Majaliwa ataka elimu ya hisa isiishie vyumbani
Waziri Mkuu mstaafu, Kassim Majaliwa akizungumza katika haflaya uzinduzi wa ununuaji Hisa Stahiki za benki ya Mwalimi (Mwalimu Bank PLC).
Muktasari:
- Bado anaona jamii haijawa na elimu kuhusu biashara hiyo inavyofanyika na faida inavyopatikana katika masoko hayo.
Dar es Salaam. Mamlaka zinazohusika na usimamizi wa ununuzi na uuzaji wa hisa zimetakiwa kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuwekeza katika hisa badala ya elimu hiyo kubaki nayo chumbani.
Majaliwa amezitaja mamlaka hizo kuwa ni pamoja na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Wito huo umetolewa leo Jumatano Mei 6, 2026 na Waziri Mkuu mstaafu, Kassim Majaliwa alipokuwa akizindua uuzaji wa hisa stahiki zinazouzwa na Benki ya Mwalimu (MCB Bank) kwa wanahisa wake kwa Sh110 kwa hisa moja, kwa uwiano wa tatu kwa moja, kutoka Sh1,700 hadi Sh1,800 waliyokuwa wakiuziwa awali.
Amesema ununuzi wa hisa ni uwekezaji mzuri na wa uhakika, ambapo bado anaona jamii kubwa ya Watanzania haijawa na elimu kuhusu biashara hiyo inavyofanyika na faida inavyopatikana.
Waziri Mkuu mstaafu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na menejimenti ya Mwalimu Bank PLC.
“Ninasikia faraja kusikia hapa kwenye taarifa zenu kwamba Tanzania tunaongoza katika nchi za Afrika Mashariki katika biashara ya hisa, kwani kipindi cha nyuma tulikuwa nyuma kwa sababu bado tulikuwa tunajifunza.
“Hivyo ni wakati sasa mamlaka mnazosimamia hili kuendelea kutoa elimu ya umuhimu wa jamii kuwekeza huko badala ya kubaki nayo chumbani wenyewe, kwani hii ni sehemu ya uhakika katika uwekezaji,” amesema Majaliwa ambaye ni mmoja wa waasisi wa benki hiyo.
Kuhusu ununuzi wa hisa stahiki, Majaliwa amesema unatoa fursa kwa wanahisa wote, akiwemo yeye mwenyewe, kuongeza umiliki katika benki hiyo.
Majaliwa katika shughuli hiyo ya uzinduzi aliweza kununua hisa 30, akiwa tayari anamiliki hisa 4,000.
Mwenyekiti wa bodi Benki ya Mwalimu, Francis Ranadhan, akizungumza wakati wa uzinduzi uuzwaji wa 'Hisa Stahiki' zinazouuzwa na benki hiyo
“Kwa maneno mengine, hii ni fursa siyo tu ya kifedha, bali fursa ya kuchangia ukuaji wa benki yetu, na kwa pamoja kuchangia katika maendeleo ya uchumi wa taifa letu,” amesema Majaliwa.
Akielezea namna ya ununuzi wa hisa hizo utakavyokuwa, Mwenyekiti wa bodi wa benki hiyo, Francis Ramadhan amesema wanahisa wote ambao majina yao yapo kwenye rejesta ya wanahisa hadi kufikia Mei 5, 2026 wana haki ya kununua hisa mpya tatu (3) kwa kila hisa moja (1) waliyonayo.
Ramadhan amesema hisa hizo zitauzwa kwa bei ya punguzo ya Sh110, ambapo dirisha la ununuzi wa hisa stahiki limefunguliwa kuanzia leo na litaendelea mpaka Juni 5, 2026, na wanahisa wataweza kununua hisa za benki kidijitali, kugusa ofisi za Chama cha Walimu (CWT), matawi na ofisi za Benki ya Mwalimu.
“Hatua hii ni muhimu sana kwani inalenga kuimarisha mtaji wa benki, kuwezesha ukuaji endelevu wa biashara na kuboresha huduma tunazotoa kwa wateja wetu kote nchini.
“Hivyo tunawahimiza wanahisa kushiriki ili kuhakikisha kuwa benki yetu inapata mtaji wa ziada utakaosaidia kupanua wigo wa mikopo, kuimarisha huduma za kidijitali na kutimiza viwango vya kisheria vya mtaji vilivyowekwa na BoT,” amesema Mwenyekiti huyo.
Waziri Mkuu mstaafu, Kassim Majaliwa (wa nne kushoto), akiwa anafurahia na menejimenti ya Mwalimu Bank PLC wakati hafla ya uzinduzi wa uuzwaji wa Hisa Stahiki zinazouzwa na benki hiyo.
Awali, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Mwalimu, Richard Makungwa akitoa taarifa kuhusu ufanisi wa benki hiyo, amesema kwa miaka mitano iliyopita wamepiga hatua ikiwemo kwenye mizania ongezeko la mali kutoka chini ya Sh30 bilioni mwaka 2019 hadi Sh98 bilioni mwaka 2025, ukuaji unaoakisi ufanisi wa usimamizi wa rasilimali na kuongezeka kwa shughuli za kibenki.
Kwa upande wa amana za wateja, amesema zimeongezeka kutoka wastani wa Sh16 bilioni mwaka 2019 hadi kufikia Sh75 bilioni mwaka 2025.
Huku mikopo ikiongezeka kutoka Sh16 bilioni mwaka 2019 hadi Sh66 bilioni mwaka 2025.
“Katika mikopo tunalenga zaidi wateja binafsi, hususan walimu, watumishi wengine, wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs) ambao ni nguzo za uchumi wa taifa,” amesema.
“Kwenye upande wa faida, faida kabla ya kodi imeongezeka kutoka hasara ya Sh4.8 bilioni (2019) hadi faida ya Sh487 milioni (2025), ikiashiria mwenendo chanya wa kibiashara na usimamizi bora wa gharama.”
Naye mwakilishi kutoka DSE, Sara Mrema amesema hadi kufikia mwaka 2026, soko la hisa limefikia Sh33.3 trilioni huku kampuni 28 zikiwa zimeorodheshwa na kuwa na wawekezaji wapatao 800,000.
Hata hivyo, amesema Sh20.4 bilioni zinazotarajiwa kukusanywa kupitia hisa stahiki za benki hiyo zitasaidia kuongeza mtaji wa soko hilo na kuboresha huduma za kibenki kwa wananchi, ikiwemo mikopo.