Wasanii Tanzania walivyoshindwa tuzo za Soundcity MVP, Burna Boy atikisa

Muktasari:

  • Tuzo za Soundcity MVP zimefanyika  usiku  wa kuamkia leo Jumapili Januari 12, 2020 nchini Nigeria huku wasanii kutoka Tanzania wakishindwa kufanya vizuri katika tuzo ambapo wamekosa tuzo hata moja na msanii wa Nigeria Burna Boy akinyakua tuzo tatu.

Wasanii kutoka Tanzania wameshindwa kufanya vizuri katika tuzo za Soundcity MVP zilizofanyika ukumbi wa Eko Convention Centre jijini Lagos nchini  Nigeria na kushuhudiwa wasanii wa Tanzania wakitoka bila kupata tuzo hata moja.

Tuzo hizo ambazo ni za kwanza kufungua mwaka 2020 nchini Nigeria, ziliwashirikisha  wasanii mbalimbali kutoka Afrika ambapo vipengele 15 viliwaniwa.

Pamoja na kusubiriwa kwa hamu kuona kama wasanii wa Tanzania wanaofanya vizuri kwa sasa Diamond Platnumz na Harmonize watanyakua tuzo hizo hali haikuwa hivyo na kujikuta wakitoka kapa.

Washindi katika tuzo hizo ni pamoja na Burnaboy ambaye ameshinda tuzo tatu ya msanii bora wa kiume (Best Male MVP), msanii bora Afrika na wimbo bora wa mwaka.

Washindi wengine ni Rema aliyeshinda msanii mpya, Gugulethu wimbo bora wa kushirikiana, JoeBoy msanii bora wa Pop, KHALIGRAPH Jones msanii bora wa HipHop na msanii DopeNation.

Wengine ni Rexxie ambaye ameshinda kipengele cha mtayarishaji bora wa mwaka, Teni (NG) msanii bora wa kike, DJ Spinall Dj bora wa mwaka, Davido Msanii bora wa Digital, Jealous – Fireboy DML, Soapy – Naira Marley, Pamoja na  Tiwa Savage aliyeshinda kipengele cha Video bora ya mwaka.

Katika tuzo hizo, Msanii Diamond alikuwa anawania vipengele  vitatu  ikiwamo msanii bora wa Afrika, msanii wa kidigitali na msanii bora wa kiume.

Pia staa huyo wa kibao ‘Baba lao’ alitajwa kuwania kipengele cha chaguo la msikilizaji, kupitia wimbo wa ‘Kainama’ alioimba kwa kushirikiana na msanii Harmonize na Burna Boy.

Wasanii wengine wa Tanzania waliokuwa wanawania tuzo hizo ni Rayvanny na Nandy katika kipengele cha msanii bora wa Pop na mtengenezaji wa muziki S2Kizzy katika kipengele cha mtengenezaji bora wa muziki na msanii Marioo katika kipengele cha msanii mpya,

Kama vile haitoshi wimbo wa ‘Tetema’ alioimba Rayvanny kwa kumshirikisha Diamond ulitajwa katika vipengele viwili ikiwamo wimbo wa mwaka na chaguo la watazamaji.