Wema Sepetu, Diamond Platnumz uso kwa uso Dar

Muktasari:

Wasanii Wema Sepetu na Diamond wamekuwa kivutio katika mkutano wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda unaotarajiwa kuanza muda mfupi ujao katika viwanja vya Leaders

Dar es Salaam. Msanii wa Bongo Fleva, Wema Sepetu na Diamond Platnumz leo Alhamisi Januari 31, 2019 wamekuwa kivutio katika viwanja vya Leaders Club ambako mkutano kati ya wasanii na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda unatarajiwa kufanyika.

Diamond amewasili viwanja hivyo  majira ya saa 9:15 alasiri akiwa katika gari jeusi aina ya BMW X6 huku akiwa amevalia  kanzu nyeupe na kilemba.

Akiwa amesindikizwa na walinzi wake, Diamond alipofika alielekea kushoto mwa jukwaa na kusalimia baadhi ya  wasanii kabla ya kuelekea jukwaa kuu ambapo Wema na wasanii wengine walikuwa wamekaa.

Alianza kumsalimia ofisa habari wa klabu ya Simba Haji Manara , meneja wake Babu Tale na kisha kumkumbatia mrembo huyo kwa takribani dakika moja kabla hajaenda kusalimia wasanii wengine akiwemo King Kikii, Masanja Mkandamizaji na wengine.

Tukio hilo lilionekana kuwavutia watu waliofika katika viwanja hivyo wakiwemo waandishi wa habari ambao kila mmoja alikuwa akipambana kupata picha.