Bei ya mafuta Zanzibar yapaa licha ya kupokea shehena ya mafuta
Muktasari:
- Katika bei hizo ambazo zitaanza kutumika kesho Juni 9, 2026 lita moja ya petroli na dizeli itauzwa Sh3,890 huku lita ya mafuta ya taa ikiuzwa kwa Sh4,341.
Unguja. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura), imetangaza bei mpya za mafuta kwa Juni 2026 ambapo lita moja kwa kila aina ya mafuta imeongezeka ikilinganishwa na mwezi uliopita.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Juni 8, 2026 na kitengo cha uhusiano cha Zura, ikimnukuu Mkurugenzi Mkuu wa Zura, Omar Ali Yussuf, Juni petroli kwa bei za jumla itauzwa Sh3,775 na bei ya rejareja itauzwa Sh3,890 wakati mwezi uliopita lita moja iliuzwa kwa Sh3,820 sawa na ongezeko la Sh70.
Kwa upande wa mafuta ya dizeli, lita moja kwa bei ya jumla Juni itauzwa Sh3,775 na rejareja itauzwa Sh3,890 ikilinganishwa na Sh3,850 za mwezi uliopita, sawa na ongezeko la Sh40.
Pia, katika taarifa hiyo bei ya mafuta ya taa kwa jumla itakuwa Sh4,226 na rejareja itauzwa kwa Sh4,341 sawa na ongezeko la Sh91.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bei hizo zinaanza kutumika kesho Juni 9, 2026.
“Pamoja na gharama za ununuzi na uagizaji mafuta kutoka soko la dunia kuwa juu, Serikali imeendelea kutoa ruzuku kwa mafuta ya petroli na dizeli kwa lengo la kulinda ustahimilivu wa bei na kupunguza athari kwa wananchi,” amesema.
Mei 31, 2026 kupitia Bandari Jumuishi ya Mangapwani, ilipokea meli kubwa ya mafuta ya MT Clearocean Miracle kutoka moja kwa moja Saudi Arabia ikiwa na lita 36,271,100.
Akizungumza wakati wa kuipokea meli hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini, Joseph Kilangi alisema Zanzibar kwa sasa inatumia lita milioni 30 kwa mwezi, hivyo ikiwekwa tanki la kuhifadhi mafuta milioni 85 itakuwa na uwezo wa kujihifadhi mafuta ya takribani miezi mitatu.
“Zanzibar ilikuwa na changamoto ya upungufu wa mafuta kwa kipindi kirefu kipindi cha nyuma japo sio kwa kiasi kikubwa kutokana na vita vinavyoendelea mashariki ya kati kwa nchi ya Israel, Iran na Marekani na tulikuwa na mletaji mmoja wa mafuta kutoka Tanga,” amesema.
Naye, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Zura, Rashid Abdullah Fadhil alisema mafuta hayo ni petroli ni lita 14,702,045, dizeli lita 11,476,392 na mafuta ya ndege lita 10,092,663.
Alisema mara nyingi Zanzibar ilikuwa ikipokea meli ndogondogo kwa ajili ya ushushaji wa mafuta kiwango ambacho kilikuwa hakitoshelezi.