Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sanya hatasahaulika kwa mambo haya

Unguja. Aprili 21, mwaka huu Zanzibar ilimpoteza mwanasiasa mkongwe na machachari, Muhammad Ibrahim Sanya, ambaye alifariki dunia wakati akiendelea na matibabu katika Hospitali ya Lumumba, Unguja.

Sanya anatajwa kuwa machachari katika siasa za Zanzibar na alikuwa miongoni mwa wabunge waliopata fursa hiyo mapema mwanzoni mwa siasa za vyama vingi mwaka 1995.

Sanya amekuwa mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa vipindi vitatu kupitia Chama Cha Wananchi (CUF), kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2010, kabla ya mwaka 2015 chama chake kutompitisha wakati wa kura za maoni, licha ya kuibuka mshindi.

Katika kipindi hicho alikuwa mbunge wa jimbo la Mkunazini wakati huo, baadaye likaitwa jimbo la Mjimkongwe na sasa linaitwa jimbo la Malindi.

Wanasiasa waliofanikiwa kufanya naye kazi wanamuelezea Sanya kwamba alikuwa mpambanaji, mkweli, hodari wa kujenga hoja na alikosoa pale alipoona panahitaji kukosolewa kwa maslahi ya umma na alipongeza alipona kuna kitu kizuri kimefanywa bila kuangalia yeye ni chama gani.

Mchambuzi wa siasa za Zanzibar, Ali Makame ambaye kwa wakati huo alikuwa chama kimoja na Sanya, anasema ni mtu ambaye alikuwa mkweli katika utendaji kazi wake wa kazi na alikuwa anawapenda watu wa jamii zote.

“Alikuwa anapenda umoja, hakuwa mbaguzi, penye haki hakujali chama chake, aliwapenda wananchi wote bila kuangalia huyu ni wangu huyu chama kingine, huyu ni miongoni mwa viongozi tunaowataka kwa sasa wenye sifa kama hizo,” anasema.

Anasema ni miongoni mwa wabunge wakati huo alikuwa akifanya vizuri na alikuwa muumini wa kutoa misaada kwa akina mama na watoto ambapo alitenga fungu maalumu katika fedha yake mwanamke anapojifungua, bila kujali chama alikuwa akitoa vifaa vya kujifungua bila ubaguzi.

Kwa hiyo alipenda sana wajawazito na watoto kwa kujua umuhimu wao, hili ni jambo ambalo jimbo aliloongoza watamkumbuka sana.

Makame anasema kwa njia moja au nyingine, licha ya chama wakati mwingine kinakuwa na misimamo tofauti, alikuwa anaangalia zaidi uzalendo katika taifa lake badala ya maslahi ya kitu kingine.

“Kuna nasaha aliwahi kutoa kwenye chama namna gani ya kuunganisha umoja na siasa zao, kwa hiyo ni mtu ambaye kwa kiasi kikubwa ameondoka bado hajapata mrithi wa kufanana naye tangu alipokosa ubunge katika jimbo hilo, kwani hata waliochukua nafasi hiyo hawajamfikia,” anasema.

Pamoja na hilo, Sanya atakumbukwa kwa misimamo yake ya kujenga umoja katika jimbo aliloongoza.

Anasema jamii itamkumbuka zaidi katika jimbo, kwa jinsi alivyokuwa akiwaunganisha watu, licha ya kuwa alikuwa na asili ya Kihindi, lakini alijichanganya na watu wa aina zote.

“Wakati mwingine hata alipokuwa akienda kwenye mikutano anajichanganya na watu anazungumza kwa lugha Kimakunduchi kama yupo eneo hilo kulingana na mazingira aliyopo kwa wakati huo.

Anashauri iwapo kuna mtoto ambaye anaweza akafuata nyayo za baba yake afanye hivyo ili kuendeleza aliyoyafanya, kwani kilikuwa kioo cha jamii.

Naye Ali Saleh ambaye alichukua mikoba ya Sanya kuwa mbunge katika jimbo hilo mwaka 2010, anakiri Sanya alikuwa akipendwa na watu kwa sababu ya uzalendo wake na umahiri aliokuwa nao katika kuzungumza hoja.

Licha ya Sanya kuibuka mshindi wakati wa kura za maoni kupitia CUF, chama kilimteua Saleh ambaye alikuwa mshindi wa tatu kuwania nafasi hiyo na aliibuka mshindi wa kiti cha ubunge.

Saleh, aliyechuana mara mbili na Sanya katika kura za maoni kwa tiketi ya CUF mwaka 2015 na 2020, ambaye kwa sasa yupo katika Chama cha ACT Wazalendo, anakiri kwamba alikuwa machachari.

Anasema Sanya alikuwa mwanasiasa ambaye alichipukia mapema kwenye siasa na zikamkubali.

 Anasema alikuwa na sifa mbili kubwa: Kwanza alikuwa mtu wa watu na mara nyingi alikuwa akitembea na mkoba wake wa ukiri kila baraza anapita anazungumza na wananchi.

Sifa ya nyingine inayotajwa na Saleh kwa Sanya, alikuwa na karama ya kuzungumza, kwani alikuwa na nguvu ya kujieleza na mara nyingi hoja zake alizipangilia vizuri.

“Alikuwa anajua wapi apande, wapi ashuke, wapi apande tena akiwa anazungumza jukwaani, kwa hiyo alijua kujipangilia na vituo alivielewa, hilo lilimpa nafasi kubwa na kupendwa na watu,” anasema.

Anasema; “Ulikuwa ukipenda umsikilize akizungumza, alikuwa hodari kuzungumza katika majukwaa ya kisiasa, lakini hata bungeni alikuwa akisimama kuzungumza anazungumza vizuri sana.”

Anasema katika kura za maoni mwaka 2015, Sanya aliibuka mshindi na yeye Saleh alikuwa mshindi wa tatu, lakini chama kiliamua nafasi hiyo apewe yeye mshindi wa tatu.

Inadaiwa chama kiliamua kumuweka pembeni kwa madai kwamba utaratibu wake wa kutafuta kura haukuwa mzuri, hata hivyo duru za siasa zinadai kwamba chama kilimnyima nafasi hiyo kwa sababu ya misimamo yake na hakutaka kukwepesha jambo kwenye ukweli.


Sanya hatasahaulika kwa mambo haya

Hata hivyo, mpaka anafariki dunia, hakuwahi kusema kama aliondoka CUF na kujiunga na chama kingine na wala hakuonekana tena kujishughulisha sana na siasa hata hukohuko CUF.

Anasema kuenguliwa kwake katika kinyang’anyiro, pia kunatajwa kulimkasirisha na kumfanya ajiengue na masuala ya siasa.

Saleh anasema atakumbukwa kwa nguvu yake ya kujieleza na ukaribu na watu wengi, lakini alijenga alama ya CUF kwa Zanzibar.

“Hii ni alama yake kubwa kwa hapa, japo hakuna kitu ambacho unaweza kukiona kwa macho kwamba kimeachwa na Sanya wakati wa ubunge wake.”

Kutoonekana kwa alama ya moja kwa moja (physically) ni kutokana na sababu kwamba mbunge wa Zanzibar hana bajeti ya mfuko wa jimbo, anakuwa bungeni kwa sababu ya kutetea masula ya Muungano lakini hana fungu.

“Yeye aliipigania Zanzibar kwa ujumla wake, kwa hiyo ndio maana huwezi kuona labda kuna kitu amejenga ama vinginevyo, maana hakuna fedha za mfuko wa jimbo,” anasema.

Naye Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto, anasema Sanya ambaye kitaaluma alikuwa mwalimu, hakuwa na siasa za ukakasi.

Hata hivyo, anasema alianza kuvunjika moyo kwenye siasa baada ya chama chake kumkata jina lake na kuweka wagombea wengine.

“Alikuwa mwanasiasa mahiri, mtulivu akipangilia hoja zake, lakini baada ya pale alipoteza ladha na hamu ya siasa, hakuwa tena wa kujishirikisha na siasa,” anasema Mbeto.

Mbali na kuwaunganisha wananchi wake kuwa kitu kimoja, pia anatajwa alifanikiwa kuunganisha madhehebu yake.

Anasema licha ya Sanya kutowahi kurejea CCM, katika kipindi cha miaka saba ya ugonjwa wake alikuwa akizungumza mara kwa mara na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akimshauri masuala mbalimbali. “Alikuwa ni mtu ambaye anazungumza naye anamshauri kila mara, kwa hiyo amekuwa karibu naye sana, maana tangu awali Sanya hakuwa na siasa za kupinga, bali alitaka kuona maendeleo kwa kila mtu.”

Kupitia kipawa chake cha ualimu, Sanya ameandika vitabu vingi ambavyo vinatajwa vitaanza kutolewa muda mfupi ujao.

Anaelezwa hakuwa na siasa za kupinga kila kitu, alikuwa anakosoa pale panapostahiki kwa maslahi ya jamii, nakumbuka alizungumza sana katika maboresho ya elimu kwa maana ya majengo, taaluma na vifaa vya kufundishia na ndio ukiangalia hata maeneo ambayo Serikali imewekeza zaidi.

Mbeto anasema: “Kwa hiyo alichokuwa akipinga Sanya ujue kina maslahi kwa Wazanzibari wote na Watanzania, kama jambo linakwenda vizuri atapongeza, akiona halipo sawa atapinga kwa namna ya kushauri na jinsi ya kulifanya.”

Kupitia msingi huo, Mbeto anasema Sanya ameacha funzo kwenye siasa, siyo kila wakati ukimuona mpinzani ni adui na siyo kila wakati mpinzani akiona chama tawala ni adui, kikubwa ni kusimamia hoja.