NO AGENDA: Hebu kujeni niwaambie mchezaji wa Simba aliyetibua ndoa ya Stamina

Monday January 13 2020

 

By LUQMAN MALOTO

DAKTARI Remmy Ongala alimaliza kesi kuhusu muziki. Mzigo wa mwaka tisini wenye jina “Muziki Asili Yake Nini” unasema yote. Remmy aliimba: “Muziki asili yake wapi? Muziki ni nini? Muziki hakuna mwenyewe. Muziki ni wito. Muziki ni fundisho. Muziki maombolezo, kilio.” Kisha Dk Remmy akatupa siri hii: “Usinione ninaimba, ukadhani ninayo furaha, kumbe ninayo hudhuni moyoni.”

Yes, music can tell anything. Ni mwanamuziki na uwasilishaji wake. Ashindwe yeye tu. Akiamua kuwasilisha michongo ya kula bata au burudani ndani ya mapenzi, hakuna wa kumzuia. Dk Remmy alishamaliza kesi kuwa muziki hauna mwenyewe. RIP Legend Remmy.

Hapangiwi mtu cha kuimba. Muziki ni hisia. Papii Kocha alipotoka jela kwa msamaha wa Rais John Magufuli, alitoa “Waambie” akifikisha ujumbe kuwa wakati wowote Mungu yupo, akiombwa anasikia maana hata yeye alimuomba akasikia. Sasa hapa unataka ufafanuzi upi mwana kama si kuchoshana? Basi bwana, ukubwa jalala, ngoja nikukumbushe; Papii Kocha na baba yake, Nguza Viking ‘Babu Seya’ walipewa msamaha na Rais wakiwa kwenye adhabu ya kifungo cha maisha jela.

Mwaka 2003, Papii, Babu Seya na wanawe wengine Nguza Mbangu na Francis Nguza walitupwa mahabusu kisha wakafikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashitaka ya ubakaji na ulawiti wa watoto wanane. Mwaka 2004 walihukumiwa kifungo cha maisha jela. Mwaka 2005 Mahakama Kuu ikakazia hukumu. Mwaka 2008, Mahakama ya Rufaa iliwaachia Mbangu na Francis.

Muziki ni hisia; Papii baada ya kutoka jela, akaona amtukuze Mungu. Wimbo wa shukrani na hamasa kwa makundi yote kutambua kuwa Mungu anasikia. Ni suala la kumuomba na kuweka matumaini hai.

Nimeusema mwaka 2003 nimemkumbuka Juma Nature na kesi yake dhidi ya aliyekuwa girlfriend wake Sinta. Na hapa tena unataka kukumbushwa? Sinta alikuwa staa bwana! Tusiongee sana, kwa kifupi Sinta ndiye alikuwa mrembo aliyebamba zaidi Bongo mwanzoni mwa miaka ya 2000. Alitikisa kupitia mauzo ya sura Kaole Sanaa Group, runinga ni ITV. Halafu bwana, Nature ndiye alikuwa the real deal kwenye Bongo Fleva. Basi couple la Nature na Sinta ikatikisa nchi wakati huo. Nini kilitokea? Yakatokea manyokanyoka. Nini kikafuata? Ile kesi ya Sinta wala Sir Nature hakutafuta wakili, jaji, hakimu, mwamuzi wala mwenyekiti wa baraza. Aliimaliza mwenyewe kwenye booth ya P Funk, Bongo Records.

Advertisement

Nature akatoa “Sitaki Demu”, akamnanga Sinta, akaona haitoshi, akaipua “Sitaki Demu Remix”. Mfalme wa Temeke hakuridhika akaipua “Inaniuma Sana” halafu baada ya kumchamba sana akamwambia “haya sasa na wewe si msanii, nenda kalipize kwenye TV”. Eti Sinta akalipe kwenye maigizo yake runingani. Dunia haijabadilika sana kutoka mwaka 2003 Nature alipomalizana na Sinta kwenye booth. Stamina na yeye kafanya yake, kaingia booth ya Kiri Records kaachia mzigo “Asiwaze”. Humo ndani Stamina anadhihirisha hasira nyingi. Ni kweli Stamina ni mwenye hasira lakini mbona kama zimezidi kipimo? Yaani kweli hajui uhusiano na aliyekuwa mke wake ulikuwa unahusiana na nini? Kweli, akifa mkewe asifike msibani na akienda atafufuka ampige vibao? Aah, mbona mbali sana?

In short, Stamina ameimaliza kesi kibabe sana. Anaponda kila kitu kilichofanyika kufunga ile ndoa na mkewe. Anauliza ile suti alivaa ya nini? Michango ya harusi alichangisha ya nini? Ndugu nao aliwaita wa nini wamsadie safari ya kufunga ndoa? Na kiapo sasa aliapa kwa nini?

Kila kitu kuhusu ndoa yake anakiona najisi. Anauliza ile keki alikata ya nini na kulishana na mkewe? Na mahari alilipa kwa nini? Mshenga naye alimtuma wa nini?

Nini ambacho hajaacha kulaumu? Hata wasimamizi wa ndoa amewaambia walipoteza muda wao wa bure, kwani muda walioutumia kusimamia ndoa yake bora wangeutumia kujenga familia zao. Padri na waimba kwaya nao anawasikitikia.

Pitia lyrics, mstari kwa mstari. Kuna ile laini anachana “hiki cheti cha ndoa nimebaki nacho kwa nini, siwezi kuombea kazi, hakina mchongo hapa mjini.”

Dakika nne na sekunde 49 za “Asiwaze” zinatuma ujumbe kutoka kwa Stamina kuwa hakuna uamuzi wa hovyo ambao amewahi kuufanya kama ule wa kumuoa mke wake. Na hakuna ndoa ya hovyo kuwahi kufungwa kama ya kwake. Achana na stori zake kuhusu mambo ya eti mwanaume mpaka mkorogo anaweza kumridhisha mke wa mpaka vumbi la Mkongo, hizo ni punchline tu! Tunene kile chenye uwezo wa kudhibiti presha ya maji. Ni hivi, aliyesababisha yote hayo ni mchezaji wa Simba.

Sema Stamina sometime hasomeki. Maeneo yote kagusa moja kwa moja, lakini kwenye jina la mchezaji wa Simba amemyuti. Matokeo yake mitaani kuna msako mkubwa unaendelea wa kumtafuta huyo aliyeingiza purukushani kwenye ndoa ya Stamina.

Kuna watu wameingia chomboni mpaka Zanzibar, eti waende kwenye kambi ya Simba, wapate kumjua huyo mchezaji aliyefanya ndoa ya Stamina ivunjike.

Yote hayo sababu ni Stamina kuficha jina la mhusika. Ngoja sasa niwarahishie. Rudia laini ya Stamina: “Mwambieni yule dogo aliyechezea klabu ya Simba, kutembea na mke wangu asijione ameshinda. Mimi samaki mapenzi yangu yana shombo, kaka yake nilishakula ruksa kutoa vyombo.”

Ujumbe wa Stamina unaonyesha kuwa huyo dogo aliyepeleka sokomoko kwenye ndoa ya memba wa Rostam alikuwa mchezaji wa Simba, lakini sasa hayupo kwenye klabu hiyo. Rudia mstari “mwambieni yule dogo aliyechezea klabu ya Simba”. Aliyechezea ni kitenzi chenye kuashiria wakati uliopita.

Tumejua ni mchezaji aliyeondoka Simba, sasa tuanze kuulizana. Nani na nani waliachwa Simba msimu uliopita? Tukokotoe zaidi, Stamina amesema ni dogo. Chukua umri wa Stamina halafu angalia walioachwa Simba mwaka jana, nani dogo kwa Stamina?

Haruna Niyonzima, James Kotei, Emmanuel Okwi, Deogratius Munishi ‘Dida’, hao si madogo kwa Stamina. Sasa ni nani? Tafuta sasa dogo aliyeachwa Simba. Utamjua tu. Hata ambao wametolewa kwa mkopo. Tafuta. Ndiye yeye!

Wakati unatafuta jina la mchezaji nikupe burudani ya kiitikio cha Asiwaze, kimeimbwa na Atan: “Naubembeleza upepo usizime kibatari (Asiwaze), kichwani kwangu hayumo moyoni nipo shwari (Asiwaze), kwangu hajaacha pengo mwambie (Asiwaze), huko alipo atulie (Asiwaze), kama amepoteza lengo mwambie (Asiwaze), huko alipo atulie (Asiwaze).

Mwisho mwambieni Stamina aache dharau; kafunga ndoa ambayo imeishi siku 379 tu, halafu anatamba eti mambo ya ndoa aulizwe yeye.

. Bado hajui chochote kuhusu ndoa. Na mimi namwambie, Asiwaze!

Advertisement