Ni mwaka wa BurnaBoy, awakalisha chini Wizkid, Davido

Monday November 25 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi

Unaweza kuuita ni mwaka wa bahati wa msanii kutoka nchini Nigeria, Damini Ebunoluwa Ogulu maarufu kwa jina la  Burna Boy.

Hii ni baada ya kushinda tuzo mbalimbali kubwa mwaka huu ikiwamo ya African Muzik Magazine Awards (Afrimma) na All Africa Muzik Awards(Afrima).

Sambamba na hilo, amekuwa miongoni mwa wasanii kutoka barani Afrika kuingia kwenye tuzo kubwa duniani za muziki za Grammy zinazotarajiwa kutolewa Januari mwakani, nchini Marekani.

Katika tuzo hizo ambazo Burna Boy ameingia katika kipengele cha World Best Music Album, kupitia albamu yake ya nne aliyoipa jina la African Giant yenye nyimbo kali ikiwamo ya ‘On The Low’ na ‘Gbona’.

Katika tuzo za AFRIMMA zilizofanyika Oktoba 28, 2019, Burna Boy alishinda tuzo nne ikiwamo ya wimbo bora wa kushirikiana na Wimbo wa mwaka kupitia wimbo wa Killing Dem alioimba na msanii Zlata, kipengele ambacho mwaka jana alishinda msanii Wizkid kutoka Nigeria na wimbo wake wa ‘Soco’.

Pia, alishinda kipengele cha Msanii wa mwaka na msanii bora wa kiume Afrika Magharibi, kipengele ambacho mwaka jana alishinda msanii wa Nigeria Davido.

Advertisement

Wakati katika tuzo za Afrima zilizotolewa Novemba 23, 2019, Burna ameshinda kipengele cha msanii bora wa kiume Afrika Magharibi kupitia wimbo wa ‘Ye’, kipengele ambacho mwaka jana alishinda Davido, Msanii wa mwaka Afrika kupitia wimbo wake wa Gbona kipengele ambacho mwaka jana alishinda pia Davido.

Burna Boy mwenye miaka 28 ambaye ni mwimbaji na mtunzi, jina lake lilipata umaarufu pale alipoachia kibao chake cha kwanza mwaka 2012 alichokipa jina la “Like to Party” katika albamu yake ya kwanza ya L.I.F.E.

Advertisement