Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Watakaoteka masanduku ya kura kushughulikiwa kisheria

Muktasari:

  • Mdahalo huo umeshirikisha wadau mbalimbali wakiwamo vyama vya siasa, viongozi wa dini na viongozi wa serikali kwa lengo la kujadili kwa kina, kutafakari na kupanga mikakati itakayoongoza kuhifadhi amani kutetea haki na kuimarisha demokrasia wakati wa uchaguzi.

Mbeya. Jeshi la Polisi nchini limesema litaendelea kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria za nchi, huku likitoa angalizo kwa vyama vya siasa vitakavyoenda kinyume na taratibu za nchi wakati huu wa mchakato wa uchaguzi mkuu kuwachukulia hatua kali.

Pia, limesisitiza kufuatilia viashiria vya aina yoyote ya uvunjifu wa amani, mikusanyiko isiyo halali, matukio ya uhalifu na makosa ya mtandao kuhakikisha amani na utulivu unakuwapo kabla, wakati na baada ya uchaguzi na halitasubiri kutokea machafuko bali kuzuia kwanza dalili.

Akizungumza leo Jumatano, Agosti 20 wakati wa mdahalo wa ulioandaliwa na Jumuiya ya Maridhiano na amani nchini kuelekea Uchaguzi Mkuu, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema Jeshi hilo limejipanga kusimamia amani.

Muliro amesema Jeshi la Polisi lipo kwa mujibu wa sheria, ambapo chombo hicho kimekubalika kikatiba na jukumu kubwa ni kuhakikisha Tanzania au himaya inakuwa na amani na utulivu wakati wowote.

Amesema wakati wa utekelezaji wa mchakato wa uchaguzi, kuwapo usawa wa kibinadamu, kuwapo sura ya usawa, haki ya kuishi kwa watu, uhuru wa maoni na mawazo katika kipindi hiki cha uchaguzi mambo hayo yapo kikatiba.

“Watu wana haki ya kuchagua na kuchaguliwa, kuteua na kuteuliwa na hili Jeshi la Polisi linatambua na linahakikisha kila mchakato unaenda kwa amani na utulivu, lakini kwa kuzingatia sheria,” amesema.

“Wengine wanadhani tukiwa katika uchaguzi anaweza kufanya lolote kinyume na sheria, wajibu wa kila mtu ni kuzingatia sheria za nchi, wote tunao wajibu na jukumu la kulinda nchi yetu, kujua na kutambua mipaka ya uhuru na haki zetu,” amesema Kamanda huyo.

Ameongeza kuwa Jeshi la polisi na vyombo vingine vya dora wajibu ni kutekeleza majukumu yao kiasili, akibainisha kuwa maisha ya watu yanakuwa salama sawa na mali zao na kuzuia na kugundua uhalifu, kuzuia machafuko kutotokea.

“Jukumu letu ni kuzuia vitendo vya kihalifu, hatuwezi kusubiri ushahidi kwenda mahakamani, haiwezekani tusubiri machafuko ndio twende kuthibitisha, hili halihitaji mzaha na kazi hii inafanyika kwa haki, weledi na utulivu.

“Katika uchaguzi huu hatutakubali kama kuna dalili au viashilia vya fujo, tatizo katika uchaguzi hatutasubiri vikamilike ndio tunafanya kazi kitaaluma (professional), hivyo tunalo jukumu la kudumisha Amani,” amesema Kamanda huyo.

“Makosa yanayotarajiwa na huwa inajirudia ile kughushi mikusanyiko isiyo halali, mauaji, uchochezi, makosa ya mtandao, kujeruhi, kuharibu mali na rushwa, tutafuatilia na ukikamatwa usiwe na mtazamo kuwa upo chama fulani,” amesema.

Akifungua mdahalo huo kwa niaba ya Makamu wa pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah, Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hamza Hassan Juma, amesema Tanzania ni uti wa mgongo kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Amesema amani ikiteteleka Tanzania, itakuwa kama Cosovo ilivyoparaganyika kutokana na kukosa amani, akitolea mfano wa baadhi ya nchi zilizokuwa na amani kisha kutoweka kwa tofauti na udini na itikadi mbalimbali.

“Tanzania tumebahatika kuwa kisiwa cha amani, tumekuwa uti wa mgogngo kwa mataifa mengine, tulikuwa nchi tatu lakini kwa sasa ipo nchi nyingine imejiunga nasi kwenye Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kujifunza na imepona,” amesema Juma.

Ameitaka jumuiya ya maridhiano na amani nchini kuendelea kushikamana akieleza kuwa misingi iliyowekwa na viongozi waliotangulia akiwamo Hayati Mwalimu Julius Nyerere kuendelea kutunzwa.

Mweneyekiti wa Jumuiya ya maridhiano na amani nchini, Sheikh Alhad Mussa Salum amesema mdahalo huo unalenga kujadili kwa kina, kutafakari na kupanga mikakati itakayoongoza kuhifadhi amani kutetea haki na kuimarisha demokrasia.

Amesema uchaguzi ni fursa ya kuonesha uzalendo wa kitaifa kuamua kuchagua kiongozi kwa namna ya ushirikishi na kwamba lengo la mdahalo huo ni kutoa elimu na kufuata sheria katika mchakato huo.

“Madhumuni ya jumuiya yetu ni kusimamia amani na utulivu katika nchi yetu, kuleta muafaka katika mambo ya tofauti dini na vyama, hiki ni kielelezo cha demokrasia, ili uchaguzi uwe huru na haki lazima kila mmoja anao wajibu wa kuheshimu mwingine,” amesema Sheikh Salum.

Amevitaka vyombo vya uamuzi katika uchaguzi ikiwa ni Tume huru ya Taifa ya uchaguzi, Jeshi la Polisi na vyombo vya habari kufanya majukumu yao kwa weledi na kutenda haki katika maamuzi yao.