Wanawake wapewa mbinu za kukuza biashara
Muktasari:
- Wamehimizwa kutumia teknolojia, kutunza kumbukumbu za kifedha na kuendesha biashara kwa misingi ya kitaalamu ili kuongeza tija na ushindani.
Dar es Salaam. Zaidi ya wanawake wafanyabiashara na wajasiriamali 100 wamepatiwa mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SabaSaba), wakihimizwa kutumia teknolojia, kutunza kumbukumbu za kifedha na kuendesha biashara kwa misingi ya kitaalamu ili kuongeza tija na ushindani.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa kupitia programu ya Think Equal Lead Smart (TELS), inayotekelezwa na Jukwaa la Wakurugenzi Watendaji Tanzania (CEOrt) kwa ushirikiano na Vodacom Tanzania Foundation na Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), yalilenga kuwajengea uwezo wanawake kukuza biashara zao.
Akitoa mafunzo hayo, Mshauri wa Masuala ya Biashara na Ujasiriamali kutoka Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Bw. Elia Mbise, aliwataka washiriki kuachana na kufanya biashara kwa mazoea na badala yake kutumia mbinu za kisasa zitakazowawezesha kuongeza faida na kupanua masoko.
Alisema wafanyabiashara wanapaswa kutunza kumbukumbu za manunuzi, mauzo, mapato na matumizi ili kufuatilia mwenendo wa biashara zao na kufanya maamuzi sahihi.
"Ni muhimu kuifahamu vizuri biashara unayoifanya, kujenga mtandao wa wateja na kuwa na maono ya kukuza biashara yako hata kama una mtaji mdogo," alisema Mbise.
Aliongeza kuwa matumizi ya mifumo ya kidijitali, kuongeza thamani ya bidhaa na kujifunza mahitaji ya soko ni miongoni mwa mambo yatakayowasaidia wajasiriamali kukabiliana na ushindani na kuendeleza biashara zao.
Baadhi ya washiriki walisema mafunzo hayo yamewapa maarifa yatakayowasaidia kuboresha usimamizi wa biashara zao pamoja na kukabiliana na changamoto za mitaji na masoko.
Rose Patrick kutoka Tanga, anayejishughulisha na usindikaji wa viungo, alisema elimu hiyo itamsaidia kuboresha biashara yake na kuongeza uwezo wa kushindana sokoni.
Naye Halima Fundi kutoka Dodoma, anayefanya biashara ya kuku na ushonaji, alisema mafunzo hayo yamempa uelewa wa namna ya kupanua masoko, kuongeza thamani ya bidhaa na kuendesha biashara kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, Meneja wa Vodacom Tanzania Foundation, Bi. Sandra Oswald, alisema programu ya TELS inalenga kuwapa wanawake maarifa yatakayowawezesha kukuza biashara zao na kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi.
Katika mafunzo hayo, washiriki wawili, Fatma Omar Kibwana na Fadhila Athumani Mgumia, walitangazwa washindi wa shindano la TELS Biashara Kiosk na kila mmoja kukabidhiwa Sh500,000 kama mtaji wa kuendeleza biashara zao.