Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vyama mguu sawa bajeti za kampeni

Muktasari:

  • Kampeni za uchaguzi mkuu zitaanza Agosti 28 hadi Oktoba 28, 2025 huku wagombea wa urais wakiendelea kuchukua fomu Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC)

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimelenga kukusanya Sh100 bilioni kutoka kwa makada, wafuasi na wadau wake kwa ajili ya kampeni za uchaguzi, huku Chama cha National League for Democracy (NLD) kikilenga kutumia Sh5 bilioni katika kampeni.

Ukiacha maandalizi ya CCM na NLD, Chama cha Demokrasia Makini, kimelenga kukusanya na kutumia Sh570 milioni kwa ajili ya kampeni za uchaguzi huo, unaotarajiwa kufanyika Jumatano ya Oktoba 29, mwaka huu.

Kampeni za uchaguzi huo zitaanza Agosti 28 hadi Oktoba 28, 2025. Tayari vyama mbalimbali vinaandaa wagombea udiwani na ubunge huku wa urais wagombea wanaendelea kuchukua fomu Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Wakati vyama hivyo vikiwa katika hatua hiyo, vipo vingine, vinavyosema bado havijapanga bajeti zitakazozitumia katika kampeni za urais wa uchaguzi huo na kwamba vipo katika hatua ya kuratibu jambo hilo.

Hata hivyo, kiasi kilichopangwa kukusanywa na CCM, hakikuwekwa wazi kuwa ndiyo gharama rasmi za kampeni za uchaguzi huo, isipokuwa ni fedha inayolengwa kukusanywa kupitia harambee itakayofanyika kesho Jumanne, Agosti 12, 2025 katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.


Harambee ya CCM

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, leo Jumatatu, Agosti 11, 2025, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amesema chama hicho kinafanya hivyo kwa kuwa kinatambua wakati wa kampeni kunahitajika fedha.

“Chama kinapokwenda kwenye maandalizi ya kampeni hata CCM huwa tunajiandaa, kwa maana ya kuwa na nguvu ya fedha, magari, mabango, mafuta na vitu vingine,” amesema.

Kwa kutambua hilo, ameeleza Kamati Kuu iliamua chama hicho kianze harambee ya kutafuta fedha inayotarajiwa kufanyika Agosti 12, katika Ukumbi wa Mlimani City na mgeni rasmi ni Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan.

"Kesho ndio ile siku ambayo wana-CCM wenye uchungu na chama chao kukusanya michango na wanayo masaa takribani 28 kuanzia muda huu hadi tunapoingia kwenye ukumbi kuonesha nguvu na mapenzi yao kwa chama chao," amesema.

Katika harambee hiyo, amesema chama hicho kinalenga kutafuta Sh100 bilioni kwa ajili ya kampeni, huku akivialika vyama vingine pia kuchangia.

“Haihitaji ufanisi wa kipolisi kujua CCM inawatumikia watu wote, vikiwamo vyama vya upinzani. Kwa hiyo vichangie chama ambacho kimekuwa kikiwahudumia bila tatizo,” ameeleza.

Amesema kuchangia kampeni kwa kawaida hutolewa hadi karibu na siku ya kupiga kura, lakini wanatamani ndani ya saa 24 wanachama waoneshe nguvu kwa chama chao.

Kuhusu udhibiti wa fedha haramu, amesema jitihada zao ni kujiepusha kuwa sio kazi ya CCM kudhibiti fedha haramu, hivyo wataviachia vyombo vya dola viifanye kazi hiyo.

Hata hivyo, ameeleza wataruhusu michango kutoka kwa wachangiaji ambao hawatakuwa sababu ya kupotea kwa uhuru wa Watanzania.

Amesisitiza kwa watiania wanaosubiri uteuzi wa kwenda kugombea, michango hiyo haitakuwa sababu ya kuteuliwa au kutoteuliwa.

“Vikao vya kamati ya maadili vimeshakaa na haiwezekani kuita kikao cha dharura kujadili watu waliochangia,” amesema.


Vyama vingine

Akizungumzia hilo, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Bara, Issihaka Mchinjita amesema kwa kuwa ndiyo kwanza chama chake kimetoka kufanya mkutano mkuu, bado hakijaanza mkakati wa ukusanyaji wa bajeti za kampeni.

Lakini, amesema chama hicho kitaandaa programu maalumu ya kukusanya fedha kwa ajili ya kampeni na itatangazwa hadharani kwa ajili ya wanachama kuchangia.

"Tutazindua ilani yetu ya uchaguzi, pia tutazindua programu ya kukusanya fedha za kampeni. Wanachama watachangia kama ambavyo CCM wametangaza nasi hivi karibuni tutatangaza programu yetu," ameeleza.

Mchinjita amesema wamejipanga vema kuhakikisha wanashiriki na kushinda uchaguzi huo, kwa kutumia vyanzo vyote stahiki kwa mujibu wa sheria.

Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hashim Rungwe maarufu Mzee wa Ubwabwa amesema bado chama chake hakijaweka wazi kiasi hicho kilichopangwa kutumika.

Amesema wanaendelea na michakato ya kuhakikisha inajulikana na namna itakavyopatikana ili shughuli za kampeni zifanyike vizuri.

“Bado hatujajua kwa sasa, lakini tunaratibu, tukishajua tu lazima tutawaambia,” amesema Rungwe ambaye tayari chama chake kimewatangaza Salum Mwalimu na Devotha Minja kugombea urais na Makamu.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Husna Abdalla Mohamed amesema wapo katika maandalizi ya bajeti ya jumla ya kampeni za uchaguzi wa rais, hivyo bado haijajulikana.

“Tuliandaa ya kwanza, lakini tunaitengeneza rasmi na kwa sasa haijakamilika. Hivyo, naomba baada ya kukamilika, tutaweka wazi ni kiasi gani tunatarajia kutumia,” amesema.

Katibu Mkuu wa Chama cha UMD, Moshi Kigundula amesema suala la bajeti kwa sasa ni vigumu kwa sababu ndiyo kwanza wamechukua fomu ya uteuzi.

Amesema watatazama bajeti kulingana na maeneo waliyoyaweka kipaumbele kwenda kufanya kampeni za uchaguzi huo.

“Tukirudi Dar es Salaam, tutaangalia maeneo ya kufanyia kampeni hasa yale ya kipaumbele na bajeti yetu itajulikana kwa kutambua hilo,” amesema.

Katibu Mkuu wa NLD, Doyo Hassan amesema chama chake kimepanga kutumia kiasi cha Sh5 bilioni kwa ajili ya kufanya kampeni na uendeshaji.

“Sisi mwaka huu tumepanga kutumia Sh5 bilioni kwa ajili ya kampeni za uchaguzi na uendeshaji wake. Tunaamini ni kiasi kitakachofanikisha kumaliza kabisa kampeni,” amesema Doyo.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia Makini, Coaster Kibonde amesema chama hicho kimepanga bajeti ya Sh570 milioni kwa ajili ya shughuli za kampeni na uchaguzi wenyewe.

“Sisi tumejipanga mapema, tutatumia Sh570 milioni kwa ajili ya kampeni za uchaguzi. Ni uchaguzi ambao tumejipanga kushinda, lakini bado hatujajaza fomu za bajeti ya uchaguzi,” amesema Kibonde ambaye pia ni mgombea wa urais kwa tiketi ya chama hicho.

Mwenyekiti Chama cha Kijamii (CCK) ambaye pia ni mgombea wa urais kupitia chama hicho, David Mwaijojele amesema masuala ya bajeti yatajulikana baada ya kurudi Dar es Salaam.

Amesema kwa sasa yupo mkoani Dodoma kwa ajili ya shughuli za uchukuaji fomu katika Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), tukio litakalofuatiwa na kujulikana kwa masuala ya bajeti.

“Nikirudi Dar es Salaam nitakutafuta kisha nitakwambia ni kiasi gani kimepangwa. Kwa sasa nipo Dodoma na tupo kuchukua fomu, lazima nikirudi tutakaa kisha tutakupa taarifa,” ameeleza Mwaijolele.

Mwenyekiti wa Chama cha ADC, Shaban Itutu amesema bado ndani ya chama chake haijajulikana ni kiasi gani kitatumika kwa ajili ya kampeni za urais.

Kwa kuwa, ndiyo kwanza wamezindua ilani ya uchaguzi ya 2025/30, amesema suala la bajeti litajulikana baada ya vikao vya uongozi.

Amesisitiza kuwa, itakuwa bajeti itakayotosheleza shughuli za kampeni za uchaguzi huo.

“Tutapanga fedha za kutosha kukamilisha kila kitu. Kwa sasa bado hatujakaa kupanga bajeti ya jambo hilo,” amesema Itutu.