Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vodacom, TCDC kuimarisha ushirika kwa teknolojia

Mkurugenzi wa Biashara wa Vodacom Tanzania, Nguvu Kamando (wa pili kulia), akikabidhi kompyuta mpakato moja kati ya 35 zilizotolewa kwa Mrajisi wa Vyama vya Ushirika, Dk Benson Ndiege (wa pili kushoto), wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili kuhusu matumizi ya teknolojia ya kidijitali katika vyama vya ushirika kupitia jukwaa la M-Kulima.


Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Vodacom, ushirikiano huo pia utaweka mkazo katika mafunzo kwa viongozi wa vyama vya ushirika ili kuongeza ujuzi wa matumizi ya teknolojia na kuimarisha uwezo wao wa kiutendaji.

Dar es Salaam. Wakulima na wanachama wa vyama vya ushirika nchini wanatarajiwa kunufaika zaidi na huduma za kifedha na kidijitali kufuatia ushirikiano mpya kati ya Vodacom Tanzania PLC na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) unaolenga kuimarisha matumizi ya teknolojia katika sekta ya ushirika.

Kupitia makubaliano ya ushirikiano (MoU) yaliyosainiwa jijini Dar es Salaam Juni 5, 2026, taasisi hizo zitaunganisha nguvu katika kusajili vyama vya ushirika na wanachama wake kidijitali kupitia jukwaa la M-Kulima, hatua inayolenga kuongeza uwazi, ufanisi wa shughuli na ujumuishwaji wa kifedha kwa wakulima.

Mbali na kusaini makubaliano hayo, Vodacom Tanzania imekabidhi kompyuta mpakato (laptop) 35 kwa TCDC ili kusaidia utekelezaji wa shughuli za kidijitali na kuongeza uwezo wa taasisi hiyo katika kutoa huduma.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini, Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando, alisema ushirikiano huo ni sehemu ya juhudi za kampuni hiyo kutumia teknolojia kuleta mabadiliko chanya kwa jamii na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Alisema kupitia mfumo wa M-Kulima, vyama vya ushirika vitapata huduma mbalimbali zikiwemo usajili wa wanachama, malipo ya fedha kidijitali, huduma za akiba na mikopo pamoja na suluhisho nyingine za kidijitali zitakazosaidia kukuza shughuli zao.

“Tunaziwezesha taasisi za ushirika kwa kuwapatia zana na huduma za kidijitali zitakazoongeza ufanisi wa kiutendaji, kuboresha uwazi na kuwawezesha wakulima kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa kilimo,” alisema Kamando.

Kwa mujibu wa Vodacom, ushirikiano huo pia utaweka mkazo katika mafunzo kwa viongozi wa vyama vya ushirika ili kuongeza ujuzi wa matumizi ya teknolojia na kuimarisha uwezo wao wa kiutendaji.

Naye Msajili wa Vyama vya Ushirika na Afisa Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dk Benson Ndiege, alisema mabadiliko ya kidijitali ni nyenzo muhimu katika kuviwezesha vyama vya ushirika kuendana na mahitaji ya sasa ya uchumi.

Alisema matumizi ya teknolojia yataongeza uwajibikaji, kuboresha utoaji wa huduma na kuongeza thamani kwa wanachama wa vyama hivyo, hususan wakulima ambao ni mhimili muhimu wa uchumi wa Tanzania.

“Mabadiliko haya yatawezesha vyama vya ushirika kujiendesha kwa ufanisi zaidi na kuwafikia wanachama kwa huduma bora na za kisasa,” alisema Dk Ndiege.

Jukwaa la M-Kulima, ambalo limeundwa mahsusi kwa ajili ya vyama vya ushirika na wakulima, linatoa huduma za usajili wa wakulima, ukusanyaji wa mazao, malipo ya kidijitali pamoja na huduma za kifedha kama mikopo, akiba, bima na uwekezaji.

Takwimu za Vodacom zinaonyesha kuwa hadi sasa mfumo huo umesajili zaidi ya wakulima milioni 3.2 na kuchakata malipo yenye thamani ya zaidi ya Sh88 bilioni kwa wakulima zaidi ya 325,000, jambo linaloonyesha kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia katika sekta ya kilimo nchini.