Baraza la Kijeshi Sudan lazima jaribio la mapinduzi

Baraza la Kijeshi nchini Sudan  limesema kuwa limezima jaribio la mapinduzi na linawashikiliwa wanajeshi 16 waliohusika na tukio hilo.

Madai hayo yamekuja wakati baraza hilo pamoja na viongozi wa waandamanaji wanaoshikiza utawala wa kiraia wakiwa katika mazungumzo ya jinsi ya kugawana madaraka.

“Maofisa na wanajeshi katika Jeshi la Sudan pamoja na maofisa wa usalama, baadhi wakiwa wamestaafu, walikuwa wanajaribu mapinduzi,” alisema kiongozi wa Baraza hilo, Jenerali Jamal Omar moja kwa moja kupitia televisheni ya Taifa.

“Vikosi vyetu vimeweza kuzuia jaribio hilo,” alisema lakini hakutaja ni lini jaribio hilo lilifanyika

Omar alisema hilo ni jaribio la kuzia makubaliano yaliyofikiwa kati ya baraza hilo na waandamanaji ya kugawana madaraka na kutekeleza matakwa ya raia wa Sudan.

Makundi hayo sasa yanaendelea na majadiliano ya kina katika hoteli moja jijini Khartoum

Omar alisema vikosi vya serikali vilikuwa vinawasaka maofisa wengine zaidi waliohusika na jaribio hilo, kwa mujibu wa al Jazeera.

Wiki iliyopita, viongozi wa baraza la kijeshi na wale wa waandamanaji walikubaliana kuunda kamati huru ya pamoja  ya kuongoza nchi hiyo kwa miaka mitatu wakati uchaguzi unaandaliwa.

Makundi hayo yanakubaliana na kuwa njia ya kidiplomasia ndiyo njia pekee ya kumaliza sintofahamu inayoendelea katika nchi hiyo.

Jaribio la mapinduzi linaelezwa na wachambuzi wa masuala ya Sudan waliohojiwa na al-jazeera kuwa “si la kushangaza sana”, kwa kuwa yapo makundi yasiyokubaliana na hatia iliyofikia katika majadiliano kati ya jeshi na raia.

Sudan imekuwa katika mvutano tangu Aprili Jeshi la nchi hiyo lilipoamua kumwondoa madarakani Rais Omar al-Bashir aliyedumu madarakani kwa miaka 30 kwa mkono wa chuma.

Jeshi lilichukua hatua hiyo kufuatia maandamano yasiyokoma kwa miezi kadhaa kupinga ongezeko la bei ya mkate na hali ngumu ya maisha, na hivyo kumtaka Bashir aliyeingia madarakani kwa mapinduzi, ang’oke.