Waeleza matokeo sekta muhimu kutotengewa fedha za kutosha
Baadhi ya wachumi nchini Pakistan wametaja mambo matano yatakayolikumba Taifa hilo kutokana na uamuzi wa serikali kutenga kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya sekta ya ulinzi huku sekta nyingine zikisahaulika.
Wametaja mambo hayo kuwa ni kudorora kwa sekta ya afya na elimu, kuporomoka kwa uzalishaji, mzigo wa kodi na tozo kwa wananchi, madeni makubwa na kushuka kwa fursa za ajira.
Katika bajeti iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha, Muhammad Aurangzeb, serikali imeongeza matumizi ya ulinzi kwa karibu asilimia 18 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Wakizungumzia uamuzi huo, Profesa Idolf Bilal alisema, ‘’Fedha zinazopelekwa jeshini ni wazi kuwa zimekatwa kutoka kwenye huduma za msingi za jamii na maana yake hospitali zitakosa huduma muhumi, shule kukosa walimu na vitabu.’’
Alisema ukuaji wa uchumi wa muda mrefu hutegemea miradi ya maendeleo, ‘’bajeti kubwa ya ulinzi inapunguza fedha za miradi hii jambo linalosababisha uchumi kukosa nguvu, wawekezaji kukimbia nchi kwa sababu ya miundombinu mibovu na mazingira magumu ya biashara.’’
Naye Dk Muhammad Ahmed alisema uamuzi huo utaongeza mzigo wa kodi na tozo kwa wananchi, ‘’ili kugharamia jeshi kubwa na ununuzi wa silaha za kisasa, serikali italazimika kutafuta vyanzo vingine vya mapato hivyo itaongeza kodi na hapo kunakuwa na hatari ya umasikini kuongezeka.’’
Mchumi mwingine Ali Mustafa alisema nchi nyingi zinazoweka msisitizo mkubwa kwenye ulinzi hukabiliwa na uhaba wa fedha za ndani na kulazimika kukopa na kuingia kwenye mtego wa madeni.
‘’Tofauti na kuwekeza kwenye viwanda, kilimo au teknolojia ambako maelfu ya ajira mpya zinazalishwa, sekta ya ulinzi haisambazi ajira kwa jamii nzima. Uwekezaji mkubwa wa fedha katika sekta hii unazuia sekta binafsi kukua,’’ alisema Mustafa.