Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zanzibar kuanzisha soko la hisa

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Juma Malik Akil akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27 Baraza la Wawakilishi Chukwani Unguja Zanzibar

Muktasari:

  • Katika mwaka wa fedha 2026/26 Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar inakusudia kutumia Sh2 trilioni kutekeleza vipaumbele tisa

Unguja. Pamoja na mwenendo wa hali ya uchumi na teknolojia ya mifumo ya kielektroniki katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kudhibiti upotevu wa mapato, Wizara ya Fedha na Mipango imejipanga kutekeleza vipaumbele tisa huku akikadiria kukusanya Sh8 trilioni.

Miongoni mwa vipaumbele hivyo ni kusimamia uanzishwaji wa Benki ya Uwekezaji (ZIB) na Soko la Hisa la Zanzibar (ZSM).

Hayo yameibainishwa leo Jumatatu Juni 8, 2026 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Juma Malik Akil wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo barazani.

Ameliomba Baraza la Wawakilishi kuhidhinisha Sh2 trilioni kwa ajili ya matumizi ya wizara hiyo.

Dk Akil amesema mipango ya wizara ni kuimarisha matumizi ya kidijitali katika upangaji na utekelezaji wa bajeti ya Serikali pamoja na kusimamia utekelezaji wa bajeti inayozingatia usawa wa kijinsia.

“Katika kipindi hiki wizara itaanzisha Soko la Hisa la Zanzibar na benki ya uwekezaji,” amesema.

Dk Malik amesema wizara itakamilisha Mpango wa Maendeleo wa Muda wa Kati (ZADEP 2026–2031) pamoja na nyaraka saidizi ikiwamo mwongozo wa uandaaji wa upembuzi yakinifu na mwongozo wa uandaaji wa mipango mikakati ya kisekta na kuratibu utekelezaji wa tafiti za kimkakati Zanzibar.

Amesema katika kuandaa na kupitia sera, sheria na kanuni, wizara unakusudia kufanya mapitio ya Sheria ya Ongezeko la Thamani (VAT) namba 4 ya mwaka 1998 na kuandaa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) na sera ya idadi ya watu na miongozo ya ununuzi wa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) pamoja na makundi maalumu.

Kipaumbele kingine ni kuanzisha, kuimarisha na kukuza matumizi ya mifumo ya kielektroniki pamoja na kuunganisha mifumo ili iweze kuoana na kuanzisha bima za kilimo pamoja na kampuni tanzu ambayo inasimamia bima ya maisha.


Maoni ya kamati

Akisoma maoni ya kamati ya bajeti kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo, mjumbe wa kamati hiyo, Bakar Hamad Bakar amesema kutokana na mwenendo wa mapato na matumizi, kamati inaishauri wizara kuongeza usimamizi wa makusanyo ili kufikia malengo na kuziba mianya ya upotevu wa mapato, kusimamia ipasavyo mapato yatokanayo na uendeshaji wa masoko ili kurejesha fedha za ujenzi katika mfuko mkuu wa Serikali.

Pia, kamati imeshauri kuweka mikakati ya kuhakikisha kasi ya ongezeko la deni la Taifa inaendana na ulipaji wake, pamoja na kufanya uhakiki wa kitaalamu wa mfumo wa bajeti na matumizi ya Serikali (Bamas) ili kubaini na kutatua changamoto zinazoukabili mfumo katika uingizaji wa taarifa za bajeti za wizara na taasisi za Serikali.

Pia,  imeshauri kuweka bayana mambo muhimu yaliyobainika katika kaguzi zilizofanyika katika taasisi za Serikali, sambamba na ofisi kuwa na ufanisi zaidi katika kutumia miongozo ya ukaguzi kwa taasisi za Serikali na kuandaa ripoti zitakazotoa matokeo ya ukaguzi pamoja na hatua zinazohitajika kuchukuliwa ili kuimarisha uwajibikaji, uwazi na utawala bora.

“Kamati inaishauri Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kufikia makubaliano kuhusu usimamizi wa mapato yatokanayo na ukodishaji wa mashamba,” amesema.

Kamati pia, inaishauri Serikali kuongeza usimamizi katika eneo la upatikanaji wa fedha za mradi wa takwimu za jinsia ili kuondoa changamoto ya utekelezaji mdogo uliobainika, sambamba na kuimarisha uwezo wa taasisi husika katika ukusanyaji, uchambuzi na matumizi ya takwimu ili ziweze kutumika ipasavyo katika kupanga na kutekeleza sera na mipango ya maendeleo.

Wakichangia bajeti hiyo, baadhi ya wajumbe wa baraza la wawakilishi wamesisitiza wizara kubuni vyanzo vipya vya mapato na kusimamia mapato.

Mwakilishi wa Magomeni Mahfoudh Abdallah Mohamed (CCM) ametaka Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) kukusanya fedha bila kuwasumbua walipakodi na kufunga biashara jambo ambalo halina afya kwa biashara.

Hoja hiyo pia imezungumziwa na Mwakilishi wa Tumbe, Mmanga Mohamed Hamed (ACT- Wazalendo) amesema wapunguze kufungia biashara badala yake watafute mbinu mbadala ya kukusanya mapato.

Mwakilishi wa Ole  (ACT- Wazalendo), Seif Hamad Suleiman amesema kuna maeneo fidia imekuwa changamoto licha ya wananchi kufanyiwa tathmini

Mwakilishi wa Amani (CCM), Masoud Amour Masoud amesema mambo mengi yanayojadiliwa kwenye bajeti hiyo yameshajadiliwa kwenye wizara zingine, hivyo kikubwa ni kusimamia utekelezaji wake.

Mwakilishi wa Pandani (ACT-Wazalendo), Profesa Omar Fakih Hamad amesema licha ya nchi kutaka kuelekea kwenye sera za ununuzi wa kielektroniki hakuna miongozo inayoeleweka na ya wazi kuhusu jambo hili.

 “Mimi sikubaliani na mifumo ya ununuzi ya vifaa katika elektroniki, bado kuna ufisadi mkubwa wa kijamii, ndio biashara inayoendelea katika biashara hii,” amesema.

Pia, Profesa Fakih ameshauri Serikali kutenganisha wizara hiyo, fedha ibaki pekee yake na kuwepo na wizara inayosimamia mipango tofauti na ilivyo sasa, kwa kuwa  kufanya kazi zote mbili chini ya wizara moja kunasababisha mkwamo kwa namna fulani.