Umeme wa upepo kuibadili Zanzibar

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nishati na Madini, Joseph Kilangi (kulia) na Mkurugenzi wa mradi wa Kampuni ya Powgex Energy, Charles Lwanda    wakibadilishana nyaraka baada ya kusaini makubaliano ya kuzalisha megawati 450 za umeme Zanzibar jana. Picha na Jesse Mikofu.


Unguja. Zanzibar inakwenda kuandika historia baada ya kusaini makubaliano na kampuni ya Powgex Energy Proprietary Ltd ya Austria, ya kuzalisha umeme wa upepo wa megawati 450, kiwango ambacho ni zaidi ya mara tatu ya kinachopatikana sasa.

Kwa sasa Zanzibar inapokea megawati 125 kutoka Tanzania Bara kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na uwezo wake wa matumizi umefikia zaidi ya asilimia 90, hivyo umeme utakaopatikana utaisaidia kujitanua zaidi kichumi kupitia uwekezaji.

Makubaliano hayo yaliwekwa  saini jana kati ya kampuni hiyo na Wizara ya Maji, Nishati na Madini na uwekezaji huo utagharimu Dola za Marekani 1.2 bilioni, sawa na Sh3 trilioni.

Akizungumza wakati wa kusaini makubaliano hayo, Katibu Mkuu Wizara hiyo, Joseph Kilangi alisema mradi huo ukikamilika utakuwa mkombozi katika sekta ya nishati na kwamba tatizo la umeme litabaki historia visiwani humo.

“Huu ni mradi mkubwa kuwahi kutokea kisiwani hapa, hata miundombinu yake ni rahisi kwa sababu inawekwa baharini kwa hiyo hakuna usumbufu kwa wananchi wala uharibifu wa mazingira,” alisema Kilangi.

Alisema chini ya makubaliano hayo, megawati 300 zitazalishwa Unguja na zingine 150 zitazalishwa Pemba.

Katika awamu ya kwanza ya mradi, Unguja zitazalishwa megawati 50 na Pemba megawati 100.

Waziri mwenye dhamana ya nishati, Hassan Shaib Kaduara alitaka makubaliano hayo yasibaki kwenye makaratasi bila kuona utekelezaji wake.

“Tunawapongeza wawekezaji hawa kuona Zanzibar kuwa sehemu ya kuwekeza, tunawakaribisha wawekezaji wengine tunaendelea kuwekeza, na mazingira mazuri yamewekwa kuwapokea,” alisema Shaib.

Alisema kwa sasa Zanzibar ina uhitaji wa wastani wa megawati 130 za umeme, kati ya hizo, Unguja inahitaji megawati 115 na Pemba 15.

Hii ni kampuni ya tatu kusaini mktaba wa uzalishaji umeme  kwa kutumia vyanzo jadidifu baada ya  Kampuni ya ESR ya Ujerumani ambayo itazalisha umeme jua wa megawati 15 Pemba na Kampuni ya Taifa Group na Generation Capital ambazo zitazalisha megawati 180 kwa nguvu za jua.

Waziri huyo alisema kwa kampuni ya Powgex Energy wamesaini MoU ili ianze kufanya upembuzi yakinifu na utafiti na itatumia kipindi cha mwaka mmoja katika upembuzi huo.

“Lengo la Serikali ni kuona vyanzo tofauti. Inatafuta vyanzo mbadala kwa sababu kuna miradi mikubwa ya bandari, viwanja vya ndege, hoteli kubwa zinajengwa na viwanda ambavyo vinahitaji umeme mkubwa,” alisema Shaib.

“Huwezi kuzungumzia uchumi bila kutaja umeme, kwa hiyo hivi vyote vinavyojengwa, vinavyonataka kujengwa na mengine ili tuweze kujenga uchumi endelevu umeme ni nambari moja,”  alisema.

Kuhusu Zanzibar kujitosheleza kwa umeme, Waziri Kaduara alisema “hata kama tukijitosheleza kwa sasa, kuna programu ambayo inaruhusu nchi moja kuiuzia nchi jirani, kwa hiyo hata sisi tukiwa na ziada tunaweza kuwauzia wengine.”

Mkurugenzi wa mradi kutoka kampuni ya Powgex Energy, Charles Lwanda alisema mazingira mazuri na wezeshi yaliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ndiyo yamevutia kampuni hiyo ya kimataifa yenye uzoefu katika uzalishaji wa umeme, kuwekeza kisiwani humo.

Alisema mradi huo unaokadiriwa kufikia Dola za Marekani 1.2 bilioni, utaisaidia Zanzibar si tu kufikia malengo yake, bali pia kuwa na kiwango cha ziada cha mahitaji ya umeme.

Alisema makubalino hayo ni kwa ajili ya kufanya utafiti,  upembuzi yakinifu na kuwa na mpango wa mradi kuanza uzalishaji wa kiwango hicho cha umeme.

“Hii itahusisha upembuzi yakinifu na ujenzi wa miundombinu kwa lengo la kuzalisha na kusimika mitambo ya kuzalisha umeme Zanzibar.

“Pia mradi huu utasaidia kutunza mazingira kwa kuwa miundombinu yake inawekwa baharini na pwani,” alisema.

Alisema umeme huo utazingatia matumizi ya umeme wa viwandani na kupeleka nje kupitia teknolojia za nyaya za baharini.

“Umuhimu wa mradi huu ni kuwa na nishati endelevu na ya kudumu, kupunguza hewa ukaa na kulinda mazingira na kiuchumi iutasaidia kwenye uzalishaji na kutoa fursa za ajira za ndani,” alisema.