Vodacom: Ulinzi wa taarifa unalinda fedha za watumiaji wa huduma za kidijitali
Mkurugenzi wa Udhibiti wa Hatari na Utii wa Sheria wa Vodacom Tanzania PLC, Olaf Mumburi (wa pili kushoto), akizungumza wakati wa Mkutano wa Kwanza wa Mwaka wa Ulinzi wa Faragha na Taarifa Binafsi uliofanyika jijini Dar es Salaam. Mumburi alikuwa mmoja wa wajadili katika mada kuhusu ulinzi wa taarifa za kifedha na uchumi wa kidijitali, pamoja na Wakili Dirontsho Mohale wa Baakaedi Professional Practice (Pty) Ltd, Afrika Kusini (kushoto), Mwakilishi wa Stanbic Bank Tanzania, Winston Ishengoma (wa pili kulia), na Mwakilishi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Abdallah Thabiti (kulia).
Dar es Salaam. Kampuni ya Vodacom Tanzania imesema kuimarisha ulinzi wa taarifa binafsi za wateja ni hatua muhimu katika kulinda fedha za watumiaji wa huduma za kidijitali na kujenga imani inayochochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.
Kauli hiyo ilitolewa wakati wa Mkutano wa Kwanza wa Mwaka wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi uliofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 29 hadi Julai 1, 2026, ukiratibiwa na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), ambapo kampuni hiyo ilikuwa miongoni mwa wadhamini wakuu wa mkutano huo.
Akizungumza katika mdahalo kuhusu ulinzi wa taarifa za kifedha, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Hatari na Utii wa Sheria wa Vodacom Tanzania, Olaf Mumburi, alisema taasisi zinazotoa huduma za kidijitali zinapaswa kuendelea kuwekeza katika mifumo salama ya usimamizi wa taarifa ili kuwalinda wateja dhidi ya hatari zinazoweza kuhatarisha fedha na taarifa zao.
Alisema kadri matumizi ya huduma za kifedha kupitia simu na majukwaa ya kidijitali yanavyozidi kuongezeka, ndivyo umuhimu wa kulinda taarifa binafsi unavyoongezeka ili kuimarisha imani ya watumiaji na kuhakikisha huduma hizo zinaendelea kukua kwa usalama.
"Tunahitaji mifumo madhubuti ya usimamizi wa taarifa binafsi ili kujenga mazingira salama kwa watumiaji wa huduma za kidijitali. Imani ya mteja ndiyo msingi wa ukuaji wa uchumi wa kidijitali," alisema Mumburi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Idara ya Taarifa Binafsi wa Vodacom Group kutoka Afrika Kusini, David Smuts, alisema Maofisa wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi (DPOs) wana jukumu kubwa la kuhakikisha taasisi zinatumia taarifa za wateja kwa uwajibikaji, uwazi na kwa kuzingatia sheria.
Alisema ulinzi wa taarifa binafsi haupaswi kuonekana kama wajibu wa kufuata sheria pekee, bali ni nyenzo muhimu ya kujenga uaminifu kati ya taasisi na wateja wake.
Naye Mkuu wa Idara ya Usalama wa Mtandao wa Vodacom Tanzania, Joel Kazoba, alisema maendeleo ya teknolojia na ubunifu yanapaswa kwenda sambamba na mifumo imara ya kulinda faragha za watumiaji.
Alisema uaminifu wa wateja hujengwa kupitia uwazi wa namna taarifa zao zinavyokusanywa, kuhifadhiwa na kutumiwa pamoja na uwepo wa mifumo salama ya usalama wa mtandao.
Mkutano huo ulioongozwa na kaulimbiu "Ulinzi wa Taarifa Binafsi kama Nguzo ya Kujenga Mustakabali wa Kidijitali Jumuishi kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050," uliwakutanisha wadhibiti wa sekta, wataalamu wa teknolojia, taasisi za kifedha, wataalamu wa sheria na watunga sera kutoka Tanzania na mataifa mengine ya Afrika kujadili namna ya kuimarisha ulinzi wa taarifa binafsi katika zama za mageuzi ya kidijitali.
Mbali na kushiriki mijadala hiyo, Vodacom Tanzania ilitunukiwa tuzo maalumu ya udhamini kutoka Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), ikiwa ni kutambua mchango wake katika kufanikisha mkutano huo na kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia pamoja na uelewa wa masuala ya ulinzi wa taarifa binafsi nchini.