Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vitongoni 97 Mpimbwe kuunganishiwa umeme, Dk Nchimbi asema...

Muktasari:

  • Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amefanya mikutano mkoani Rukwa na Katavi ya kukutafutia kura chama hicho katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025

Mlele. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimeahidi vitongoji vyote 97 vya Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, Mkoa wa Katavi kuunganishiwa umeme ndani ya miaka mitano ijayo.

Pia, kimesema chama hicho kitaendelea kijikita kugusa sekta mbalimbali za afya, elimu, maji, kilimo na mifugo zinazokwenda kukuza uchumi wa Taifa na wananchi hususan vijana.

Ahadi hizo zimetolewa leo Jumanne, Septemba 9, 2025 na mgombea mwenza wa urais wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi katika mkutano wa kampeni uliofanyika Majimoto, Jimbo la Kavuu, Mkoa wa Katavi.

Mkutano huo, umetumika kueleza mambo waliyofanya miaka mitano iliyopita, wanayopanga kufanya na kumwombea kura mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani wa chama hicho.

Amesema ahadi hizo zitatekelezwa iwapo tu wananchi wa halmashauri hiyo ya Mpimbwe na mkoa mzima wa Katavi, watakichagua chama hicho katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.

"Chama cha Mapinduzi, hakijapoteza dhamira yake ya kuwatetea, kuwaongoza na kuwaletea maendeleo Watanzania. Tumepita wilaya na mikoa mbalimbali wanasema hakuna cha kumlipa Samia zaidi ya kusema Oktoba tunatiki," amesema Dk Nchimbi.

Amesema mwaka 2020 vijijini vilivyokuwa na umeme vilikuwa 25 sasa ni vitatu, vitongozi 38 sasa 135 vina umeme.

"Mkimchagua mama Samia, tunakwenda kumalizia vitongoji vipya 97 ambavyo havina umeme na hivi vitakamilika miaka mitano ijayo. Kikubwa tupeni kura," ameahidi Dk Nchimbi.

Amesema katika miaka mitano iliyopita, wamejenga Hospitali ya Wilaya ya Mlele; zahanati zilikuwa nane sasa ziko 14, vituo vya afya vilikuwa vitatu sasa viko vinane, shule za msingi 18 zimejengwa, za sekondari zilikuwa tano sasa zipo 15.

Dk Nchimbi amesema Sh6.6 bilioni zimetumika kujenga vituo vipya vya kusangambaza maji zaidi ya 300 na vimesababisha upatikanaji wa maji kufikia asilimia 64.

Eneo la barabara amesema, kulikuwa na kilomita mbili za lami kwenye halmashauri hiyo sasa zipo 17 na wanakwenda kuongeza zingine zaidi ya kumi.

"Mkituchagua, tunakwenda kujenga ICU kwenye hospitali yetu ya wilaya ili wagonjwa wanaohitaji uangalizi zaidi waweze kuhudumiwa hapo. Zahanati sita tutajenga na tunakusudia kujenga vituo vipya vinne vya afya," amesema Dk Nchimbi.

Amesema watajenga shule mpya za msingi 11 na za sekondari nne, barabara kwa kiwango cha changarawe zitajengwa kilomita 204 na minada mipya ya mifugo itaanzishwa.

Katika mkutano huo, aliyekuwa mbunge wa Kavuu, Godfrey Pinda amesema atakuwa mstari wa mbele kutafuta kura za Samia, wabunge na madiwani.

"Lazima niwe mbele, tutafute kura za mama usiku na mchana, tukatafute kura za mbunge na diwani na mimi niko na ninyi," amesema Pinda ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Pinda ameshindwa kwenye kura za maoni ndani ya CCM kuwania kutetea nafasi hiyo. Anayegombea sasa ni Laurent Luswetula ambaye amewaomba wamchague ili akawakilishe vyema.

Baada ya Pinda kumaliza kuzungumza, Dk Nchimbi akasema,"watu wanaojua maadili ya chama chetu."

Awali, asubuhi ya leo Jumanne, amefanya mkutano wa kampeni Sumbawanga Mjini, Mkoa wa Rukwa amesema malengo ya CCM ni kuboresha maisha ya Watanzania na kuwa na Taifa lenye kujitegemea, na hilo litafanikiwa ikiwa Samia atachaguliwa kuendelea kubaki madarakani.

Dk Nchimbi amezungumzia maendeleo yaliyofanywa na Samia ikiwamo uboreshaji wa Bandari ya Kasanga, Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga na utoaji mikopo kwa makundi maalumu.

Amesema chama kimejipanga kusimamia na kuimarisha huduma za afya kwa wajawazito na watoto, ili kudhibiti na kumaliza vifo vya kinamama wakati wa kujifungua kutoka asilimia 9 hadi 4.

Pia, amesema watapunguza udumavu kwa watoto wa chini ya miaka mitano na kuongeza huduma za lishe kwa makundi yanayoathirika zaidi, ikiwa ni pamoja na watoto, wajawazito na vijana balehe.

“Licha ya Mkoa wa Rukwa kulima mazao ya chakula na biashara, changamoto ya udumavu ni kwa asilimia 49.8, na tutahakikisha tunapunguza tatizo,” amesema Dk Nchimbi.

Kwa upande wake, Agnes Lyoba, aliyekuwapo mkutanoni, akizungumza na Mwananchi amesema anawaomba wagombea kutimiza wanayoyaahidi ili waendelee kuaminika.

“Niombe tu wagombea kutimiza ahadi zao, sio kuongea tu ili wapate kura, bali tunatamani kuona utekelezaji wake,” amesema Agnes.

Katika mkutano uliofanyika jioni ya jana, Jimbo la Kalambo mkoani humo, Dk Nchimbi alisema chama hicho kitaisimamia Serikali kumalizia uunganishaji wa umeme kwenye vitongoji vyote vilivyobakia.

Amesema wataisimamia Serikali kukamilisha Mradi wa Taza unaohusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Iringa hadi Sumbawanga na kuunganisha nchi za Tanzania na Zambia.

“Mradi huu pia utahusisha ujenzi wa vituo vya kupooza umeme katika Wilaya ya Sumbawanga, Kalambo na Nkasi,” amesema Dk Nchimbi.

Amesema wataimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala na kuongeza upatikanaji wa gesi asilia katika viwanda, taasisi, majumbani na kwenye magari.