Petroli, Dizeli vyashuka bei Zanzibar

Kaimu Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura), Rahma Hassan Thabit akitangaza bei mpya za mafuta. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

  • Watumiaji wa mafuta ya Petroli na Dizeli wamepata ahueni baada ya nishati hiyo kupungua bei kisiwani Zanzibar.

Unguja. Mafuta ya Petroli na Dizeli yameshuka bei baada ya kupanda kwa miezi mitatu mfululizo kisiwani hapa.

Petroli imeshuka kwa Sh277, kutoka Sh3,187 ya Novemba hadi Sh2,910 sawa na punguzo la asilimia tisa huku Dizeli ikishuka kwa Sh155 kutoka Sh3,323 bei ya Novemba hadi Sh3,168 sawa na asilimia tano.

Akitangaza bei hizo leo Desemba 8, 2023, Kaimu Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura), Rahma Hassan Thabit amesema bei hizo zinaanza kutumika kesho Desemba 9, 2023.

“Sababu za kupungua kwa bei za mafuta kwa Desemba 2023 ni kushuka kwa gharama za mafuta katika soko la dunia na uingizaji wa mafuta hadi kufika Zanzibar,” amesema Rahma.

Wakati bei za mafuta hayo zikishuka, bei ya mafuta ya taa itabaki ileile Sh3, 300 huku mafuta ya ndege yakipungua kwa Sh3 kutoka Sh2, 976 hadi Sh2, 973.

Rahma amesema mamlaka hupanga bei kwa kuzingatia mambo kadhaa, ikiwemo mwenendo wa mabadiliko ya bei za mafuta duniani na gharama za uingizaji mafuta katika bandari ya Dar es Salaam na Tanga.

Kingine kinachoangaliwa kwa mujibu wa Rahma, ni thamani ya Shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani, gharama za usafiri, bima, kodi na tozo za Serikali pamoja na kiwango cha faida kwa wauzaji wa jumla na rejareja.

Baadhi ya wananchi wamekuwa na maoni tofauti wakisema kupungua kwa bei ya mafuta huenda ikasaidia kupunguza pia ugumu wa maisha.

“Kilio cha wananchi wengi ni ugumu wa maisha, nadhani hizi zinaweza kuwa habari njema angalau kuwapa watu moyo kupungua mfumuko wa bei,” amesema Bakari Rashid Ahmada