Pato sekta ya utalii Zanzibar lapaa

Katibu mtendaji wa kamisheni ya utalii Zanzibar Hafsa Mbamba akisisitiza jambo wakati wa mahojiano ma shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC)
Muktasari:
- Kuelekea miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu Zanzibar, utalii watajwa kuchangia pato la taifa kwa asilimia 30, huku ukihusika kwa namna moja ama nyingine, kuinua hali za uchumi za watu visiwani humo.
Unguja. Wakati Zanzibar ikiwa inaelekea kwenye maadhimisho ya miaka 60 tangu kufanyika kwa Mapinduzi Matukufu Januari 12, 1964, imeelezwa kuwa kuwa asilimia 30 ya pato la visiwa hivyo linatokana na sekta ya utalii.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Shirika la Habari Zanzibar (ZBC), Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Hafsa Mbamba amesema mchango huo wa utalii unatokana na haiba na uzuri uliojaliwa visiwa hivyo.
“Hii inatokana na haiba na uzuri ambayo visiwa hivi vimejaaliwa...ukipangwa na kingo za Bahari ya Hindi pamoja fukwe nzuri katika visiwa vya Unguja na Pemba na hivyo kusababisha wageni kutoka mataifa tofauti ulimwenguni kuitembelea Zanzibar,” amesema.
Mbamba amesema kuwa katika kuhakikisha utalii unakua zaidi wameamua kuweka mpango kazi ambao unalenga kuitoa Zanzibar ilipo sasa na kusonga mbele zaidi ikiwa ni sehemu ya watu kujivunia uhuru wao walioupata baada ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964.
Kwa mujibu wa Mtendaji huyo, Kamisheni ya Utalii Zanzibari kwa sasa wamejikita kukuza utalii wa Kisiwa cha Pemba ambao kwa miaka mingi ulikua nyuma na haukua ukitangazwa vizuri, huku nguvu kubwa ikielekezwa Kisiwa cha Unguja.
“Tutahakikisha sekta ya utalii Zanzibar inakua endelevu pamoja na kutanua wigo zaidi sambamba na kubuni aina mpya ya utalii ambao utaleta wageni wengi zaidi, kuja kushuhudia mazuri ya Zanzibar ambayo hawawezi kuyapata sehemu nyingine,” amesema Hafsa na kuongeza;
‘’Kwa mfano kabla ya kuja kwa corona (Covid-19) Zanzibar ilikua ikipokea wageni 538,000 lakini kwa mwaka 2022 wageni waliotembelea 548,000 hii ni wazi kuwa ongezeko la wageni na utalii wa Zanzibar unaendelea kukua kila leo,” amesisitiza.
Akitaja sababu za kuongezeka kwa idadi hiyo ya wageni, amesema ni pamoja na suala zima la kukuzwa kwa utalii endelevu pamoja na mikutano ya kimataifa ambayo amesema imekuwa ikiitangaza Zanzibar ulimwenguni kote.
Amesema kupitia mikutano hiyo ya kimataifa, takwimu zao zinaonesha ongezeko kubwa la wageni ambao hawakua wakitembelea Zanzibar kwa wingi miaka ya nyuma na kuzitaja nchi hizo kuwa ni China, Russia pamoja na India.
Akizungumza na Mwananchi Digital, Katibu Mtendaji wa Jumuia ya Waogoza Watalii Zanzibar (Zatoga), Azizi Ramadhan Bonzo, amesema utalii wa Zanzibar unaweza kuvuka malengo yaliowekwa na Serikali iwapo mazingira yataimarishwa.
Amesema suala muhimu ni kuongezwa kwa usafi wa miji pamoja fukwe za habari na ikwezekana kuwa na utaratibu maalumu wa wanaobainika kutupa taka ovyo mitaani, kulipishwa faini.
“Tumekua tukikikumbana na maswali kutoka kwa wageni wakati mwengine wanashangaa watu wanavyotupa taka barabarani na kuona uchafu ukizagaa mitaani,” amesema.
Kuhusu usafi wa mahoteli, Bonzo amesema kuwa kuna kiwango kikubwa cha usafi kwenye maeneo hayo na kueleza kuwa usafi huo unachangia kwa kiasi kikubwa kuleta wageni.
Katika hatua nyengine sekta hiyo ya utalii pia inatajwa kuwa chachu ya kuleta mabadiliko ya kiuchumi katika familia ambazo zilikua duni.
Jine Ahmada ambaye ni mjane anaefanya shughuli za kilimo cha mboga mboga eneo la Chukwani Zanzibar, amesema anaweza kuhudumia familia bila changamoto yoyote ile, huku akibainisha kuwa soko kubwa la bidhaa yake ni kwenye hoteli ambako anauza “kwa bei yenye maslahi makubwa.”