Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kuimarisha viwanda, kutafuta masoko vipaumbele wizara ya biashara

Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shaaban akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo barazani Chukwani Zanzibar

Muktasari:

  •  Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda imeliomba Baraza la Wawakilishi kuidhinishiwa Sh57.55 bilioni ili kutekeleza vipaumbele vyake vitatu.

Unguja. Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda imepanga kutekeleza vipaumbele vitatu vikuu katika mwaka wa fedha 2025/26, ambavyo vinalenga kuimarisha sekta ya viwanda na biashara, kupanua wigo wa masoko, pamoja na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na utoaji wa huduma kwa ufanisi zaidi.

Akisoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi leo Mei 16, 2025, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Omar Said Shaaban, ameliomba Baraza la Wawakilishi kuidhinisha Sh57.55 bilioni kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa vipaumbele vya wizara hiyo katika mwaka wa fedha 2025/26.

Katika kuendeleza sekta ya viwanda, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda imepanga kuendeleza maeneo maalum ya viwanda ya Dunga, Chamanangwe na Pangatupu.

Akifafanua kuhusu mpango huo, Waziri wa wizara hiyo, Omar Said Shaaban amesema kuwa katika eneo la Dunga, Serikali inatarajia kujenga jengo la utawala pamoja na majengo ya viwanda.

Kwa upande wa Chamanangwe, miundombinu itakayowekwa inajumuisha majengo ya viwanda, huduma za maji, umeme na barabara za ndani.

Aidha, katika eneo la Pangatupu, Wizara imepanga kufanya upimaji wa udongo na kuandaa mpango kabambe wa matumizi ya ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda.

Katika kuimarisha sekta ya biashara, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda imepanga kutekeleza miradi kadhaa muhimu katika mwaka wa fedha 2025/26, ikiwemo uendelezaji wa eneo la kituo cha maonesho ya kibiashara kilichopo Dimani.

Miongoni mwa kazi zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa ghala la kuhifadhia vifaa, uboreshaji wa jengo la kuuza chakula, ujenzi wa miundombinu ya burudani kwa watoto, pamoja na uboreshaji wa ukumbi wa mikutano kwa kuweka vifaa vya kisasa vitakavyowezesha kufanyika kwa mikutano mikubwa ya kitaifa na kimataifa.

Aidha, Waziri wa Wizara hiyo, Omar Said Shaaban, amesema Serikali imepanga kuratibu ujenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano, ambapo juhudi zinaendelea za kutafuta wawekezaji watakaoshirikiana na Serikali kwa masharti nafuu ili kufanikisha mradi huo.

Pamoja na hilo, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Exim ya Jamhuri ya Korea imepanga kufanya upembuzi yakinifu wa mradi huo.

Mshauri elekezi anatarajiwa kuanza kazi ya upembuzi huo kuanzia Juni hadi Desemba 2025, katika eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.

Katika kuimarisha mazingira ya ufanyaji biashara, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda imepanga kufanya mapitio ya Sheria ya Biashara pamoja na kanuni zake, huku ikiendelea na mazungumzo ya kutatua changamoto za kibiashara kati ya Zanzibar na Tanzania Bara.

Pia, Wizara itasimamia na kufuatilia utekelezaji wa matokeo ya ripoti ya tathmini ya kuimarisha mazingira ya kibiashara, lengo likiwa ni kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, pamoja na kuratibu uandaaji wa mkakati wa mauzo ya nje ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa Waziri Shaaban ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa na kuingizwa nchini zinakidhi viwango, Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) imepanga kupata ithibati ya maabara tano.

Amesema maabara hizo ni pamoja na za nishati, nguo na ngozi, vifungashio, chakula, na vimelea, zote zitakazothibitishwa kwa kutumia kiwango cha ISO/IEC 17025:2017.

Aidha, Wizara itawekeza katika maabara ya kemikali, nishati, chakula, upimaji wa gesi, kituo cha kuhifadhia data, pamoja na ununuzi wa vifaa vya kisasa vya maabara ili kuboresha huduma na viwango vya upimaji nchini.


Maoni ya kamati

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Utalii na Biashara, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mtumwa Pea Yussuf, ameshauri Serikali kuhakikisha masoko yanapatikana ndani na nje ya nchi ili wafanyabiashara waweze kunufaika na fursa hizo.

Aidha, kamati imebaini kuwa kuna uelewa mdogo kuhusu usajili wa mali bunifu miongoni mwa Wazanzibari na pia uelewa mdogo wa madaraja ya karafuu kwa wakulima, changamoto ambazo zinakikabili Shirika.

“Kwa sababu ya umuhimu wa sekta hizi, tunapendekeza fedha zilizokadiriwa katika bajeti zipatikane haraka ili kutekeleza malengo haya,” amesema Mwenyekiti.