Wakulima waomba ruzuku ya matrekta kuongeza tija ya kilimo
Muktasari:
- Baadhi ya wakulima wa kanda ya kaskazini wameiomba Serikali kutoa ruzuku kwa matrekta na vifaa vya kisasa vya kilimo wakisema hatua hiyo itawawezesha wakulima wadogo kumudu gharama za teknolojia hizo, kuongeza uzalishaji wa mazao na kuimarisha mchango wa sekta ya kilimo katika uchumi wa taifa.
Arusha. Baadhi ya wakulima wa kanda ya kaskazini wameiomba Serikali kuweka utaratibu wa kutoa ruzuku kwa matrekta na vifaa vya kisasa vya kilimo ili kuwasaidia wakulima wadogo kupata teknolojia zinazoweza kuongeza tija na uzalishaji wa mazao nchini.
Wakulima hao wanasema licha ya uwepo wa teknolojia za kisasa za kilimo nchini, gharama za kuzipata bado ni kubwa kwa wakulima wengi wadogo, hali inayozuia juhudi za kuongeza uzalishaji na kuifanya sekta ya kilimo kuwa na ushindani zaidi.
Ombi hilo lilitolewa jana wakati wa uzinduzi wa ofisi za tawi la Kampuni ya Mobikey Agri Machinery Arusha uliofanyika katika Kata ya Kikatiti, Mkoa wa Arusha.
Akizungumza kwa niaba ya wakulima wenzake, Diwani wa Kata ya Kikatiti, Baraka Kaaya amwsema ruzuku ya Serikali katika ununuzi wa matrekta na vifaa vya kisasa vya kilimo inaweza kuwa chachu ya mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo.
Amesema matumizi ya teknolojia za kisasa yana uwezo wa kuongeza uzalishaji wa mazao kwa kiwango kikubwa, lakini wakulima wengi wadogo wanashindwa kuzinunua kutokana na gharama zake kuwa juu.
“Gharama za vifaa hivi bado ni kubwa kwa wakulima wengi wadogo. Serikali ikiweka utaratibu wa ruzuku itasaidia kuongeza matumizi ya teknolojia za kisasa na kuongeza uzalishaji wa kilimo chenye tija,” amesema Kaaya
Amesema hatua hiyo pia itasaidia kuongeza kipato cha wakulima na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya kilimo ambayo inaajiri na kuhudumia Watanzania wengi.
Uzinduzi wa tawi hilo la Mobikey Agri Machinery Arusha umetajwa kuwa sehemu ya mkakati wa kampuni hiyo wa kusogeza karibu huduma za matrekta, mashine za kisasa za kilimo, vipuri pamoja na huduma za kiufundi kwa wakulima wa kanda ya kaskazini na maeneo jirani.
Meneja Mkuu wa Mobikey Agri Machinery, Vishal Billawaria amesema sekta ya kilimo inaendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania kwa kuchangia kati ya asilimia 30 hadi 35 ya Pato la Taifa (GDP).
Amesema kuimarika kwa matumizi ya teknolojia za kisasa ni hatua muhimu katika kuongeza uzalishaji na kukabiliana na changamoto zinazowakabili wakulima.
“Tunataka kuhakikisha wakulima wanapata huduma, mashine na vipuri kwa urahisi zaidi. Ufunguzi wa tawi hili utasaidia kuongeza matumizi ya teknolojia za kisasa za kilimo katika kanda ya kaskazini,” amesema
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya SAME Deutz-Fahr (SDF), Ludovico Buccolati amesema sekta ya kilimo ina nafasi muhimu katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania na ina fursa kubwa ya kuvutia uwekezaji zaidi.
Amesema matumizi ya mashine na teknolojia za kisasa yataongeza ufanisi wa uzalishaji, kupunguza gharama za uzalishaji na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza katika maendeleo ya kilimo barani Afrika.
Makamu wa Rais wa JAP Group, Diogo Pinto, amesema kampuni hiyo imejikita katika kusaidia maendeleo ya sekta ya kilimo kupitia uwekezaji wa teknolojia za kisasa na huduma zinazolenga kuinua maisha ya wakulima.
“Tunataka kuwa sehemu ya safari ya kujenga kilimo chenye tija zaidi, kuongeza uzalishaji na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Tanzania,” amesema
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa JAP Group Tanzania, Andre Dias amesema matumizi ya mashine za kisasa yana mchango mkubwa katika kuongeza uzalishaji wa mazao, kupunguza gharama za uzalishaji na kuboresha kipato cha wakulima.
Amesema kampuni hiyo imeajiri zaidi ya watu 1,000 katika nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Tanzania, Angola, Msumbiji, Kenya na Uganda.
“Ofisi ya Arusha itarahisisha upatikanaji wa huduma kwa wakulima wa kanda ya kaskazini na kuwasaidia kupata teknolojia wanazohitaji ili kuongeza tija katika shughuli zao za kilimo,” amesema
Naye mwakilishi wa SDF, Alex Duffar amesema teknolojia ndiyo msingi wa kilimo cha kisasa na kwamba uwekezaji katika mashine za kilimo ni hatua muhimu ya kufanikisha ukuaji endelevu wa sekta hiyo.
Amesema ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali katika kuwezesha wakulima kupata teknolojia za kisasa unaweza kuongeza uzalishaji wa mazao na kuimarisha usalama wa chakula nchini.