Wema: Kilo 109 zilinitesa

Friday February 21 2020

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mlimbwende wa Tanzania mwaka 2006, Wema Sepetu amesema wakati ana umbo kubwa alikuwa na kilo 109, kubainisha kuwa hakuwa vizuri kiafya na lilimfanya asiwe huru.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Februari 21,2020 katika hafla ya kuingia mkataba na kiwanda cha rasta cha Angel kuwa balozi wa bidhaa zao.

Pamoja na mambo mengine waandishi walitaka kujua kauli yake baada ya kupungua mwili na namna watu wanavyomzungumzia.

Amesema wakati akiwa na kilo 109 alikuwa akijisikia vibaya, alifikia hali hiyo kutokana na kula bila utaratibu.

Amebainisha kuwa baada ya kulitambua hilo, alianza kula kwa mpangilio, kufanya mazoezi na kunywa dawa mbalimbali na kupungua uzito hadi kilo 65.

"Huu mwili ndio niliokuwa nauhitaji, wakati ninashinda taji la Miss Tanzania mwaka 2006 nilikuwa na kilo 55. Kwa kilo zile 109 nilikokuwa naelekea si kuzuri.”

Advertisement

"Nitajitahidi nibaki na wembamba huu kwa kuwa unanipa amani, wembamba raha jamani asikuambie mtu," amesema Wema.

Mlimbwende huyo amesema wapo wanaohusisha wembamba wake na ugonjwa, “siwajali kwani hata nilivyokuwa mnene niliitwa majina mengi kama tembo, nyumba nakadhalika.”

Advertisement