Bei ya Petroli, dizeli yashuka mafuta ya ndege yapaa

Ofisa uhusiano Mwandamizi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura), Shara Chande Omar akitangaza Bei za mafuta zitakazotumika Juni mwaka huu. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

  • Kwa sasa Zanzibar inapokea mafuta kupitia Bandari ya Tanga na kuhifadhi katika bohari ya Maruhubi iliyopo Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo bohari hiyo ina uwezo wa kuhifadhi lita za ujazo milioni 21.

Unguja. Bei ya mafuta ya petroli na dizeli imeshuka, huku mafuta ya ndege yakiongezeka bei kisiwani hapa.

Bei ya petroli imeshuka kutoka Sh3,182 kwa lita moja hadi Sh3,132 ikiwa ni tofauti ya Sh50 sawa na asilimia 1.6.

Dizeli kwa Juni, itauzwa Sh3,068 kutoka Sh3,146, ikiwa kuna tofauti ya Sh178 sawa na asilimia 2.5. Bei hizo zimeanza kutumia leo Juni 9, 2024.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura), mafuta ya ndege yatauzwa Sh2,877 ikilinganishwa na Sh2,790 ya Mei, ikiwa ni tofauti ya Sh3.2, huku mafuta ya taa yakibakia bei ileile ya Sh3,200.

Akitangaza bei hizo leo Jumapili Juni 9, 2024, Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa Zura, Shara Chande Omar, ametaja sababu za kupungua na kuongezeka kwa bei hizo ni kutokana na gharama za mafuta katika soko la dunia, gharama za uingizaji wa mafuta pamoja na mabadiliko ya fedha za kigeni.

“Sababu nyingine ni gharama za usafiri, bima na Premium hadi Zanzibar, kodi na tozo za Serikali na kiwango cha faida kwa wauzaji wa jumla na rejareja,” amesema Mbaraka.

Kwa sasa Zanzibar inapokea mafuta kupitia Bandari ya Tanga na kuhifadhi katika bohari ya Maruhubi iliyopo Mkoa wa Mjini Magharibi na bohari hiyo ina uwezo wa kuhifadhi lita za ujazo milioni 21.

Wakati bohari hiyo ikiwa na uwezo huo, matumizi ya mafuta Zanzibar ni kati ya lita za ujazo milioni 30 hadi 40 kwa mwezi, huku Zanzibar ikiwa na vituo vya mafuta zaidi ya 100.

Baadhi ya watumiaji wa nishati hiyo wamesema punguzo hilo sio dogo, lakini ni vyema kukawa na mipango mathubuti ya kuwa na vituo vya kuhifadhi mafuta mengi.

“Tukiwa na mafuta angalau ya mieizi sita itapunguza hili la kuwa inabadilika kila mara, kwani watu watahifadhi na pindi bei zitakapokuwa zinabadilika kwenye soko la dunia huku tunaendelea kuwa na ziada,” amesema Shaib Hussein Mwalim, mkazi wa Kikwajuni.