Rais Mwinyi awataka wahitimu wachochee maendeleo

Muktasari:

  • Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi, amewataka wahitimu 2,102 katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar(SUZA) kuhakikisha maarifa waliyopata yanasaidia kutafsiri changamoto zilizopo na kuchochea maendeleo.

Dar es Salaam. Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi amesema wahitimu 2,102 wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) wana jukumu kubwa la kuchagiza maendeleo ya Zanzibar kwa kutumia maarifa waliyoyapata kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Rais Mwinyi ametoa kauli hiyo leo, Alhamisi Desemba 28,2023 wakati wa Mahafali ya 19 ya chuo hicho  yaliyofanyika Zanzibar huku akiahidi kuendeleza uwekezaji katika sekta ya ubunifu wa Tehama.

Rais Mwinyi amesema maarifa waliyoyapata ni lazima yakatumike kwa ajili ya kuchechemua maendeleo ya Wazanzibar kwa kutafsiri changamoto zinazowakabili kwenye jamii.

Kwa mujibu wa Suza, kati ya wahitimu 2,102, 1,229 ni wanawake (sawa na asilimia 58) ya wahitimu wote na waliobakia ni wanaume.

Wahitimu 43 ni shahada ya uzamili, 692 shahada ya kwanza, 999 stashahada na 367 astashahada.

“Nawapongeza hususani wanawake ambao kwa mara nyingine mmekuwa wengi na kushika nafasi za juu za bado mnayo safari ndefu, hatua hii ni mafanikio lakini mnatakiwa kujiendeleza,” amesema Rais Mwinyi ambaye ni mkuu wa chuo hicho.

“Pia ninawasihi mkatumie vizuri taaluma zenu kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya nchi na taaluma zenu, Serikali inaahidi kuongeza idadi ya wahadhiri na wakutubi kwa ajili ya kuongeza uwezo wa chuo katika utoaji wa maarifa yanayokwenda na kasi ya mageuzi ya kidunia.” amesema

Katika tukio hilo, Rais Mwinyi amemtunukia Rais Samia Suluhu Hassan Shahada ya Heshima ya Uzamivu ya katika usimamizi wa Utalii na Masoko.

Rais Mwinyi amesema ongezeko la wahitimu linaendana na uwekezaji wa Serikali katika utoaji wa mikopo ili kuwezesha vijana wote wenye sifa kupata elimu.

Ametoa wito kwa Bodi ya Mikopo Elimu ya Juu Zanzibar kuendelea kuzingatia hilo.

Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Mohamed Makame Haji ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuimarisha mazingira ya elimu na chuo hicho kinachoendelea kuongeza idadi ya wanataaluma.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Leila Muhamed Mussa amesema ndani ya miaka mitatu ya uongozi wa Rais Mwinyi, bajeti ya elimu imeongezeka kutoka Sh30 bilioni hadi Sh58 bilioni.

Kwa sasa Zanzibar ina vyuo vikuu saba tangu ilipopata uhuru miaka 60 iliyopita.