Uwanja wa Sh200 bilioni kujengwa Dar
KATIKA kuhakikisha vijana wanajiajiri, Serikali imetenga Sh200 bilioni kwa ajili ya kujenga uwanja-changamani (Sport Arena) kwa ajili ya kuibua vipaji.
Uwanja huo unaotarajiwa kuanza kujengwa katika eneo la Tanganyika Packers Kawe, Dar es Salaam mwaka huu utakuwa na uwezo wa kubeba mashabiki 16,000 hadi 20,000 na mwingine utajengwa jijini Dodoma.
Akizungumza juzi wakati akizindua mashindano ya Gwajima Super Cup, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa alisema pamoja na ujenzi wa Arena, fedha zimetolewa kwa ajili ya kurekebisha viwanja saba kwa kiwango cha kimataifa.
“Rais ametoa fedha kwa ajili ya kurekebisha viwanja saba kwa ajili ya mashindano ya mpira wa miguu,” alisema Mchengerwa na kuongeza.
“Pamoja na sekta hii kuwa na ushawishi mkubwa kwa serikali, rais alianzisha wizara hiyo kutokana na kuwa na maono makubwa,” alisema.
Akizungumzia mashindano hayo ya Gwajima Cup alisema kuwa kiongozi anayetaka kuacha alama ni yule aliye karibu na watu, hivyo lengo la mbunge huyo ni kuwashika mkono vijana wa Kawe.