Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Viongozi 28, wanachama 120 wabwaga manyanga Chadema

Baadhi ya waliokuwa viongozi na wanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa mikoa ya Unguja na Pemba  wakionyesha kadi zao baada ya kutangaza kujivua nafasi zao na kuachana na chama hicho leo Mei 20, 2025 Mjini Unguja. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

  • Viongozi walioachia ngazi wamo wa majimbo, wilaya na mikoa yote ya Unguja na Pemba.

Unguja. Zaidi ya viongozi na wanachama 200 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) visiwani Zanzibar wamejivua nyadhifa na kujiondoa rasmi katika chama hicho, wakidai kuwepo kwa ubaguzi na ukandamizaji kutoka kwa viongozi wa juu wa chama hicho.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku mbili tu baada ya wajumbe sita wa sekretarieti ya Chadema kisiwani hapa kutangaza kujivua nafasi zao, hatua iliyozua gumzo katika medani ya siasa za upinzani Zanzibar.

Kati ya waliotangaza kujiondoa, viongozi 28 walikuwa wakihudumu katika ngazi mbalimbali za uongozi kuanzia majimbo ya uchaguzi, wilaya hadi mikoa yote ya Unguja na Pemba.

Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Said Mzee Said akizungumzia kuondoka kwa wanachama hao amesema Chadema siyo jela anayetaka kuondoka aondoke, kwani hiyo ndio safari ya kisiasa na wengi wanaojiondoa ni kwa sababu ya maslahi yao binafsi na siyo chama.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi na wanachama hao leo Machi 20, 2025 Mjini Unguja, Atfat Hamad Ali ambaye alikuwa Katibu wa Vijana Wilaya ya Magharibi B na Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa, amesema wamefikiwa hatua hiyo baada ya kuona wakitengwa.

"Kwa ujumla viongozi saba wa wilaya zote mbili za Pemba na viongozi 13 wa wilaya za Unguja, wenyeviti wawili wa Mkoa wa Kaskazini na Mjini Magharibi na viongozi sita wa Mkoa wa Kusini Pemba, tumeondoka rasmi Chadema," amesema.

Amesema jumla ya wanachama 80 kutoka Pemba na wanachama 120 kutoka Unguja, wamejivua rasmi nafasi zao na kuachana na chama hicho.

Aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Wilaya ya Mjini, Muslim Khamis Rajab amesema wamejiondoa kutokana na malengo yao kupotea na ndoto za Watanzania kupotea kutokana na siasa zilivyo hivi sasa na viongozi hawajali demokrasia kama wanavyohubiri.

Amesema chama watakachojiunga watabainisha baadaye kadri muda unavyokwenda.

"Kinachoendelea katika chama hiki ni ukandamizaji, ubaguzi na kutothaminiana katika chama, na chama hichi kwa upande wetu Zanzibar huwa kinaishia kwenye makablasha," amesema.

Mwingine Mwajuma Ali Khamis aliyekuwa Mwenyekiti wa Jimbo la Mkoani amesema haondoki kwa mkumbo bali ametafakari na kuona hakuna mwelekeo katika siasa za ukumbozi.

Viongozi waliokuwa wajumbe wa Sekretarieti walitangaza kujiondoa chama hicho Mei 17, 2025 wakiongozwa na Mkuu wa Idara ya Oganaizesheni Mafunzo, Sera na Uchaguzi, Haji Abeid Haji.

Viongozi wengine ni Ofisa Utawala na Fedha, Rahima Said Abdallah, Ofisa Utawala, Kassim Abdallah, Katibu wa Chadema Kanda ya Unguja, Yunus Makame, Katibu wa Chadema Kanda ya Pemba, Habib Ali Khamis na Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Asiata Said Abubakar.

Wajumbe hao wamejiondoa nafasi zao na kujivua uanachama wa chama hicho wakidai kuwa uongozi uliochaguliwa hawakai vikao kuzungumzia mpango madhubuti wa kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.

Vuguvugu la viongozi wa chama hicho kujiondoa katika nafasi zao lilianza Mei 7, 2025 kwa wanachama waliokuwa katika Sekretarieti ya uongozi wa Freeman Mbowe kutangaza kuondoka ndani ya chama hicho kwa kile walichodai chama kimekosa mwelekeo.

Akizungumzia hilo, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Said Mzee Said amesema Chadema siyo jela anayetaka kuondoka aondoke, kwani hiyo ndiyo safari ya kisiasa na wengi wanaojiondoa ni kwa sababu ya maslahi yao binafsi na siyo chama.

Amesema chama hicho hakina imani na wajumbe hao na kwamba walikuwa wameshapewa onyo kulingana na mwenendo wao katika chama.

"Napenda kuthibitisha hilo kwamba tulikuwa hatuna imani nao, kwa sababu walikuwa wanaendelea kuwasiliana na naibu mstaafu, walikuwa wakisubiri hii fursa na tulikuwa tunawatilia shaka ndio maana wameamua kujivua,"amesema Said. 

Amesema, Kamati maalumu ya chama hicho inakaa Mei 25 na 26 mwaka huu na moja ya ajenda zake ni kufanya mabadiliko kwa baadhi ya viongozi hivyo wamejiwahi kujiondoa.