Makusanyo kodi Zanzibar yapaa
Muktasari:
Katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya kodi ya robo ya nne ya mwaka wa fedha 2023/24 (Aprili hadi Juni) ZRA imejipanga kuongeza ubunifu kwa kurahisisha na kuondoa usumbufu katika kuimarisha huduma za kodi.
Unguja. Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), imekusanya Sh559.48 bilioni kwa kipindi cha miezi tisa ya mwaka wa fedha 2023/24, miongoni mwa sababu zilizochangia ni uwekezaji miundombinu, huduma za kijamii na kuimarika shughuli za kiuchumi.
Kiasi hicho ni kati ya lengo la kukusanya Sh536.2 bilioni kwa kipindi cha Julai hadi Machi, sawa na ufanisi wa asilimia 104.34 ya lengo la makusanyo ya kodi tarajiwa ya Sh536.2 bilioni.
Taarifa iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa ZRA, Yusuph Juma Mwenda leo Aprili 3, 2024 inaeleza kwa kipindi hicho makusanyo halisi ya kodi yameongezeka kwa asilimia 24.53 ambacho ni kiasi cha Sh110.2 bilioni kulinganisha na mapato halisi ya mwaka 2022/23 ambayo yalikuwa Sh449.2 bilioni.
Amesema Julai ZRA ilikusanya Sh42.4 bilioni kati ya makisio ya Sh42.8 bilioni, Agosti ikakusanya Sh55.6 bilioni kati ya makisio ya Sh57.2 bilioni, Septemba ilikusanya Sh59 bilioni kati ya makisio ya Sh61.6 bilioni na Oktoba ilikusanya Sh58.1 bilioni kati ya makisio ya Sh61.2
Novemba walikusanya Sh60.8 bilioni kati ya Sh65.2 bilioni, Desemba walikusanya Sh59.3 bilioni kati ya makisio ya Sh63.5 bilioni, Januari walikusanya Sh66.5 bilioni kati ya makisio ya Sh70.1 bilioni, Februari Sh70.7 bilioni kati ya makisio ya Sh72.9 bilioni na Machi makusanyo ni Sh63.4 bilioni kati ya Sh64.6 bilioni.
Kamishna Mwenda amesema mbali na uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa miundombinu na huduma za kijamii, sababu nuingine ya ongezeko hilo ni kuimarika kwa shughuli za kiuchumi Zanzibar kunakotokana na utekelezaji wa sera nzuri za kiuchumi.
Sababu nyingine amesema ni kuongezeka kwa uwajibikaji wa ulipaji kodi wa hiari, na kuongezeka kwa ufanisi wa ZRA katika kufanya kazi kwa kuimarisha huduma bora za kodi katika ofisi za mikoa ya kikodi ya Unguja na Pemba.
Utoaji elimu na kuimarisha matumizi sahihi ya mifumo ya ukusanyaji kodi ya VFMS na Zidras ni sababu nyingine inayotajwa kuchangia ZRA kufanya vizuri katika makusanyo.
Pia kuimarika ushirikiano na taasisi nyingine zinazofanya kazi na ZRA ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kamisheni ya utalii, na Uhamiaji.
Wadau wazungumza
Wakizungumza kuhusu ongezeko hilo baadhi ya wataalamu wa masuala ya kodi, akiwemo Burhan Ali Saleh amesema kuna uhusiano mkubwa wa kuimarika kwa kodi na ukuaji wa uchumi.
Hata hivyo, amesema bado jitihada zaidi zinatakiwa kufanyika ili kufikia hatua ambayo Taifa hilo litaweza kujitegemea kwa kiasi kikubwa badala ya kutegemea fedha za misaada.
“Binafsi siwezi kusema imefanya vizuri au vibaya, kimtazamo inaweza kuwa imefanya vizuri lakini upande mwingine wa shilingi labda waliweka target (makisio) madogo hivyo ni rahisi kuona wamevuka lengo,” amesema.
“Hata hivyo, niwapongeze kwani tunaona jitihada kubwa zinazofanyika; ZRA si ile ya kipindi cha nyuma, kwa sasa hata wanafika kwa wafanyabiashara kuona changamoto zao na kuzifanyia kazi,” amesema.
Mipango ya baadaye
Katika kuimarisha ukusanyji wa mapato ya kodi ya robo ya nne ya mwaka wa fedha 2023/24 (Aprili hadi Juni) wamejipanga kuongeza ubunifu kwa kurahisisha na kuondoa usumbufu katika kuimarisha huduma za kodi.
ZRA imesema imejipanga kuendeleza weledi wa watumishi, kuwapatia mafunzo stahiki, usimamizi makini na huduma nzuri kwa walipakodi na kuimarisha taarifa za wageni wanaoingia Zanzibar na kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na mawakala wa usafiri (OTA) zinazofanya kazi Zanzibar.
“Tutaimarisha, kusaidia kusomana mfumo wa Zidras na mifumo ya taasisi nyingine tunazofanya nazo kazi ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi za walipakodi,” amesema Mwenda.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Juma Makungu Juma ameitaka ZRA inapohisi kuna mianya ya kukwepa kulipa kodi wasisite kuchukua hatua.
Makungu alitoa kauli hiyo jana Aprili 2, 2024 wakati wa iftar iliyoandaliwa na ZRA kwa wadau na wateja wao Unguja.
“Kila tunapohisi hapa kuna mwanya wa kukwepa kodi tuzidi kubana kusudi mapato yasipotee, kufanya hivyo tutaendana na uhalisia huu umeonyesha leo lakini tutawatia moyo wenzetu walipakodi kwamba tunachokitoa kinaenda kunufaisha jamii yote,” amesema.