Dk Shein alivyoingia madarakani ‘kiulaini’

Muktasari:

  • Baada ya kumuangalia Rais wa sita, Amani Abeid Karume, leo tunaanza kumuangalia Rais wa saba wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.

Dodoma. Rais wa saba wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ndiye kiongozi wa kwanza ambaye ushindi wake ulikubaliwa na mgombea wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad na Rais wa kwanza kuongoza Serikali iliyojumuisha upinzani.

 Tangu Uchaguzi Mkuu wa vyama vingi ulipofanyika mwaka 1995, 2000 na 2005, mgombea wa CUF, Maalim Seif ambaye aligombea chaguzi zote hizo, hakuwahi kukubali matokeo ya uchaguzi kwamba ameshindwa na mara zote walikuwa wakitangaza kutomtambua Rais aliyetangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Dk Shein mbali na kuwa Rais wa kwanza kutambuliwa na upinzani, pia wakati wa kuapishwa kwake aliyekuwa mshindani wake mkuu kwenye uchaguzi huo wa 2010, Maalim Seif, wanachama na wafuasi wa CUF na vyama vingine vvya upinzani kama vile NCCR-Mageuzi, Chadema walihudhuria sherehe ya kuapishwa kwake.

Ilikuwa ni siku ya historia kwa siasa za Zanzibar ambapo wafuasi wa CCM pia walivaa sare na bendera za CUF, wafuasi wa CUF na vyama vingine nao walichanganya sare kuonyesha maridhiano na kwamba Zanzibar imezika uhasama wa kisiasa.

Kabla ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi huo na ZEC kwenye hoteli ya Bwawani, hali ilikuwa tofauti kwa wafuasi wa CUF kujaa ndani ya uzio wa hoteli hiyo wakidai mgombea wa CUF Maalim Seif atangazwe mshindi, huku juhudi za kuwatoa ndani ya uzio zikishindikana.

Maalim Seif aliyekuwepo kusikiliza matokeo ya uchaguzi kwa mara ya kwanza, akiwa amesimama juu ya gari la polisi na kutumia kipaza sauti cha polisi, aliwaomba wafuasi wake wakubali kutoka kwenye eneo la hoteli lakini walimkatalia na kumwambia awaachie chama chao na yeye aliwaambia, “Basi naondoka nawaachia chama chenu.”

Maalim Seif alishuka kwenye gari la polisi na kutembea akitoa nje ya geti la hoteli, nyuma yake alifuatwa na wafuasi wakiwa kwenye sura za huzuni na wote walitoka na geti lilifungwa.


Matokeo kutangazwa

Akitangaza matokeo hayo, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec), Khatib Mwinyichande alisema Dk Shein alipata kura 179,809 ambazo ni sawa na asilimia 50.1.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, Maalim Seif, ambaye amegombea urais kwa mara ya nne, alipata kura 176,338 ambazo ni sawa na aslimia 49.1 ya kura zote 358,815.

Alisema kuwa vyama vilivyosimamisha wagombea urais katika uchaguzi huo ni pamoja na AFP, CCM, CUF, Jahazi Asilia, NCCR-Mageuzi, NRA na Tadea.

"Matokeo yanaonyesha kuwa mgombea wa NRA amepata kura 480 sawa na asilimia 0.1 wa CCM kura 179,809 sawa na asilimia 50.1, wa CUF kura 176,338 sawa na asilimia 49.1, Jahazi Asilia kura 803 sawa na asilimia 0.2, NCCR kura 363 sawa na asilimia 0.1, NRA kura 525 sawa na asilimia 0.1 na Tadea kura 497 sawa na asilimia 0.1," alisema Mwinyichande.


Maalim Seif akubali matokeo

Ilikuwa mara ya kwanza kwa mgombea wa CUF, Maalim Seif kukubali kushindwa kwenye uchaguzi na kusema:

"Dk Shein ana uwezo, uzoefu na mahaba kwa nchi yake. Tunatumaini ataongoza kwa busara na hekima kwa lengo la kuunganisha nchi yetu. Naamini kuwa Wazanzibari walifanya maamuzi sahihi Julai 31. Tarehe hiyo waliamua kuunda Serikali shirikishi."

Kwa mara ya kwanza mshindi na aliyeshindwa walipongezana huku Maalim Seif akisema uamuzi huo umeweka enzi mpya ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) na kwamba Wazanzibari wamempa Dk Shein jukumu la kuongoza kwa mara ya kwanza SUK.

Maalim Seif aliishukuru ZEC kwa kuendesha uchaguzi ambao ulikuwa na afadhali kulinganisha na chaguzi nyingine. "Lakini, kuna dosari ambazo ni lazima zirekebishwe. Mwenye matatizo si wewe mkurugenzi... ni baadhi ya maofisa wako.

"Alieleza matatizo ambayo maofisa wa uchaguzi wamekuwa wakiyafanya akisema yanasababisha watu wasiwe na imani na tume."

“Dk Shein ni Rais mteule. Ametangazwa tu kuwa mshindi, lakini hakuna mshindi. Washindi ni Wazanzibari wote na Shein ni mteule tu. Siasa za kubezana zitachafua hali ya hewa kabisa," alionya Maalim Seif akimtaka Dk Shein afikishe ujumbe huo kwa viongozi wenzake wa CCM na wanachama wao.

Dk Shein alimshukuru Maalim Seif kwa hotuba yake, aliyoielezea kuwa ilijaa busara na hekima na kuahidi kutekeleza yote ambayo kiongozi huyo wa CUF aliyazungumzia.

Hali kadhalika alimsifu Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharrif Hamad, kwa msimamo wake wa kukubali matokeo ya uchaguzi, kauli ambayo alisema imempa matumaini kuiongoza Zanzibar.

Aliahidi kuwa atashirikiana naye kila itakapobidi, ili kudumisha na kulinda maridhiano yaliyoasisiwa na kiongozi huyo wa CUF na Rais wa sita Amani Abeid Karume anayemaliza muda wake akiiacha nchi ikiwa tulivu.


Mchakato ndani ya CCM

Wakati wa mchakato wa kumpata mgombea wa CCM kwenye uchaguzi huo wa Zanzibar wa mwaka 2010 kurithi nafasi iliyoachwa na Rais wa sita, Amani Abeid Karume, walijitokeza watangaza nia 11 waliojadiliwa na Kamati Kuu Maalumu ya CCM Zanzibar kwa kuwapa alama kabla ya majina hayo kuwasilishwa kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (Nec).

Waliojitokeza na Dk Ali Mohamed Shein ambaye kwa wakati huo alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk Mohamed Gharib Bilal aliingiza jina lake kwa mara ya pili, mara ya kwanza ilikuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 uliomuingiza madarakani Amani Abeid Karume. Dk Bilal aliwahi kuwa Waziri Kiongozi kwenye Serikali ya tano ya Dk Salmin Amour.

Wengine waliojitokeza ndani ya CCM, Ali Juma Shamhuna (kwa sasa ni marehemu) ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Waziri wa habari utamaduni na Michezo.

Watangaza nia wengine waliku Shamsi Vuai Nahodha aliyekuwa Waziri Kiongozi katika Serikali ya Rais wa sita, Amani Abeid Karume. Shamsi ndiye Waziri Kiongozi pekee aliyekaa kwa miaka 10 mfululizo kwenye nafasi hiyo. Pia, mtangaza nia mwingine alikuwa Ali Abeid Amani Karume ambaye ni mdogo wa Rais aliyekuwa akiondoka madarakani, Amani Abeid Karume.

Ali wakati huo anatangaza nia alikuwa balozi wa Tanzania nchini Italia, wengine ni Maalim Haroun Ali Suleiman ambaye wakati anatangaza nia alikuwa Waziri wa Elimu, Mohamed Aboud Mohamed ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Viwanda, Waziri wa Kilimo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Serikali ya Jamhuri na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.


Kesho usikose nakala ya Mwananchi, tutaendelea kuangalia namana Dk Shein na Maalim Seif walivyofanya kazi baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.