Rais Mwinyi aridhishwa kasi ujenzi uwanja wa Amani
Muktasari:
- Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Novemba 24, 2023 alipofanya ziara maalumu ya kukagua uwanja huo ambapo amesema lengo la Serikali ni kuona sherehe za miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu, ambazo zitakuwa kubwa zaidi ikilinganishwa na miaka mingine, zinafanyikia katika uwanja huo.
Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameridhika na hatua ya ujenzi wa Uwanja wa Amani unaotekelezwa na kampuni ya Orkun Group ya nchini Uturuki.
Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Novemba 24, 2023 alipofanya ziara maalumu ya kukagua uwanja huo ambapo amesema lengo la Serikali ni kuona sherehe za miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu, ambazo zitakuwa kubwa zaidi ikilinganishwa na miaka mingine, zinafanyikia katika uwanja huo.
Amesema kutokana na muda uliobaki kabla ya sherehe hizo Januari 12, 2024; ameona ni vyema kuutembelea uwanja huo na kuona hatua zilizofikiwa ili kujiridhisha kama azma ya kutumia uwanja huo itafanikiwa.
“Kwa bahati nzuri tumejionea wenyewe hali imekwenda vizuri na kwa mujibu wa mkandarasi mwisho wa mwezi Desemba mwaka huu atakabidhi uwanja huu. Na hili ni jambo la kutia faraja sana,” amesema Dk Mwinyi
Hata hivyo, Dk Mwinyi amesema baada ya muda mfupi atarudi kuangalia tena ili kuona hatua ya mwezi mmoja uliobaki itafikiwa kama walivyosema.
Kiogozi huyo, amesema ni vyema kuendelea kumuombea mkandarasi huyo akamilishe kazi hiyo kwa wakati kwani zipo changamoto zinazojitokeza ikiwemo mvua na mizigo kuchelewa kutoka bandarini.
“Hii kazi iliyofanywa hapa ni kubwa kwani wenzetu wameifanya ndani ya miezi sita jambo ambalo sio kawaida nawapongeza sana,” amesema Dk Mwinyi; na kwamba ameridhika baada ya kuona yale waliyokubaliana ndiyo yanafanyika kwa kuzingatia ubora unaotakiwa.
Rais Mwinyi amesema ni jambo la kujivunia kama taifa kuwa na uwanja mzuri wa aina yake ambao utatumika katika michezo ya kitaifa na kimataifa hususani mpira wa miguu.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Ilhan Karadeniz, amesema wameshakamilisha hatua kubwa ya ujenzi wa kiwanja hicho na kazi iliyobakia ni ndogo hivyo wanaamini ndani ya mwezi mmoja watakamilisha na kuukabidhi serikalini.
Uwanja huo utakaokuwa na uwezo wa kuchukua watu 15,500 kwa wakati mmoja, umefanyiwa marekebisho makubwa kwa gharama ya zaidi ya Sh50 bilioni.