Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Wazanzibari tunanufaika zaidi ndani ya Muungano’

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakiwa wamenyoosha mikono wakato wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali baada ya kuulizwa na Spika wa Baraza, Zuberi Maulid wanaounga mkono hoja kupitisha bajeti hiyo

Muktasari:

  • Hoja za Muungano, ajira vyaibuka kivingine barazani safari hii baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na mawaziri wa SMZ wakisema vijana wa Kizanzibari wanabagua kazi na ndani ya Muungano Wazanzibari wapo wengi Tanganyika na wanaishi bila kubaguliwa.

Unguja. Wakati kukiwa na mijadala kuhusu masuala ya ubaguzi ndani ya Muungano, baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamewataka wenzao kuacha kupotosha umma, kwani Zanzibar ndio inanufaika zaidi katika Muungano ikilinganishwa na Tanganyika.

Hayo yamebainika leo Juni 18, 2026 wakati wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakiendelea kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali Chukwani Unguja Zanzibar.

Hatua hiyo ni mwendelezo wa hoja ambazo zimeibuka hivi karibuni kuhusu ajira za Zanzibar kupewa watu wengine tofauti na Wazanzibari.

Akichangia mjadala huo mwakilishi wa Kwahani ambaye pia Naibu Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Mohammed Sijamini Mohammed ameonya kauli za upotoshaji zinazotolewa na baadhi ya wawakilishi ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria.

“Kama kuna watu wanaonufaika ndani ya Muungano ni sisi Wazanzibari, ifike hatua tuseme ukweli, sasa tunalalamika nini,  tunyamaze na tutumie fursa hii kuwaelimisha watu wetu badala ya kupotosha,” amesema Sijamini.

Kuhusu Zanzibar inavyonufaika ametolea mfano Mashindano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) mechi hizo zinaandaliwa na mataifa matatu: Kenya, Uganda na Tanzania, lakini kwa kutaka kuweka usawa na Zanzibar kuna baadhi ya mechi zitakwenda kuchezwa katika visiwa hivyo.

Pia, ametolea mfano wa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ambaye kwa sasa yupo nchini Kenya kumwakilisha Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwamba inayonufaika zaidi katika uwakilishi huo ni Zanzibar.

“Tumuogope Mungu, tuache kupotosha mambo tofauti ni ilivyo,” amesema.

Naye Mwakilishi wa Amani, Masoud Amour Masoud (CCM) amesema kuna mafanikio makubwa ya Muungano kwani kuna ushirikiano na mwingiliano mkubwa kati ya Zanzibar na Tanganyika, hivyo wanaubeza wanataka kuleta chokochoko.

“Mimi nimekaa Kahama (Shinyanga), kule ukienda kwenye majaluba unakuta Wazanzibari watupu ndio wanauza mpunga na ukiwaambia waje Zanzibar hawakubali na wala hawabaguliwi, kwa hiyo hizi kauli za kibaguzi hazifai na sisi tutaendelea kuwa kitu kimoja,” amesema Masoud.

Amesema wataendelea kuulinda Muungano na hakuna atakayethubutu kuuvunja na wanatakiwa waseme ukweli kuhusu manufaa yake badala ya kupotosha wananchi.

Akizungumza kuhusu kubaguliwa kwenye ajira na kwenda kwa watu wengine, mwakilishi huyo amewataka wanaosema hivyo pia kuwa wakweli.

Amesema changamoto ya Wazanzibari kutopata ajira kwenye maeneo ya sekta binafsi hususani hotelini inatokana na vijana wengi kubagua kazi hizo ambazo zinatokana na tamaduni na mitazamo.

 “Sio kwamba watu wanabaguliwa ajira zinachukuliwa na watu wengine, isipokuwa ajira zipo na hatuzitaki wenyewe badala yake tunataka kukimbilia ajira za Serikali.”

“Hata mimi kwangu mtu akisema binti yangu anavaa sketi fupi, ukimwambia kwenda hotelini anaonekana sio kazi inayofaa, kwa hiyo watu wengine wanakuja kufanya kazi hizo, niwaombe wajumbe wenzangu tukabadilishe mitazamo ya watu wetu ajira zipo na watu hawabaguliwi,” amesema

Hoja ya ajira pia imezungumziwa na Sijamini ambaye amesema ajira sio za vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) tu, lakini zipo nyingi mtaani ila watu hawazitaki.

“Tuwaelimishe vijana wetu, tutumie fursa hii kuwapa elimu na kubadilisha mitazamo yao kuhusu ajira. Zanzibar inaongoza kwa ajira, lakini watu wetu hawazitaki, wajumbe tubadilike na kuwasaidia watu wetu katika hili,” amesema Sijamini.

Mwakilishi wa Konde (CCM) ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Zawadi Amour Nassor amesema hakuna ukweli kwamba ajira Zanzibar zinatolewa kibaguzi isipokuwa zinatolewa kulingana na vigezo na sifa.

“Hii kasumba kwamba zinachaguliwa, zinabaguliwa sio kweli tuache kupotosha umma, isipokuwa kinachozingatiwa ni sifa za watu na elimu zao, sasa kueleza hapa kwamba kuna ubaguzi katika ajira za Zanzibar sio kweli na tuwaeleze watu usahihi,” amesema.  

Mwakilishi wa nafasi za Wanawake, Jabu Kame Juma (ACT Wazalendo) amesema licha ya Muungano kila nchi inatakiwa kuheshimu nyingine, lakini Zanzibar imekuwa ikinyanyaswa ndani ya Muungano.

“Zanzibar imekuwa koloni kwa muda mrefu kwenye Muungano,” amesema

Amehoji ni kitu gani kinaifanya Zanzibar isiwe mjumbe katika mashirikisho ya mpira likiwamo Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Shirikisho la Soka la Duniani (FIFA) akidai haki hizo zinabebwa na Tanganyika.

Kuhusu ajira Jabu amesema, “wanakuja watu wasiokuwa Wazanzibari wanachukua ajira za vijana wa Kizanzibari, lazima tuwape kipaumbele na sio kuwapa watu ambao hawahusiki.”

Naye Mwakilishi nafasi za Rais ambaye pia ni Waziri wa Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ, Idrissa Kitwana Mustafa amesema kama kuna watu wanafitinisha Muungano kwamba utavunjika, hauwezi kuvunjika kwani sio wa kisiasa tu bali ni maisha ya watu.

Kuhusu upatikanaji wa vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi ambavyo vinasimamiwa na wizara yake, Kitwana amesema suala hilo lipo wazi kikatiba.

“Katiba imeweka wazi kumtambua Mzanzibari ni nani na iwapo mtu akiishi miaka 10 akiwa Zanzibar anaruhusiwa kupewa kitambulisho cha Zan ID, na ili awe Mzanzibari tayari anakuwa ni Mtanzania,” amesema.