Serikali za mitaa Mjini Magharibi zatakiwa kubuni miradi ya mapato
Meya wa Jiji la Zanzibar, Kamal Abdulsatar Haji akizungumza baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa Zanzibar (ZALGA) katika ofisi za Baraza la Jiji Unguja Zanzibar
Muktasari:
- Hatua hiyo mbali na kuharakisha maendeleo kwa wananchi lakini itachochea ukuaji wa uchumi wa Zanzibar.
Unguja. Watendaji wa serikali za mitaa wamehimizwa kubuni na kuendeleza miradi itakayoongeza mapato katika mamlaka zao.
Wito huo umetolewa leo Jumapili Juni 7, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Moh’d Ali Abdallah, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Viongozi wa Jumuiya ya Mamlaka za Serikali za Mitaa Zanzibar (ZALGA) uliofanyika katika Baraza la Jiji la Zanzibar.
Abdallah amesema ongezeko la mapato katika mamlaka za serikali za mitaa litasaidia kuboresha utoaji wa huduma za kijamii, kuimarisha miundombinu na kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.
Amesema ni wajibu wa mamlaka hizo kutumia rasilimali zilizopo kwa ufanisi na kutafuta vyanzo vipya vya mapato vinavyoendana na mazingira yao.
“Serikali za mitaa zinapaswa kubuni miradi itakayoongeza mapato na wakati huohuo kusaidia kutatua changamoto zilizopo katika jamii. Ni muhimu kuanzisha miradi ya usimamizi wa taka ili kuhakikisha miji yetu inabaki safi na yenye kuvutia,” amesema Abdallah.
Pia, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha huduma za usafiri na kupendezesha miji kwa njia endelevu ili kuendelea kuvutia uwekezaji na kuboresha maisha ya wananchi.
Aidha, amezitaka mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha zinakusanya kodi stahiki na kuziba mianya yote inayosababisha upotevu wa mapato ya umma.
Katika mkutano huo, Meya wa Jiji la Zanzibar, Kamal Abdulsatar Haji amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa ZALGA.
Akizungumza baada ya uchaguzi huo, amesema yupo tayari kuwaunganisha madiwani wa Unguja na Pemba ili kuimarisha ushirikiano na kusukuma mbele ajenda za maendeleo ya serikali za mitaa Zanzibar.
Amesema viongozi na wanachama wa ZALGA wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ili kuimarisha utendaji wa jumuiya hiyo.
“ZALGA ya sasa itakuwa tofauti na ilivyokuwa awali. dhamira yetu ni kuleta mabadiliko chanya yatakayowanufaisha wanachama wetu, mamlaka za serikali za mitaa na wananchi kwa ujumla,” amesema Kamal.