Dk Mwinyi ashtushwa viongozi kuchelewa kurejesha fomu za maadili

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akizungumza katika maadhimisho ya siku ya maadili na haki za Binadamu Unguja Zanzibar.
Muktasari:
- Kwa mujibu wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma hadi jana Desemba 18,2023 viongozi 922 sawa na asilimia 36 ndiyo waliorejesha fomu.
Unguja. Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi, amewakumbusha viongozi waliotajwa katika sheria ya maadili ya viongozi wa umma kwa mujibu wa vyeo na nafasi zao kuhakikisha wanajaza fomu za tamko la rasilimali na madeni na kuziwasilisha kwa wakati.
Amesema ameshtushwa na idadi ndogo ya waliorejesha fomu hizo mpaka sasa.
Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo, Jumatatu Desemba 19, 2023 katika maadhimisho ya siku ya maadili na haki za binadamu Unguja, Zanzibar.
Amesema fomu hizo zinatakiwa kurejeshwa kwa mujibu wa sheria kabla ya Desemba 31 na atakayeenda kinyume atachukuliwa hatua za kinidhamu.
Kwa mujibu wa Tume ya Maadili, hadi jana Desemba 18,2023 viongozi 922 sawa na asilimia 36 ndiyo waliorejesha fomu.
Mwaka jana 2022, watumishi 2,677 walirejesha fomu hizo na waliochelewa walikuwa 11 pekee.
“Nimeshtuka kuona wapo baadhi ya viongozi wanadhani hakuna hatua itakayochukuliwa ikiwa hujarejesha fomu kwa muda uliowekwa kisheria, basi tutaonana wabaya kwani hatutokubali, hakuna sababu ya mtu kutotii sheria na kutekekeza wajibu wako,” amesema.
Dk Mwinyi amesema bado kuna tatizo la kukosekana nyaraka za umiliki wa mali zilizoorodheshwa kwenye fomu za tamko la mali na ma deni.
Rais Mwinyi amesema viongozi wengi wameorodhesha mali ambazo ama hawajakamilisha taratibu za uhaulishaji au hawana nyaraka halisi za umiliki.
Akizungumzia malalamiko ya ukiukwaji wa sheria ya maadili dhidi ya viongozi wa umma, ambayo yanahusisha watendaji wa wizara, idara na taasisi za Serikali, amesema takwimu za uchambuzi zinaonyesha Ofisi ya Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ ndiyo inaongoza kuwa na taasisi zinazolalamikiwa.
Amesema kupitia uchambuzi wa malalamiko hayo, takwimu zinaonyesha matumizi mabaya ya madaraka ndiyo eneo ambalo linalalamikiwa zaidi ikilinganishwa na mengine.
Hivyo, amesema ni vyema wahusika wakajitathmini zaidi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, akiwataka viongozi wote waliopewa madaraka na dhamana kuyatumia kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazowaongoza.
Ameipongeza Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi (Zaeca) kwa kuokoa Sh2.3 bilioni.
Kati ya fedha hizo, Sh97.9 milioni zimerejeshwa kwa wananchi na Sh2.2 bilioni zimerejeshwa serikalini kutokana na makosa tofauti ya rushwa, uhujumu wa uchumi na ukiukaji wa maadili.
Ametaka Zaeca kuendelea kuungwa mkono kufanikisha ufuatiliaji wa miradi 49 ya maendeleo inayotekelezwa Unguja na Pemba yenye thamani ya takribani Sh652.9 bilioni.
Amesema Serikali imejipanga kuimarisha maadili, haki za binadamu na misingi ya utawala bora katika nchi, hivyo viongozi na wananchi washirikiane kuendeleza jitihada za kuimarisha utawala bora nchini.
Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, maendeleo yanayoonekana na yanayokuja yanatokana na kuwa na misingi imara ya utawala bora ikiwamo kusimamia utawala wa sheria, haki, uwajibikaji, uwazi, usawa, uadilifu, kuzuia rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.
“Suala la kuimarisha misingi ya utawala bora si la Serikali na taasisi zake pekee, bali ni la wote likijumuisha jumuiya za kimataifa, asasi za kiraia, sekta binafsi, viongozi wa dini, vyombo vya habari na wananchi kwa ujumla,” amesema.
Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Asaa Ahmad Rashid, amesema siku hiyo inatoa fursa ya viongozi wa umma kukaa pamoja kutafakari kwa kuwa wao ndio wenye jukumu na wajibu wa kupanga au kusimamia malengo ya Serikali.
Amesema pia inatoa fursa ya kujitathmini katika mapambano ya rushwa na ulinzi wa haki za binadamu ili kupatikana kwa maendeleo na ustawi wa Wazanzibari.
Asaa amesema hatua ya viongozi kuzingatia misingi ya utawala bora inachochea ufanisi wa utekelezaji wa mipango ya Serikali, hivyo kuwezesha kupatikana kwa huduma bora, maendeleo na ustawi wa jamii.