Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wananchi walalamikia wizi wa mazao Kaskazini Unguja, RC atia neno

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mattar Zahor Masoud akizungumza na baadhi ya wananchi wa Mkoa Ofisi kwake, Mkokotoni.

Muktasari:

  • Wakati wananchi wakilia na vitendo vya wizi, Serikali imeeleza ilivyojipanga kukabiliana na vitendo vyote vya uhalifu.

Unguja. Wananchi Mkoa wa Kaskazini Unguja wameiomba Serikali kufanya operesheni za mara kwa mara katika maeneo yanayotajwa kushamiri kwa vitendo vya wizi wa mazao, mifugo na uuzaji wa dawa za kulevya ili kuwapunguzia kadhia wanayokutana nayo.

Hayo wameyasema leo Julai 8, 2025 katika kikao cha mwezi kilichowakutanisha baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja na Mkuu wa Mkoa huo, Mattar Zahor Masoud.

Akizungumza katika kikao hicho, Khadija Kombo Shaib amesema kuna tabia za wizi wa mazao katika maeneo yao hivyo zinatakiwa kuwapo operesheni kubwa na endelevu, kwani wizi huo huwafanya waendelee kuwa maskini.
“Serikali isilegeze kupambana na wizi kwani vijana wetu wanaharibiwa na dawa za kulevya ndio sababu ya kuwa wezi wa mazao na mifugo,” amesema Khadija ambaye ni mkulima kutoka Donge.

Naye, Fatma Rajab Ismail amesema maeneo yenye changamoto hizo hatua za haraka zichukuliwe ili kudhibiti uhalifu na biashara haramu ikiwemo dawa za kulevya.

Haji Said Mbarouk amesema tabia hizo zinawarejesha nyuma katika jitihada zao za kuendeleza kilimo na uchumi wao.

Akijibu hoja za wananchi hao, Mattar Masoud ambaye pia ndio mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo, amekiri kupata taarifa hizo za wizi wa mazao na tayari wamejipanga kuhakikisha wanatokomeza hali hiyo ili kila mwananchi anufaike na shughuli anayoifanya.

Mattar amesema katika kukabiliana na hilo mkoa kwa kushirikiana na Serikali za wilaya pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama imeanzisha kampeni maalumu ya kuzuia na kutokomeza kabisa vitendo hivyo.

“Hatutakubali mkoa wetu kuwa kichaka cha wahalifu, amani na utulivu ni msingi wa maendeleo, na sisi kama viongozi tunawajibika kuhakikisha vinadumu, kwa hiyo niwatoe hofu hatua zimeshaanza kuchukuliwa,”amesema.

Hata hivyo, ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na Serikali kwa kutoa taarifa za uhalifu na kuepuka kuficha wahalifu kwa misingi ya undugu au muhali, kwani wanapohitaji mafanikio lazima jamii iwe sehemu ya suluhisho