Nafasi ya Maalim Seif, Balozi Iddi kwenye mafanikio ya Dk Shein

Muktasari:

  • Jana tuliangalia namna Rais wa saba wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein alivyoingia madakarani na sherehe ya kuapishwa kwake ilivyoungwa mkono na upinzani. Leo tunaangalia Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ilivyofanya kazi ikiwamo kuungwa mkono na mabalozi.

Dodoma. Rais wa saba wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ndiye kiongozi aliyeanza na muundo mpya wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), yenye makamu wawili wa Rais, ikijumuisha chama cha upinzani.

Dk Shein chini ya SUK alimteua Maalim Seif Shariff Hamad kutoka Chama cha Wananchi (CUF) kuwa makamu wa kwanza wa Rais na Makamu wa Pili wa Rais alimteua Balozi Seif Ali Iddi kutoka CCM.

Kabla ya mabadiliko hayo ya Katiba ya Zanzibar, kulikuwa na nafasi ya Waziri Kiongozi na Naibu Waziri Kiongozi.

Nafasi za Makamu wa Kwanza wa Rais na Makamu wa Pili wa Rais zilitokana na marekebisho ya Katiba ya Zanzibar kukidhi mahitaji ya maridhiano ya kisiasa ya mwaka 2010, yaliyofanyika kati ya Rais wa sita, Amani Abeid Karume na Maalim Seif.

Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ibara kuanzia ya 39, makamu wa kwanza wa Rais atakuwa ni mshauri mkuu wa Rais katika kutekeleza kazi zake na atafanya kazi zote atakazopangiwa na Rais.

Pia, makamu wa pili wa Rais atakuwa ndiye mshauri mkuu wa Rais katika kutekeleza kazi zake na pia atakuwa ndiye kiongozi wa shughuli za Serikali katika Baraza la Wawakilishi.

Makamu wa kwanza wa Rais na Makamu wa pili wa Rais wakati wote watakapokuwa madarakani watawajibika kwa Rais.


Majukumu ya Maalim Seif

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais chini ya Maalim Seif ilipewa majukumu kadhaa ikiwamo kusimamia, kuratibu na kuhakikisha jamii ya Zanzibar inaishi katika mazingira endelevu bila ya athari za Ukimwi, VVU, dawa za kulevya na inayolinda haki na fursa za watu wenye ulemavu.

Maalim Seif katika utekelezaji wa majukumu, ofisi yake ilianzisha Mfuko wa wenye ulemavu na ilizindua Sera ya Mazingira na Uhifadhi wa Mazingira, mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya na vita dhidi ya ongezeko la maambukizi ya virusi ya Ukimwi.

Miongoni mwa mafanikio ni utekelezaji wa Ilani ya CCM 2010 – 2015 katika suala la mazingira, kuandaa sera ya mazingira na kusimamia utekelezaji wa mpango wa hifadhi ya mazingira katika maeneo ya ardhi, bahari na ukanda wa pwani.

Pia, alitekeleza jukumu la kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa utunzaji na uhifadhi wa mazingira katika maeneo ya makazi na sehemu za kazi, viwanda na mahotelini.

Ofisi hiyo pia iliweka jitihada za kuimarisha mpango wa kitaifa wa kupanda miti na miti ya asili kila mwaka kwa kushirikisha viongozi wa vitongoji, vijiji na mitaa.

Pia, ofisi hiyo ilifanya utafiti wa kujua mahitaji ya watu wenye ulemavu kwa kuzingatia namna ya kuwafikia kwa urahisi na namna ya kuwapatia haki yao ya elimu kwa kuzingatia ulemavu walionao na namna ya kuwawekea mazingira rafiki.

Chini ya Maalim Seif, Ofisi ya makamu wa kwanza wa Rais, ilianzisha mfuko wa watu wenye ulemavu pamoja na bodi mpya ya Tume ya Ukimwi kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kazi zake.

Pia, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, ilitenga fungu maalum kwa ajili ya kuzisaidia nyumba za kurekebisha tabia “’Sober House’ kwa vijana walioamua kuacha matumizi ya dawa za kulevya.

Sambamba na hatua hiyo, pia Serikali iliweka eneo maalum kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya karekebisha tabia.


Ofisi ya Makamu wa Pili

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, chini ya Balozi Seif Ali Iddi ilitekeleza majukumu yake kwa mafanikio kwa kuratibu miradi midogo midogo ya wananchi kwa kupitia mpango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na mfuko wa maendeleo ya jimbo (CDF) kwa lengo la Serikali kuwasaidia wananchi wake kupunguza umaskini.


Mchango wa Balozi Iddi

Chini ya Balozi Seif Iddi kaya nyingi Unguja na Pemba zilinufaika na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) na fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo.

Pia, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais ilifuatilia utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010-2015 katika wizara zote za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na kuandaa taarifa ya utekelezaji wa ilani hiyo.

Ofisi hiyo iliendelea kuratibu vikao vya kero za Muungano kati ya Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais kwa uongozi wa Makamu wa Rais wa Muungano kama mwenyekiti.

Pia, ofisi hiyo iliandaa sera ya kukabiliana na maafa ya mwaka 2013, mkakati wa mawasiliano wakati wa maafa na mpango wa kujikinga na kukabiliana na maafa, ngazi ya wilaya, ikiwamo mwongozo wa ufuatiliaji na tathmini wa sera ya maafa.

Kazi nyingine zilizosimamiwa na ofisi hiyo ni kuratibu uokoaji katika ajali mbili kubwa za meli, MV Spice Islander 1 iliyotokea Oktoba 2011 na MV Skagit iliyotokea Julai 2012 na kuua mamia ya watu.

Pia, ofisi ilisimamia na kuratibu ufunguaji wa ofisi ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kisiwani Zanzibar.


Mabalozi wavutiwa na SUK

SUK ilipotimiza miaka minne ilivuta hisia za wafuatiliaji wa masuala ya siasa Afrika na duniani, kutokana na historia ya Zanzibar kuwa na mitafaruku ya kisiasa wakati na baada ya uchaguzi.

Tofauti na miaka mingine Dk Shein ambaye alikuwa Rais wa kwanza kutambuliwa na upinzani na kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwake, hali hiyo iliwavutia washirika wa maendeleo kuendelea kuisaidia Serikali hiyo.

Dk Shein alitembelewa na kundi la mabalozi SUK ilipotimiza miaka minne, akiwamo aliyekuwa Balozi wa Marekani nchini, Mark Childress aliyeonyesha kufurahishwa na amani na utulivu tangu ilipoundwa SUK.

Mbali na Marekani, pia aliyekuwa Mwakilishi wa Jumuiya ya Ulaya (EU) nchini, Balozi Filibe Sebriga naye alieleza kufurahishwa na SUK kwa kujenga amani na kuwaunganisha Wazanzibari.

Aliyekuwa Balozi wa Ujerumani nchini, Egon Kochanke alikwenda Zanzibar kuonana na Dk Shein na kueleza namna Ujerumani ilivyoridhishwa na mazingira ya visiwani humo.

Lakini pia, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kusaidia Maendeleo ya Wakulima na wafugaji (IFAD), Perin Saint Ange naye mbali na kufurahishwa aliahidi shirika lake litaendelea kusaidia miradi ya kuendeleza wakulima na wafugaji kwa kuwapa mbinu mpya za kilimo na ufugaji.

Norway, nchi ambayo ni mdau wa maendeleo wa Zanzibar katika nishati ya umeme, ilitoa taarifa kuwa SUK imekuja kuleta maendeleo na kuondosha migogoro na malumbano ya kisiasa.

Pia, Waziri wa Biashara wa Nje kutoka Uholanzi kwa wakati huo, Liliane Ploume alifika Zanzibar akiwa na ujumbe wa wawekezaji 50 kutoka nchini kwake akieleza kufurahishwa na mazingira ya uwekezaji na zaidi kuwepo kwa amani na utulivu.


 Inaendelea kesho kwa kuangalia namna alivyokuza uchumi wa Zanzibar.