Mbinu za kukuza uwezo wa akili wa mtoto

Muktasari:

  • Lakini kadri utaalam wa kupima utendaji wa ubongo ulivyoendelea kuongezeka, sasa tunaelewa akili za binadamu zinaweza kubadilishwa na mazingira anayokutana nayo mtu.

Kwa muda mrefu wataalam wengi wa saikolojia ya elimu waliamini uwezo wa akili anaokuwa nao mtu unarithiwa na haubadiliki. Katika kuthibitisha kuwa akili za mtu haziwezi kubadilika, wapo wataalam, tena wengi tu, waliobuni kipimo cha akili za mtu kilichojulikana kama IQ. Kipimo hiki kilitumia mfululizo wa maswali anayoulizwa mtu kujua anawezaje kufikiri, kuelewa na kuchambua mambo.

Lakini kadri utaalam wa kupima utendaji wa ubongo ulivyoendelea kuongezeka, sasa tunaelewa akili za binadamu zinaweza kubadilishwa na mazingira anayokutana nayo mtu.

Mtazamo huu mpya unatupa faida mbili kubwa. Kwanza, unatusaidia kujua mambo yanayoweza kufanyika kubadili uwezo wa akili anazokuwa nazo mtu. Pili, unaongeza wajibu tulionao sisi kama wazazi katika kumwekea mtoto mazingira sahihi yanayoweza kusisimua utendaji wa ubongo wake.

Katika makala haya tutazame mambo manne unayoweza kuyafanya kukuza uwezo wa mtoto kufikiri, kuelewa na kuhambua mambo.

Badili lugha anayojisemea mtoto

Kila mtu anayo lugha ya ndani anayoitumia kufikiri. Lugha hii ya ndani ina kazi kubwa ya kujenga vile unavyojichukulia. Unapofikiri jambo, kwa mfano, unaweza kusema maneno fulani yanayokuhamasisha, kukusifu, kukukosoa, kukutia wasiwasi, mashaka na hata kukukatisha tamaa.

Wataalam wanasema kuna uhusiano mkubwa kati ya mawazo ya mtu na kile anachokifanya. Kama mtoto, kwa mfano, atayaamini mawazo yanayomvunja moyo, matokeo yake yatakuwa ni kushindwa. Mtoto mwenye mawazo yanayomnyong’onyeza hawezi kuzidi mawazo hayo. Kukata tamaa, kujizomea, kujikosea kulikopitiliza, kunamnyima fursa ya kufikiri sawa sawa.

Mzazi jenga mazoea ya kumsemea mwanao maneno yanayomjenga. Tambua mazuri anayoyafanya na yaseme maneno chanya. Usiwe na tabia ya kumkosoa mno mtoto hata kama kweli hajafanya vizuri.

Fikiria mtoto amefanya vibaya darasani. Mzazi wa kwanza anamwambia, “Nikijua tu utafeli. Kwanza huna akili. Naona napoteza tu hela kukusomesha.”

Mzazi wa pili anamwambia, “Kwa namna ninavyokufahamu, uwezo wako ni mkubwa. Najua ukikazana, ukimsikiliza mwalimu na kujisomea, uwezo wa kufanya bidii kufikia uwezo wako halisi.”

Mzazi wa kwanza anaongea kwa hasira shauri ya matajiro makubwa aliyonayo kwa mwanae. Hachagui maneno ya kumwambia mwanae kwa sababu anaamini kufeli mtihani ni kukosa akili. Hajua athari ya maneno yake katika kujenga lugha ya ndani itakayoathiri uwezo wake wa kujituma.

Mzazi wa pili anaweza kuwa na hasira lakini anajua nguvu ya maneno yake. Anamtamkia mtoto maneno yanayomtia hamasa hata katika kufeli kwake. Maneno haya chanya yatajenga lugha chanya itakayokuwa hamasa ya kufanya vizuri zaidi.

Ongeza fursa za mawasiliano

Mazungumzo yana nafasi kubwa ya kuongeza uwezo wa akili anaokuwa nao mtu. Kuzungumza na mwanao mara kwa mara kunakuza uwezo wake wa lugha, msamiati wake, na hata kusisimua utendaji wa ubongo wake.

Unaweza kushangaa lakini ndivyo wataalam wanavyotuambia. Wazazi waongeaji wenye tabia ya kuzungumza na watoto huwasaidia kuwa na msamiati zaidi.

Lugha ina nafasi kubwa katika kujenga uwezo wa akili.

Bila kujali umri wake, jenga mazoea ya kujadiliana na wanao masuala mbalimbali yanayohusu maisha yao. Wape nafasi ya kukusimulia yale wanayokutana nayo shuleni, kwenye michezo, mambo wanayoyasikia mitaani, matarajio waliyonayo na hata hofu wanazohitaji kupambana nazo. Fanya mazungumzo yawe utaratibu wa kawaida wa maisha ya hapo nyumbani.

Mfano, mwombe mwanao akuambie siku yake imekwendaje. Mwuulize maswali yanayomtaka ajieleze badala ya kujibu kirahisi ‘ndiyo’, ‘hapana’ na ‘sijui.’ Mruhusu mtoto akuulize maswali na jitahidi kuyajibu kadri unavyoweza.

Mara nyingi mtoto huuliza kutaka kuyaelewa mazingira yake, kuelewa mambo anayoyaona na kukutana nayo katika maisha. Kumbuka muhimu hapa sio majibu unayompa, bali uwezo wa kufikiri, kuelewa, na kuchambua mambo anayoyasikia.

Simulia hadithi

Tangu zamani utamaduni wetu ulitambua umuhimu wa masimulizi kwa watoto. Nyakati za jioni, wazazi walikuwa na utaratibu wa kukaa na watoto wao na kuwasimulia hadithi mbalimbali.

Hadithi hizi, mbali na kukuza ukaribu baina ya wazazi na watoto wao, zilikuza uwezo wa watoto kufikiri. Hadithi, mathalani, zinatumia wahusika wenye tabia na mikakati tofauti kwa kutumia madhari ya kufikirika. Haya yote humfanya mtoto alinganisha anayoyasikia na maisha yake ya kila siku.

Siku hizi desturi hii, hata hivyo, imeanza kupungua. Watoto wanatumia muda mwingi kufanya kazi za kitaaluma ambazo mara nyingine hazihusiani na maisha yao ya kila siku. Mbali na kufifiisha uwezo wao wa kuyaelewa mazingira yao, kazi hizi nyingi zinafunga fikra zao kwenye mambo fulani pekee.

Tunahitaji kufufua desturi ya hadithi kwa watoto. Mbali na kuwasimulia, tuwape nafasi wao wenyewe wabuni hadithi kuwasaidia kujua kuchagua wahusika, kupangilia matukio na kusema wanachokifikiri.

Hamasisha usomaji wa vitabu

Sambamba na masimulizi, mzazi una fursa ya kumhamasisha mtoto kusoma vitabu. Unaweza kuanza kwa kumsomea kitabu chenye hadithi zinazogusa mambo anayokutana nayo kwenye maisha.

Usomaji wa vitabu kwa watoto si tu unaimarisha uhusiano wenu, lakini unaongeza kumbukumbu, uzingativu na hata kukuza msamiati.

Hata hivyo, ni muhimu kuzingatia kuwa huwezi kukuza tabia fulani kwa mtoto kama wewe mwenyewe huna. Lazima kwanza uanze wewe mwenyewe kupenda kusoma ili mwanao ajifunze.

Swali kwako mzazi, kwa mwaka 2017 ulisoma vitabu vingapi? Je, uliwahi kuonekana ukisoma hapo nyumbani au muda mwingi unautumia kutazama televisheni na kutumia simu?

Je, kuna vitabu vinaonekana kwenye mazingira ya nyumbani?

Lenga kumfundisha mwanao kwa vitendo. Onekana ukisoma ukiwa nyumbani. Kama huna vitabu au magazeti, unavyo vitabu vya dini. Anza na hivyo.

Pia, mnunulie vitabu kama zawadi yake na msomee nyakati za jioni anapojiandaa kulala. Watoto wanapenda sana fursa kama hizi. Kila inapowezekana, mpeleke kwenye maduka ya vitabu na maktaba kupanda mbegu ya mtoto kuwa na urafiki wa kudumu na maandishi.

INAENDELEA WIKI IJAYO

Blogu: http://bwaya.blogspot.com