Ajali ya Dk Kigwangalla yaondoka na mwanahabari wa pili, Lugola ageuza kibao

Waziri wa Maliasili na Utalii,Dk Hamis Kigwangala akisaidiwa na maafisa afya wa hospitali ya mkoa ya Mount Meru baada ya kushuka kwenye helkopta akitoka eneo Magugu wilaya ya Babati mkoa wa Manyara alikopata ajali  ya gari jana.Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

  • Jana, gari la waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla lilipata ajali katika eneo la Magugu mkoani Manyara, huku kiongozi huyo akipata majeraha sehemu mbalimbali za mwili.

Dar es Salaam. Mzimu wa ajali za barabarani umetafuna maisha ya maofisa habari wawili wa Serikali katika kipindi cha siku nane.

Jana, gari la waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla lilipata ajali katika eneo la Magugu mkoani Manyara, huku kiongozi huyo akipata majeraha sehemu mbalimbali za mwili.

Katika ajali hiyo, ofisa habari wa wizara hiyo, Hamza Temba alifariki dunia.

Ajali hiyo imekuja ikiwa ni siku nane tangu gari la Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji lilipopata ajali Katoro mkoani Geita na kusababisha kifo cha ofisa habari wa wizara hiyo, Shadrack Sagati. Ajali hiyo ilitokea Julai 28.

Ajali hiyo, licha ya kuchukua maisha ya Sagati aliyezikwa jana wilayani Bunda, watu wanne walijeruhiwa akiwamo naibu katibu mkuu wa wizara hiyo, Ludovick Nduhiye; dereva Lucas Wambura; mchumi wa wizara, Nickson Matembo na Yusuph Mbwalwa.

Dk Kigwangalla na wenzake

Kaimu mganga mkuu wa Wilaya ya Babati, Dk Madama Hossea alitaja majina ya majeruhi wa ajali hiyo mbali na waziri kuwa ni mwandishi wa habari Michael Mlingwa (30) na msaidizi wa waziri, Ramadhan Magumba (30).

Dk Hossea alisema dereva wa gari hilo Juma Saleh (59) na katibu wa waziri, Ephraim Mwangombe (47) hawakupata jeraha lolote na kwamba, walitoka salama kwenye ajali hiyo.

Baada ya ajali hiyo, Dk Kigwangalla alitibiwa kwa muda katika Kituo cha Afya Magugu kisha akasafirishwa kwa helikopta hadi Hospitali ya Selian mkoani Arusha kwa matibabu zaidi kabla ya badaye kusafirishwa kupelekwa Dar es Salaam. Alipofikishwa hospitali ya Selian mjini Arusha, viongozi mbalimbali wa Serikali wa mkoa huo na mawaziri waliokuwa mjini humo kikazi walifika kumjulia hali.

Mwananchi liliwashuhudia viongozi hao wakiongozwa na mkuu wa mkoa, Mrisho Gambo wakiwa katika eneo la hospitali. Viongozi wengine waliokuwapo ni mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira; waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina; naibu waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa mkoa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi alisema licha ya Kigwangalla kuendelea vizuri kuna haja ya kupata matibabu zaidi na ndio maana alikuwa anasafirishwa kupelekwa Dar es Salaam.

Awali, kamanda wa polisi Mkoa wa Manyara, Augustine Senga alisema ajali hiyo ilihusisha watu sita waliokuwa wakisafiri kutoka Arusha kwenda Dodoma ambapo mmoja alifariki dunia, watatu walijeruhiwa na wawili walitoka salama.

Alisema chanzo cha ajali hiyo ni twiga aliyekatiza barabara ghafla na dereva wa gari katika jitihada za kumkwepa liliyumba kushoto na kulia kisha likapinduka.

Taarifa ya wizara hiyo iliyotolewa jana mchana ilisema mwili wa marehemu Temba (32), unatarajiwa kuzikwa leo Jumapili saa saba mchana kijijini Masama wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.

Lugola na madereva serikalini

Wakati ajali hizo zikiibua mijadala mbalimbali mitandaoni, jana waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alisema magari ya Serikali ndiyo yanayoongoza kwa kuvunja sheria za barabarani.

Akizungumza wakati akizindua Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Lugola alisema viongozi wa umma ni lazima waonyeshe mfano katika kufuata sheria.

“Kwa mujibu wa taarifa za polisi, magari ya Serikali na hasa ya viongozi ndiyo yanayoongoza kwa uvunjifu wa sheria,” alisema. Alisema ameshaagiza polisi wasiangalie cheo, bali wakamate.

Lugola alisema madereva wakiendesha kwa kasi si viongozi watakaokamatwa, bali wao ndio watakaotiwa mbaroni.

Aliliomba baraza hilo kumshauri mambo kadhaa ikiwamo adhabu zinazotokana na makosa ya usalama barabarani.

Pia aliomba ushauri kuhusu madereva wa bodaboda akisema katika nchi nyingine pikipiki hizo hufunga matela ili kuongeza idadi ya abiria.

“Tatizo kubwa ni kuwa bodaboda (nchini) hubeba watu wengi (mishikaki) na hicho ndicho chanzo cha ajali hizo,” alisema huku akishauri kuwa ufungaji wa tela husaidia kupunguza ajali.

“Nimeshuhudia kuwa pikipiki ni tatizo kubwa, hawaheshimu trafiki,” alisema.

Aliliomba baraza hilo kumshauri kuhusu uanzishwaji wa vituo vya ukaguzi wa magari kwa sababu sheria inasema mkaguzi ni lazima atangazwe na waziri kwenye gazeti la Serikali.

“Lakini katika nchi nyingine, mkaguzi anatoka katika sekta nyingine,” alisema.

Mjumbe wa baraza hilo, Hamza Kasongo alisema litaanza kufanyia kazi mapema suala la magari ya viongozi wa Serikali.

Ajali nyingine

Ajali nyingine za hivi karibuni ni pamoja na ile ya Julai 14, ambapo gari la Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu lilipata ajali likiwa limebeba madiwani, mkurugenzi na mwenyekiti wa halmashauri. Ajali hiyo ilisababisha vifo vya diwani mmoja na dereva. Tukio jingine lilitokea Mei 21, ambapo maofisa watatu wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), walifariki dunia katika ajali ya gari eneo la Mtelela, Barabara ya Msolwa - Chalinze mkoani Pwani wakiwa njiani kwenda Dodoma kikazi. Waliofariki katika ajali hiyo ni Saidi Amiri, Zacharia Kingu na Martin Masalu.

Ajali hiyo ilihusisha gari ya Serikali aina ya Toyota Land Cruiser lililogonga Scania.

Juni 10, madiwani saba kati ya 11 walijeruhiwa katika ajali kwenye msafara wa mwenyekiti wa UVCCM, Kheri James.

Machi 29, gari likiwa na wabunge sita lilipata ajali mkoani Morogoro wakati likitokea Dodoma kuelekea Dar es Salaam. Ingawa hakukuwa na kifo, lakini majeruhi waliripotiwa.

Wakati huohuo, jana basi la Modern Coach lilipata ajali na kusababisha vifo vya watu wawili na wengine 10 kujeruhiwa. Basi hilo lililokuwa likitokea Nairobi kwenda Dar es Salaam lilipata ajali mkoani Pwani.