, mara baada ya wagombea kusaka wadhamini mikoani, watarudi tena INEC na kuangalia waliokidhi vigezo watateuliwa Agost 27, 2025 na siku itakayofuata kampeni zitaanza.
Watakaopitishwa watakuwa na siku 60 za mchakamchaka wa kunadi sera zao ambapo uchaguzi mkuu utafanyika Oktoba 29, 2025.
Kama wangepewa ushindi kwa namna walivyoingia kwa matarumbeta na mbwembwe nyingi, basi chama pekee ambacho kingekosa ushindi kingekuwa NCCR Mageuzi ambacho wagombea wake, Haji Ambar Khamis na mgombea mwenza, Evaline Munisi waliongozana na wapambe wao 11 pekee.
NCCR Mageuzi hawakuwa na hata pikipiki moja iliyowasindikiza au hata kuwa na mtu wa kuanzisha wimbo ili wenzake waitikie.
Vijana walivyopiga pesa
Ilikuwa ni kama sinema na maigizo kwa vijana hasa waendesha pikipiki ambao walikuwa wakibadirisha sare za vyama na bendera, lakini nyimbo na miondoko ilibaki vilevile na walipoulizwa walijibu ni mwaka wa mavuno.
Mbali na shamrashamra za wagombea na wapambe, mambo muhimu yaliyotajwa mara nyingi afya ilichukua sehemu kubwa karibu kila mgombea alitaja suala la afya.
Vijana hao na kikundi cha matarumbeta walionekana kwenye misafara mingi ya wagombea wakiwa ndani ya sare za vyama, hivyo na baada ya muda walikuwa na sare zingine na bendera za vyama zilizopepea kwenye pikipiki zao.
Shamrashamra, ahadi za vyama
Mteule wa CCM, Rais Samia alifunika kwa maandamano yaliyofunga karibu mji wote wakati akichukua fomu na baadaye kufanya mkutano katika ofisi za makao makuu ya chama hicho.
Vijana walipamba pikipiki kwa bendera za kijana na msululu wa magari mengi na bajaji na alipozungumza na wajumbe alitaja mambo mengi katika ilani lakini akagusa sekta ya afya.
Mgombea wa AAFP, Kunje Ngombale Mwilu alikuwa na mbwembwe katika msafara wake lakini akataja kipaumbele mojawapo ni kilimo na afya kama ilivyokuwa kwa mgombea wa NRA, Hassan Almasi.
Naye Coaster Kibonde wa Demokrasia Makini, mbali na kutaja afya, alizungumzia Katiba mpya na kusisitiza usawa.
Msafara wa mgombea wa NLD, Doyo Hassan Doyo ndio ulikuwa wa namna yake kwani alionekana kutoka mbali akiwa kwenye bajaji akiwa amesimama akipunga mkono na hata hotuba yake iligusa watu wa hali ya chini ikiwemo waendesha pikipiki na bajaji.
Kwenye misafara ya pikipiki na mdundiko, Abdallah Kadege wa UPDP), Georges Busungu wa Ada-Tadea na Mwajuma Mirambo wa UMD, walizungumzia mambo ya afya, elimu na maji wakati mgombea wa TLP, Yusta Rwamugira akizungumzia kwenda kushughulikia matatizo Katiba.
Mwingine ambaye alizungumzia kwenda kushughulikia matatizo ya wastaafu alikuwa David Mwaijojele wa CCK ambaye hata hivyo msafara wake uliingi ukiwa na kikundi cha pikipiki chache.
Ukiacha CCM, msafara wa Chaumma ulifunika, idadi ya watu walikuwa wengi, vikundi vya burudani na muziki vilitosha kuamsha watu hata njia walizopita.
Mgombea wake, Salum Mwalimu alirudia zaidi ya mara tatu kusema “sijabebwa, niko safi na chama changu ni safi” akieleza ni zamu ya waandishi wa habari kwenda Ikulu.
Mgombea wa SAU, aliingia na kundi la akina mama ambapo alizungumzia haki, elimu na afya kuwa ni baadhi ya mambo atakayoyafanyia kazi, kama ilivyokuwa kwa Abdul Mluya wa DP, lakini tofauti yao ni kwamba Mluya aliingia na kundi vijana.
Hata hivyo, mteule wa CUF, Gombo Samandito Gombo wa CUF alikuwa na hoja kuu ya haki na suala la matibabu akisisitiza jamii kujitambua.
Msafara wa ADC chini ya mgombea wao, Wilson Mulumbe walikuwa na vijana na ngoma wakati mgombea wao akigusia elimu na jinsi atakavyokuwa suluhisho katika kilio cha wastaafu nchini.
Katika siku ya saba ambayo imehitimisha uchukuaji wa fomu kwa wagombea 18, Saum Rashid wa UDP, Haji Ambar Khamis (NCCR Mageuzi) na Luhaga Mpina (ACT Wazalendo) hawakuwa na mambo mengi wala mbwembwe walipofika ofisi za INEC.
Hakuna ngoma, milio ya pikipiki wala vikundi vilivyowasindikiza huku Mpina akishukia nje ya lango na kuanza kutembea akiingia ndani ya jengo.