Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sura mpya 2025 bila vigogo, wanawake wakiibuka juu

Muktasari:

  • Kwa jumla, uchaguzi wa mwaka huu unaashiria sura mpya katika siasa za upinzani nchini, bila uwepo wa vigogo waliokuwa nguzo kuu kwa miongo mitatu.

Dar es Salaam. Katika historia ya miaka 33 ya mfumo wa vyama vingi nchini, uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025 huenda ukaweka rekodi ya kipekee kwa kukosekana kwa vigogo waasisi na wakongwe waliodumu kwa muda mrefu katika majukwaa ya siasa za upinzani.

Kwa zaidi ya miongo mitatu, majina kama Freeman Mbowe, Maalim Seif Sharif Hamad, Profesa Ibrahim Lipumba, Augustine Mrema, John Cheyo, Fahmi Dovutwa na James Mbatia yamekuwa yakisikika kwa nguvu katika medani za siasa hususani kipindi kama hiki cha uchaguzi.

Hata hivyo, kwa mara ya kwanza tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa kwanza mwaka 1995, uchaguzi wa mwaka huu unafanyika bila ushiriki wao wa moja kwa moja.

Miongoni mwa wagombea wapya waliochukua fomu za kugombea urais ni  Majalio Kyara wa Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Abdul Mluya (DP),  Gombo Samandito Gombo wa Chama cha Wananchi (CUF).

Wagombea wengine ni Samia Suluhu Hassan wa  Chama cha Mapinduzi (CCM),  Salum Mwalimu (Chaumma), David Mwaijojele(CCK), Yustas Rwamugila (TLP), Mwajuma Noty (UMD),   Georges Bussungu (Ada Tadea),  Twalib Kadege(UPDP),          Doyo Hassan(NLD), Coaster Kibonde(Demokrasia Makini), Hassan Almas (NRA),      Kunje Ngombale Mwiru(AAFP), Saum Rashid (UDP), Haji Ambar Khamis (NCCR-Mageuzi)  na Luhaga Mpina (ACT – Wazalendo) .


Sura mpya za watiania wanawake zikiibuka

Katika uchaguzi wa mwaka huu, sura mpya zimeibuka huku wanawake wakipanda juu kisiasa tofauti na chaguzi zilizofanyika tangu uhuru wa Taifa hili.

Wanawake wawili, Samia wa CCM na Saum wa UDP, wameaminiwa kupeperusha bendera za vyama vyao kugombea urais wa Tanzania.

Mbali na hao, wanawake wengine saba wameteuliwa na vyama vyao kugombea nafasi ya makamu wa Rais Tanzania.

Wanawake waliosimama kuwania nafasi hizo ni Chausiku Khatib Mohamed wa NLD, Devotha Minja wa Chaumma, Chumu Abdallah (AAFP) na Azza Haji Suleiman (Demokrasia Makini). Wengine ni Fatma Abdulhabib Fereji wa ACT-Wazalendo, Husna Abdallah wa CUF, Dk Evaline Munisi (NCCR-Mageuzi) na Amana Suleiman Mzee (TLP).


Vigogo waliokosekana

Kwa Wazanzibari na watetezi wa demokrasia nchini, jina la Maalim Seif lilihusishwa moja kwa moja na mapambano ya siasa zenye misimamo mikali.

Aliibuka kama kiongozi mwenye ushawishi mkubwa visiwani Zanzibar, akiweka historia ya mapambano yaliyosababisha mabadiliko ya kisheria na kuanzishwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Maalim Seif aligombea urais wa Zanzibar mara tano mfululizo kuanzia mwaka 2000 hadi 2020 kupitia  Chama cha Wananchi (CUF) na baadaye ACT-Wazalendo na kila mara alishika nafasi ya pili nyuma ya mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Alibaki kuwa nembo ya upinzani kwa kuamini kura ni silaha halali ya mabadiliko.

Kifo chake mwaka 2021 kilipunguza kwa kiasi kikubwa nguvu za ACT-Wazalendo na harakati za kidemokrasia Zanzibar.

Uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa kwanza tangu wa 1995; kufanyika bila jina lake katika mabango ya kisiasa.


Profesa Lipumba

Kwa upande wa Tanzania Bara, Profesa Ibrahim Lipumba alijulikana kama injini ya CUF.

Mwanazuoni huyu wa uchumi aliyeacha kazi ya kimataifa katika Benki ya Dunia, aliingiza usomi na tafakuri za kiuchumi kwenye siasa za upinzani.

Kwa miongo kadhaa akiwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba alisimama mara tano kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akibeba ajenda za mageuzi ya uchumi na mgawanyo sawa wa rasilimali.

Umaarufu wake ulipanda zaidi katika chaguzi za mwaka 2000 na 2005 aliposhika nafasi ya pili mfululizo nyuma ya wagombea wa CCM.

Hata hivyo, mwaka huu kwa mara ya kwanza tangu 1995, jina lake halitaonekana kwenye kinyang’anyiro baada ya kutokuchukua fomu ya kugombea, badala yake, amewatambulisha Samandito Gombo na Husna Abdallah kama wagombea wa urais wa CUF.

“Mimi sijagombea mwaka huu, lakini tumewaleta wagombea bora zaidi. Wanaoniunga mkono wanapaswa kuwaunga mkono wao pia,”amesema Profesa Lipumba alipozungumza na Mwananchi.

Hata hivyo, unapozungumzia siasa za Tanzania, huwezi kuiachahistoria ya NCCR-Mageuzi iliyokuwa ikiongozwa na mwenyekiti wake, James Mbatia.

Mbatia alijulikana kwa utulivu wake na ushawishi wa hoja. Umaarufu wake ulimfanya Rais mstaafu Jakaya Kikwete kumteua kuwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia nafasi za uteuzi wa Rais.

Hata hivyo, tangu mwaka 2022, chama hicho kimekumbwa na migogoro ya kiuongozi iliyomweka kando.

Mgawanyiko huo umeendelea hadi sasa, kundi jingine linaandaa uchaguzi mkuu likiwa halimtambui tena kama mwenyekiti wa chama hicho. Hivyo basi, uchaguzi wa 2025 hautaona jina wala taswira ya Mbatia kwenye mabango ya kisiasa.

Kwa zaidi ya miaka 30, jina la Freeman Mbowe lilihusishwa moja kwa moja na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Alijiunga na chama hicho akiwa kijana na baadaye akawa mwenyekiti kwa muda mrefu, akiiongoza Chadema kufikia kilele cha umaarufu wake.

Mwaka 2005, Mbowe aliwania urais wa Tanzania na kushika nafasi ya tatu nyuma ya wagombea wa CCM na CUF. Chini ya uongozi wake, Chadema iligeuka kuwa tishio kwa CCM, ikiunda Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni baada ya chaguzi za mwaka 2010 na 2015.

Hata hivyo, baada ya kushindwa kutetea uenyekiti wa chama katika uchaguzi wa ndani uliompa ushindi Tundu Lissu, Mbowe amekuwa kimya katika siasa.

Uchaguzi wa mwaka huu unafanyika huku sauti yake ikikosekana majukwaani, jambo linaloibua maswali mengi kwa wafuasi na wachambuzi wa siasa.

Kwa upande wa, Mwenyekiti wa sasa wa Chadema, Tundu Lissu naye hayupo kwenye mbio za mwaka huu. Kukosekana kwake kunatokana na msimamo wa chama chake wa kutoshiriki uchaguzi bila maboresho ya sheria za uchaguzi, pamoja na yeye kukabiliwa na kesi za jinai katika Mahakama Kuu.

Lissu anayejulikana kwa hoja kali kuhusu haki, Katiba na mageuzi ya kisheria, kwa mara nyingine anakosa nafasi ya kuzungumza na wafuasi wake majukwaani, hali inayopunguza nguvu ya upinzani katika uchaguzi wa mwaka huu.

Unapozungumzia siasa za Tanzania, huwezi kuacha kulitamka jina la Fahmi Dovutwa. Huyu aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha UPDP na alijipatia umaarufu kupitia ucheshi na vioja vyake majukwaani ambaye pia kwa mwaka huu hataonekana.

Tangu kupokwa uongozi wa chama mwaka 2019, hajajitokeza tena kwenye siasa za kitaifa. Hivyo, uchaguzi wa 2025 utapita bila taswira ya Dovutwa katika kinyang’anyiro cha urais.

Hata hivyo, historia ya vyama vingi nchini haiwezi kuandikwa bila jina la Augustine Mrema. Italumbukwa mwaka 1995, akiwa mgombea wa NCCR-Mageuzi, alikitikisa chama tawala kwenye uchaguzi mkuu kwa kushika nafasi ya pili nyuma ya mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa.

Lakini baadaye alikihama chama hicho na kuhamia Chama cha Tanzania Labour Party (TLP) alikoendelea kugombea urais mara kadhaa. Ingawa alibaki kwenye siasa hadi mauti yalipomkuta Agosti 21, 2022.

Uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa kwanza kufanyika bila ya sauti ya Mrema, mwanasiasa aliyejulikana kwa sera na maneno makali ya mabadiliko.

Mwenyekiti wa muda mrefu wa UDP, John Cheyo, anafahamika kwa kauli zake tata na utani uliopamba siasa za Bunge, maarufu kwa misemo kama “visenti” na “mapesa.”

 Kwa miongo kadhaa, jina lake halikuwahi kukosekana katika majukwaa ya kampeni za kuomba kura za urais wakati wa uchaguzi mkuu,  ama akijinadi au akinadi wagombea wa chama chake sambamba na mgombea mwenza wake.

Hata hivyo, kutokana na umri na hali ya afya, mwaka huu Cheyo amebwaga manyanga hali inayoashiria mwanzo wa kujitenga kwake na siasa za moja kwa moja.

Unapomtaja Cheo, ni wazi pia Hashimu Rungwe, Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) hatobaki nyuma.

Rungwe ambaye pia katika kinyang’anyiro cha mwaka huu, hayumo. Rungwe amejibebea umaarufu kutokana na sera zake za kipekee zenye mvuto akiwa majukwaani.

Miongoni mwa sera aliyokuwa akiinadi kila akipanda majukwaani kujinadi, Rungwe alikuwa na kauli mbiu yake iliyoota mizizi hadi sasa na kumpatia umaarufu mkubwa ya ‘Ubwabwa kwa wote’ na akajikuta akipachikwa jina la mzee wa ubwabwa.

Mwaka huu, amejiweka kando baada ya  kuwapa nafasi vijana waliojiunga na chama chake wakitokea Chadema.

Rungwe alipozungumzia hilo, ameeleza furaha yake baada ya chama chake kuwateua Salim Mwalimu na Devotha Minja akisema huu ni wakati wa vijana nay eye anapumzika.

“Ninaamini vijana hawa watakifikisha chama chetu na Tanzania kwenye nchi ya ahadi tuitakayo,” amesema Rungwe kauli aliyoitoa wakati akiwatangaza wagombea hao na kuirudia tena alipozungumza na Mwananchi.

Aliyekuwa kiongozi wa Chama cha DP, Christopher Mtikila alikuwa miongoni mwa wanasiasa waliotumia hoja nzito, mbinu za kisheria na hata ucheshi na kujijengea jina kubwa kisiasa.

Mtikila (marehemu), alikuwa kila akipanda kwenye majukwaa ya kampeni za urais, alikuwa akisisitiza ndoto ya kuirejesha Tanganyika ndani ya Muungano.

Lakini mwaka huu sauti hiyo haipo tangu alipoaga dunia kwa ajali ya gari mwaka 2015.

Hivyo basi, uchaguzi wa mwaka huu unaendelea bila ya sauti yake majukwaani.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa National League for Democracy (NLD), Emmanuel Makaidi anakumbukwa kwa hotuba zake kali, hususan wakati wa Bunge Maalumu la Katiba.

Katika siasa za mwaka 2015, alijiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), akionekana kama mmoja wa wapinzani waliopigania mageuzi ya Kikatiba na kidemokrasia.

Makaidi alifariki dunia na hivyo mwaka huu, sauti yake pia haipo kwenye majukwaa ya kisiasa.


Kauli za wachambuzi wa siasa

Wataalamu wa siasa nchini wamesema kutokuwapo kwa baadhi ya wanasiasa wakongwe katika Uchaguzi Mkuu wa 2025 si jambo la kushangaza.

Hata hivyo, wamesema hali hiyo haiwezi kubezwa kutokana na nafasi kubwa waliyokuwa nayo katika vyama vyao na ushawishi walioujenga kwa muda mrefu.

Mtaalamu wa Siasa na Utawala Bora kutoka Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA), Profesa Mohammed Makame amesema mabadiliko katika siasa ni jambo la lazima kuanzia ngazi ya viongozi, sheria na mwelekeo wa nchi.

Hata hivyo, amesema cha muhimu zaidi ni dira ya chama na mwendelezo wa maono ya waasisi wake kwa wanaorithi nafasi zao.

“Mabadiliko yataendelea kutokea si tu kwa watu, bali pia katika sheria za uchaguzi, Katiba na mwelekeo wa vyama. Wazee kuhudumu kisha kukaa kando si jambo la ajabu, lakini si la kupuuzwa,” amesema Profesa Makame.

Amesema jukumu kubwa la viongozi wapya na wafuasi wao ni kuenzi misingi waliyoachiwa na waasisi ili kulinda Taifa lenye utulivu na siasa zinazojengwa kwa misingi ya amani.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Paul Loisulie amesema kwa Zanzibar hana sababu ya kuona pengo la kisiasa baada ya kutokuwapo kwa Maalim Seif, akieleza kuwa wafuasi wa vyama visiwani humo ni watu wenye msimamo thabiti kwenye ajenda zao.

“Uzuri wa Zanzibar ni kwamba, wafuasi wa vyama hawaongozwi na upepo wa kisiasa. Wakiamua kujiunga na chama fulani wanabaki hapo na wakibaki wanabaki kwa msimamo mmoja. Hivyo, kutokuwapo kwa Maalim Seif hakutaathiri upinzani. Wanasiasa wapya wengi wamelelewa na Seif, kwa hiyo ACT bado ipo imara,” amesema Dk Loisulie.

Naye Mtaalamu wa Siasa na Utawala Bora kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda amesema Watanzania inapaswa kufahamu kuwa, mabadiliko ni sehemu ya maisha ya watu na kisiasa, hivyo viongozi wanapaswa kuandaa vijana wa kubeba ajenda za vyama vyao kwa mustakabali wa Taifa.

“Mabadiliko lazima yawepo. Swali ni viongozi wanaoondoka wamewaandaa vipi watu wa kurithi dira za vyama vyao,” amesema Dk Mbunda.

Amesema changamoto kubwa ni kwamba, viongozi wengi wa vyama hawawaandai vijana ipasavyo, hali inayovifanya vyama hivyo kurudi nyuma kila mara wanapojitenga na siasa.

Ametoa mfano akisema, “Profesa Lipumba aliwaandaa vijana kama kina Mtatilo, lakini leo hawapo CUF. Vivyo hivyo, Mbowe aliwahi kulea vijana wengi lakini, wameishia kuhamia vyama vingine.”

 “Mabadiliko ni jambo endelevu. Tutaendelea kushuhudia sura mpya zikiibuka zenye fikra mbadala. Jamii lazima iache kuishi kwa mazoea kwani kila hatua ya mabadiliko inaleta fursa mpya na mawazo mapya,” amesema.

Kwa mujibu wa wachambuzi hao, demokrasia ndiyo imekuwa ikiamua mwelekeo wa kisiasa, na ongezeko la wanawake katika nafasi za juu ni dalili njema kwamba, jamii inazidi kupata uelewa wa masuala ya kisiasa na kijamii.