Mfupa mgumu kwa Lampard Chelsea FC huu hapa

Maurizio Sarri ametua Juventus ‘Kibibi Kizee’ cha Turin akitokea Chelsea baada ya kuinoa kwa msimu mmoja tu, sasa anarejea katika Ligi Kuu ya Italia akienda kuvaa viatu vya Maximilliano Alegri.

Tangu Sarri alivyoweka bayana dhamira yake ya kutua Juventus, majina mengi yaliyochoza nani atakuwa mrithi wake kwa mashindano ya msimu ujao hasa ikizingatiwa timu hiyo itashiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Baadhi ya majina makubwa katika soka yaliyochomoza ni pamoja na kocha wa zamani wa timu hiyo Jose Mourinho ambaye alinogesha Ligi Kuu England kwa tambo zake.

Lakini, pamoja na tetesi kuenea kila kona ya dunia, bilionea wa Chelsea Roman Abramovich, ameelekeza macho yake kwa nyota wa zamani wa timu hiyo Frank Lampard.

Baada ya kucheza kwa kiwango bora akiwa mmoja wa wachezaji wa nafasi ya kiungo, Lampard anaweza kurejea nyumbani akiwa kocha mkuu kujaza nafasi ya Sarri endapo pande mbili zitafikia makubaliano.

Lampard sasa amekomaa katika benchi la ufundi, baada ya kuiongoza Derby County kupata mafanikio katika Ligi Daraja la Kwanza. Timu hiyo ilikaribia kupanda Ligi Kuu kabla ya kuzidiwa kete na Aston Villa katika mechi ya fainali ilipofungwa mabao 2-1.

Lampard anaweza kuwa kocha wa 13 chini ya Abramovich na haitashangaza hata yeye akitupiwa virago kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake.

Lampard anakwenda Chelsea akitambua kuwa hana mamlaka ya kusajili mchezaji yeyote katika msimu wake wa kwanza kutokana na kibano ilichopata klabu hiyo kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Endapo atapewa kibarua hicho kizito, Lampard atakabiliwa na mambo makubwa matatu ambayo kama atachanga vyema karata zake anaweza kuvuka kiunzi hicho vinginevyo atakwaa kisiki.

Mambo matatu yanayomkabili Lampard ni kujenga kikosi imara hasa ikizingatiwa atakuwa hana mamlaka ya kufanya usajili, kupangua kikosi ambacho kinaonekana kusheheni idadi kubwa ya wachezaji wenye umri mkubwa akina Olivier Giroud na jambo jingine ni jukumu kubwa alilopewa la kufundisha timu kubwa yenye rekodi bora duniani.

Mazingira magumu ya Chelsea yatamfanya Lampard kubaki na uamuzi mmoja tu wa kugeukia wachezaji chipukizi ili kupata timu ya ushindani msimu ujao.

Hakuna namna Lampard anayetarajiwa kuingia mkataba wa miaka mitatu Chelsea atalazimika kutupia jicho wachezaji chipukizi ingawa atakuwa na machaguo matatu tofauti ya mfumo atakaokutumia msimu ujao.

Hata hivyo, Lampard si mgeni wa kutumia wachezaji chipukizi akiwa Derby alikuwa muumini mkubwa wa kuendeleza vipaji vya wachezaji wenye umri mdogo.

Lampard anajua Chelsea ina hazina ya wachezaji vijana chini ya miaka 81 na 21 ambao anaweza kuwapandika katika kikosi cha kwanza. Mtangulizi wake Sarri anapenda kutumia mfumo wa 4-3-3 aliotumia katika idadi kubwa ya mechi za msimu uliopita.

Lampard anaweza asitumie mfumo huo kulingana na mahitaji yake na huenda akaendeleza mbinu yake akiwa Derby.

Kocha huyo ni mpenzi wa kutumia viungo watatu washambuliaji ambao wamekuwa na nguvu kubwa wanapoingia ndani ya eneo la timu pinzani.

Kurejea kwa kiungo nyota wa Ufaransa, N’Golo Kante katika eneo la kiungo mkabaji, linaweza kuwa na faida kubwa kwa Lampard ambaye ni hodari wa kutoa pasi za mwisho.

Msimu ulipita Lampard alitumia mfumo 4-3-3, lakini anaweza kubadili mbinu kwa kutumia mfumo 4-2-3-1. “Ni jambo jema kuiga mifumo mingine ingawa si lazima,” anasema nguli huyo wa zamani wa England.